Utesaji wasaidizi wa nyumbani ukomeshwe

16Jul 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Utesaji wasaidizi wa nyumbani ukomeshwe

ONGEZEKO la unyanyasaji wa wasaidizi wa kazi wa nyumbani linalalamikiwa na watu wengi kutokana na wengi wao kupigwa na kunyimwa chakula.

Wengi wa wasaidizi hao, huchukuliwa kwa wazazi wao wakiwa na umri mdogo na wanapofika kwenye nyumba za mabosi wanaowachukua, hufanyishwa kazi nyingi kuliko uwezo wao.

Matukio ya kunyanyaswa kwa watoto wanaofanya kazi za ndani yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari na baadhi ya watoto hao hubaki na vilema vya maisha.

Wazazi wa watoto hao wengi huwatoa watoto wao kwenda kufanyakazi kwa malengo ya kusaidiwa kimaisha kutokana na kuishi katika hali duni.

Baadhi ya watu wanaokwenda kuwachukua (wengi wakiwa mawakala), huwadanganya wazazi wa watoto hao kuwa wanawachukua watoto hao kwenda kuwatafutia kazi za kuuza duka au kuwasomesha, lakini wanapofika mjini hujikuta katika hali ya kufanyishwa kazi ngumu.

Wengi watoto wanaochukuliwa ni kati ya umri wa miaka 12 hadi 15, ambao wamehitimu darasa la saba na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya wazazi kukosa fedha za kuwanunulia mahitaji watoto wao.

Hata hivyo, watoto hao wanapofika kwenye nyumba za mabosi wao hujikuta katika mazingira magumu, wengine wakilazwa kwenye stoo za kuhifadhiwa vyakula, au jikoni bila kitanda au godoro.

Mtoto huyo huwa wa kwanza kuamshwa ili kuwatayarisha watoto wa bosi kwenda shule na kuwaandalia kifungua kinywa.
Akishamaliza kazi hiyo, atapangiwa kufanya usafi wa nyumba na kufua nguo ambazo zingine hazipaswi kufuliwa na mtoto kama huyo.

Anaweza kufanyishwa kazi hizo bila kuachiwa chakula na kuambiwa mpaka mabosi wake watakaporudi na akiwaandalia chakula, basi yeye atapewa kile kilichobaki.

Wengi wa watoto hao wanaposhindwa kutimiza kazi walizopangiwa huishia kupata vipigo ambavyo wengine huwaacha na vile vya maisha.

Wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakipinga vitendo hivi kwa kutoa elimu kupitia njia mbalimbali ili jamii ipate uelewa pale inapoona jirani au ndugu anayewafanyia unyama watoto wanaowasaidia kazi za ndani kutoa ripoti kwenye vyombo husika.

Hatahivyo, kuna baadhi ya watu wanaoshuhudia vitendo hivyo, lakini wanashindwa kutoa taarifa kwa kuhofia kuonekana mbaya mbele ya jirani au ndugu yake hasa pale anapochukuliwa hatua za kisheria kwa kufikishwa mahakamani au kupata kifungo.

Wazazi pia hupatiwa elimu ya kutoruhusu watoto wao kuchukuliwa na watu bila kuwa na uhakika watoto wao wanakwenda kufanyishwa gani gani.

Baadhi ya watoto huokolewa na wasamaria wema pale wanapoona mateso yakiongezeka ambayo yanaweza kumsababishia mtoto kupoteza maisha au kumuathiri kisaikolojia.

Kuna kesi nyingi zimekuwa zikiripotiwa za wasaidizi wa ndani kuwanyanyasa watoto wa mabosi wao na uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya vitendo hivyo vinatokana na hasira za wasaidizi wa ndani kunyanyaswa na mabosi wao kuwalipiza watoto hao.

Ingawa mtoto hutumika kama chambo cha kuwakomesha mabosi, lakini kama wasaidizi hao wa ndani wangekuwa wanalelewa kwa upendo kama wanaoonyeshwa watoto wao wa kuwazaa, matatizo haya yasingekuwapo.

Hakuna mtu anayependa kumtoa mtoto wake akafanye kazi za ndani, wazazi /walezi wenye kufanya hivyo ni wale ambao hali yao ya maisha imewalazimu kufanya hivyo.

Sio mabosi wote wenye tabia ya kunyanyasa wasaidizi wa ndani, kuna baadhi huishi nao vizuri na kuwafanya kama ndugu zao hata kufikia hatua ya kuwaendeleza kimasomo.

Wahenga walisema mtoto wa mwenzako ni wa kwako, unapomfanyia unyama mtoto wa mwenzako kumbuka kuna siku yatakuja kukuta na wewe.

[email protected]; Simu: 0774 466 571