Uuzaji barakoa kwa mtindo 'sagurasagura' si salama

08May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uuzaji barakoa kwa mtindo 'sagurasagura' si salama

HII ndiyo hali halisi iliyopo sasa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, hasa kwenye vituo vya mabasi vikiwamo vya daladala. Ni hali gani hiyo? Mauzo ya barakoa yanazidi kushamiri.

Utakuta wake kwa waume na makudi ya vijana, wanaranda kila upande wameshikilia lundo la barakoa, wengine wamezipanga kwenye meza kutangaza biashara hiyo inayozidi kupata umaarufu sio katika jiji hili, bali kwingi.

Imekuwa maarufu karibu kila kona, hasa wakati huu ambao nchi inapambana dhidi ya maambukizo ya virusi vya corona, ambavyo ni tishio kwa dunia.

Barakoa zinauzwa kwa lengo la kuwakinga watu dhidi ya maambukizo ya virusi hivyo wakati wa kuongea, kupiga chafya na kukohoa. Pia, inazuia mate na majimaji kutoka kinywani au puani kuwarukia wengine.

Katika kukabiliana na gonjwa hilo, Watanzania wameelekezwa kutumia vifaa hivyo, kama njia mojawapo ya kuepuka maambukizo na sasa baadhi ya watu wamegeukia biashara ya kushona na kuziuza.

Hali ya sasa katika biashara hiyo, kuna hitaji la elimu ya haraka kwa umma, kwani ikiachwa kiholela kuna hatari ya kuchangia kuenea kwa virusi hivyo, badala ya kupunguza maambukizo, kama inavyokusudiwa.

Mauzo ya barakoa kwa sasa yanafanywa katika mtindo unaofanana sana na uuzaji wa nguo za mitumba, ambazo wateja wake huchagua nguo anayokusudia, anajipima na kisha anafikia uamuzi wa ama kununua au la. Jina la hilo kwa ufupi ni 'sagurasagura'.

Yaani, mteja anafika kwa muuzaji wa barakoa na anachambua hata kufikia kile akipendacho, kwa mtindo uleule wa biashara ya nguo anakisaka akipendacho.

Msingi wa mazingira ya namna hiyo si salama katika kukabiliana na virusi vya corona, kwani yanaweza kuongeza maambukizo kama wauzaji na wateja wao hawatachukua tahadhari zinazotakiwa.

Kwa mtindo huo wa wauzaji kuruhusu wateja kujaribu kuvaa barakoa kabla ya kuzinunua, ni wazi kwamba kuna hatari ya wateja wao kujikuta wakiambukizwa kwa kutojua au wakiwa wanajua.

Mtu anaweza kuwa tayari ameambukizwa na akaenda kujaribu kujipima barakoa, hali inayoweza kuwa chanzo cha kuacha virusi kwa muuzaji na hata wateja wengine.

Tahadhari zilishachukuliwa, ikiwamo kuzuia mikusanyiko mikubwa katika maeneo mbalimbali, kuliko zilizozoeleka katika maeneo kama maeneo ya ibada na sokoni.

Inashauriwa, zama zilizopo siyo za kuuza barakoa wala kununua kwa mtindo wa 'sagurasagura,' kwani inaweza kusababisha maambukizo kuendelea kuwapo nchini.

Hata wauzaji wanaopanga barakoa kwenye meza huku zikipigwa na vumbi huku wateja nao wakishika moja baada ya nyingine, inaweza kuwa na mwendelezo wa kusambaa maambukizo ya maradhi hayo.

Baadhi ya mafundi wa kushona nguo, kwa sasa wamejikita kushona barakoa, kwa sababu ndiyo biashara msimu huu wa corona, lakini wanaozinunua kwa jumla na kwenda kuuza mitani wawe makini.

Zipo barakoa za kuanzia bei ya Sh. 500 na kuendelea, zinazouzwa maeneo mbalimbali na kwenye mikusanyiko ya watu wengi vikiwamo vituo vya daladala, lakini tatizo ni baadhi ya wauzaji na wateja kutozingatia afya.

Kila mmoja atambue kuwa kuuza barakoa kwa mtindo wa 'sagurasagura' si salama kabisa, kinachotakiwa ni pande zote mbili kuchukua tahadhari katika biashara hiyo inayoendelea kupata umaarufu.

Pamoja na hayo, ni vyema pia mamlaka husika kutoa malekezo yatakayosaidia kuwafanya wauza barakoa na wateja wao kutambua kuwa uuzaji na ununuaji wa vifaa hivyo haufanani na biashara ya nguo za mitumba.

Hapa umakini mkubwa unahitajika kwa ajili ya usalama wa wauzaji na wateja wao hasa kutokana na ukweli mdomo, macho pia ni viungo vinavyotajwa kuwa na uwezekano wa kupitisha virusi hivyo.

Ni bahati mbaya baadhi ya wateja wamekuwa wakichagua barakoa na kujaribu kuzivaa na kuacha, kwa lengo la kutaka kupata zile zinazowafaa, lakini inasemekana mtindo huo si salama kiafya.