Uvutaji sigara ulivyonitesa - 2

08Jan 2017
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Uvutaji sigara ulivyonitesa - 2

MPENZI msomaji, wiki iliyopita tulimsikia jinsi Bi. Jane Mwisenge, raia wa Burundi alivyotoa ushuhuda wake wa uvutaji sigara kupindukia. Alianza na vipisi viwili vilivyoisha vya sigara, akajikuta anamaliza sigara pakiti 20 ndani ya wiki mbili!

Tatizo hili linawatesa watu wengi, lakini hawajui wafanyeje ili waweze kuondokana nalo hasa linapokuwa chronic (sugu). Wengine huona ni kawaida, kumbe iko nguvu nyuma ya tatizo lolote lile.

Yapo mapepo yasiyoonekana ambayo yamekuwa yakitesa wanadamu pasipo wao kujitambua. Mapepo ni roho asi zisizoonekana ambazo zipo katika ulimwengu wa roho. Lakini roho hizi mtu anaweza kuzishinda kwa imani kupitia maombi.

IMANI imetafsiriwa vema kwenye maandiko ya Mungu. Tazama Biblia Takatifu kitabu cha Waebrania 11:1 Imeandikwa; “basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.

Yapo mambo yanayotutesa, lakini hatuyaoni kwa macho ya kimwili. Lakini ukiamini kwa kuomba, Mungu anasikia na anakujibu. Anasema; Hata sasa hamkuomba, ombeni lolote kwa jina langu, nitawapa, ili furaha yenu iwe timilifu.

Binti huyo baada ya kuteswa na sigara tangu mwaka 2006 alipoanza kuvuta akiwa darasa la sita, alikubali ushauri wa watu wamchao Mungu kwamba endapo atakwenda kanisani na kuomba kwa bidii, tatizo hilo litakuwa historia katika maisha yake, yaani litakwisha kabisa. Na ndivyo ilivyotokea kwake na sasa yuko huru havuti tena.

Mpenzi msomaji, hebu sasa msikie Jane alivyotii sauti zilizokuwa zinamshauri aende kanisani ili kujua chanzo cha tatizo lake, na, hatimaye apone.

Anasema: Nikiwa hapa Dar nililetwa kanisani na jamaa yangu. Nilikuwa nasita na bado nilikuwa navuta sigara kabla ya kuja.
Siku niliyofunguka ilikuwa siku ya Jumatatu (Februari 8, 2016) . Hata hiyo Jumatatu kabla sijaja kanisani nilikuwa nimevuta sigara tatu.

Jumatatu nilikuja hapa nikiwa nimevuta sigara hizo tatu. Nikawa naongea mwenyewe moyoni nikisema mbona wameniombea, lakini sigara siachi? Wakati natoka nyumbani nikawa nasema leo naenda tu mwenyewe lazima niache sigara na ikiwezekana nimfuate mchungaji aniombee.

Wakati natoka nyumbani kuja kanisani nikachukua sigara moja nivute lakini roho ikaniambia niiache kwanza niende kanisani halafu nitaijia baadaye. Nilipofika kanisani nikaenda kwenye darasa la mafundisho lakini moyoni nasema maombi yataanza saa ngapi.

Nikakumbuka darasa la imani hapa kanisani mwalimu alitufundisha kuwa lazima kila kitu tuwe na shauku ya kupona. Baada ya maombi kilichotokea ni kwamba nilipiga magoti nikaomba nikasikia sauti inaniambia niondoke niende nyumbani. Baadaye nikasikia kichwa kinaniuma sana huku kitu kinaniambia niende nyumbani.

Baada ya maombi kichwa kikaendelea kuuma, nikamfuata mwalimu nikamwambia naye akanijibu niendelea kusubiri, lakini nikawa simwelewi. Nikamuuliza tena mama mmoja kuhusu kichwa kuniuma naye akaniambia pia niendelee kusubiri.

Ikabidi nisubirie maombi. Yalipoanza nikaomba, nikaomba, nikajikuta nimeanguka. Ilipofika kipindi cha mahubiri, mchungaji akasema kuhusu mamlaka. Akasema ukitumia mamlaka hakuna kitu kinachoshindikana.

Ndipo nami nikasema; kwa mamlaka ya sasa hivi sigara mimi naacha. Tangu siku hiyo ya Jumatatu, leo ni siku ya sita sijavuta tena sigara(kanisa likalipuka kwa kushangilia kwa ushindi wa nguvu za Mungu!).

Mpenzi msomaji, hakika, ukiwa na shauku ya kupona lazima Mungu atatenda jambo juu ya lile ulilokusudia kwa kuamini.

Huo ndio ulikuwa ushuhuda wa binti huyo ambaye sasa ameondokana na mateso ya kuvuta sigara. Na tatizo hadi likawa kubwa, mwanzo wake huwa ni mdogo. Unaanza taratibu na kisha inakuwa ni balaa. Yatupasa tujifunze kutokana na makosa au shuhuda za wengine.

Naamini wale wote ambao wanasumbuliwa na roho ya uvutaji wa sigara kama Jane watakuwa wamejifunza kitu kupitia ushuhuda huu.

Kijana mmoja aitwaye Juma akanipigia simu Jumanne wiki hii baada ya kuisoma makala ile. Anaishi Arusha. Akaniambia alifurahia sana makala yenye ushuhuda wa Jane. Akasema naye alikuwa na mpango wa kuvuta sigara lakini kwa mateso ya Jane, ameghairi kuvuta.

Akaniuliza; Je, sigara ina madhara gani? Kwa kifupi nikamjibu; Sigara ni kilevi, japo wavutaji hudai ni kiburudisho cha mawazo na akili lakini madhara ni makubwa; 1. Huleta athari kwenye ubongo.

2. Huathiri mapafu kwani moshi hufanya utando mweusi kwenye mapafu mwishowe huyatoboa na kusababisha kikohozi, kutapika damu na kasa. 3. Sigara huharibu bajeti yako 4. Hupoteza hamu ya kula na kadhalika. Niishie hapa;

Toa maoni na leta kisa chako!

Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]