Uwe ni mwaka wa ustawi kwa watoto wa mitaani  

02Jan 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uwe ni mwaka wa ustawi kwa watoto wa mitaani  

 

KUWAPO kwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani hasa katika miji mikubwa nchini ni changamoto kubwa inayohitaji ufumbuzi wa haraka.

Hata Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari mwanzoni mwa mwaka huu akikiri kuwapo kwa changamoto hiyo. 

Alikuwa akijibu swali Bungeni kutoka kwa Khatib Said Haji, mbunge wa jimbo la Konde aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na ongezeko la watoto wa mtaani.

Kutokana na swali hilo, akafafanua kuwa serikali ina jukumu la msingi la kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto hao unapatikana pamoja na kushirikisha jamii iweze kuwasaidia kuwaokoa vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwamo watoto wa mtaani.

Hicho ndicho alichosema waziri, lakini tunapoingia mwaka mpya wa 2018, ni vyema jamii nayo ikahusika kikamilifu katika kutatua changamoto hii ili waondoke kwenye mazingira hayo na ikiwezekana wapate elimu.

Kwa muda mrefu imekuwa kama jambo la kawaida kuona watoto wadogo wa kuanzia umri ya kwenda shule wakiwa kandokando ya mabarabara wakiomba msaada wa fedha kwa watu mbalimbali wakiwamo madereva wa magari na wapita njia.

Kama nilivyosema, umri huo ni wa kwenda shule ili kupata elimu, lakini ajabu ni kwamba wanazurura mitaani hali, ambayo haieleweki kama watakuwa wa aina gani hapo baadaye wakishakuwa watu wazima.

Wapo wengine wanafanya kazi ya kusafisha vioo vya magari na wakati mwingine hufanya kazi hiyo bila kuruhusiwa na wakishamaliza huomba pesa, wasipopewa huwafanyia fujo madereva na hasa wanawake.

Hali kama hii siyo nzuri kwani wakiendelea hivyo wanaweza kuwa watu hatari hapo baadaye kama watoto hawa hawataondolewa katika mazingira waliomo sasa na kupelekwa shule ili angalau wapate elimu.

Mwaka 2018 serikali iandae mkakati maalum wa kuhakikisha watoto walio katika mazingira haya wanaondolewa ili kuepuka kuandaa bomu la kesho badala ya vijana wa kesho watakaoliongoza taifa hili.

Kwa maana hiyo mwaka 2018 jitihada za makusudi za kuwaondoa katika ajira hizi zifanyike na kuwapeleka shule ili wapate elimu itakayowasaidia kumudu maisha yao ya baadaye kuliko kuendelea kuwa katika mazingira hayo.Ninajua kwamba serikali ina mipango yake ambayo imeiweka katika bajeti ya mwaka 2017/2018, lakini siyo vibaya tatizo hili la watoto wa mitaani likachukuliwa kwa udharura wake na kupatiwa ufumbuzi katika mwaka huu mpya wa 2018.

Pamoja na hayo ni vyema jamii nayo ikabadilika na kutambua umuhimu wa malezi bora, ambayo yatawafanya watoto watulie nyumbani badala kukimbilia mitaani kama ilivyo sasa.

Ninasema hivyo kwa sababu utafiti uliowahi kufanywa hapa nchini mwaka 2009 na shirika lisilo la kiserikali la Uingereza “Consortium for Street Children” ulibaini chanzo cha kuwapo idadi kubwa ya watoto wa mitaani kuwa ni njaa na ukatili.

Utafiti huo ulifanyika katika miji mikuu saba hapa nchini ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida na Kilimanjaro na kubaini sababu mbalimbali zinazochangia watoto kukimbia kutoka kwao, lakini kubwa zikiwa ni hizo mbili.

Niseme kuwa suala la njaa linaweza kuwa juu ya uwezo wa wazazi au walezi, lakini ukatili ni tabia ambayo wanaweza kuiacha na wakalea watoto wao vizuri na tena katika maadili mema.

Hivyo mwaka 2018 unapoanza, wazazi na walezi wenye tabia ya ukatili waachane nayo na kulea watoto wao vizuri ili wasikimbilie mitaani na mwisho wake ndoto zao za baadaye zinaharibika. Muungwana anaona kwamba wazazi wakitoa malezi mazuri kwa watoto wao hata idadi ya wanaokimbilia mitaani wakiogopa mateso itapungua kama siyo kwisha kabisa.

Tanzania bila watoto wa mitaani inawezekana iwapo jamii itatimiza wajibu wa malezi bora.