Uwekezaji Simba ukikwama, soka la Tanzania pia litakwama jumla

23Nov 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uwekezaji Simba ukikwama, soka la Tanzania pia litakwama jumla

NIMEKUWA nikifuatilia sakata la uwezekaji kwenye klabu ya Simba kwa siku hizi mbili tatu, kuhusu sakata la klabu hiyo na Tume ya Taifa ya Ushindani (FCC).

Nimesikiliza redio, nimeangalia televisheni na kusoma mitandao mbalimbali ya kijamii, nikagundua vitu kadhaa. Kuna upande unataka uwekezaji ufanikiwe ili klabu ya Simba ianze kujitegemea yenyewe na kuendeshwa kwa mfumo ya hisa, kufuatia kupata Mwekezaji, Mohamed "Mo" Dewji.

Wanachama na mashabiki wa Simba wanaamini kuwa Dewji kwa sasa ndiye mtu sahihi kwenye klabu yao anayeweza kuitoa sehemu moja na kuipeleka sehemu nyingine na klabu yao ikaendeshwa kisasa na kuwa mfano ya klabu zingine Tanzania.

Lakini suala hili linaonekana kama vile kuna watu nyuma ya pazia, wana mpango wa kutaka kulikwamisha.

Hii imetokana na taarifa iliyotolewa na FCC hivi majuzi, ambayo ilikuwa ikikanusha madai yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kuwa wao ndiyo wanakwamisha mabadiliko ya mfumo kwenye klabu hiyo.

FCC walikuwa wakijibu madai ya Mo na Mkuu wa Idara ya Habari wa klabu hiyo, Haji Manara, ambao kwa nyakati tofauti, walinukuliwa wakisema kuwa wanachosubiri ni ruhusa kutoka kwa tume hiyo ili mchakato wa mabadiliko uwe umekamilka.

Tume hiyo ni Taasisi ya Serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani namba 8 ya mwaka 2003, ili kusajiisha na kulinda ushindani na biashara na kuwalinda walaji dhidi ya mienendo isiyo ya haki na ya kupotosha.

Sitaki kuingia sana ndani, kuangalia nani kasema nini na nani kajibu nini, lakini suala hili linaonekana kukuzwa bila sababu yoyote ile. Lengo hapa ni kuisaidia Simba kutoka hapa ilipo na kwenda kwenye mabadiliko. Ikumbukwe kuwa kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hakuna klabu yoyote ambayo imeshawahi kutoka kwenye mfumo wa wanachama na kuingia kwenye hisa na uwekezaji, hivyo hata FCC yenyewe inajifunza kupitia hili.

Ni wajibu wa tume hiyo na viongozi wa Simba kukaa pamoja kwa lengo la kulitatua suala hilo na si kuonekana kama kutaka kulifanya liwe gumu na kuleta taharuki kwa mashabiki na wadau wa soka nchini.

Hata kama kuna makosa ambayo Simba wameyafanya, tume ilipaswa kuwaita na kuwaambia mapungufu yote yanayotakiwa kufanyiwa kazi ili mchakato usonge mbele.

Kuhusu upatikanaji wa Ofisa Mtendaji kwenye klabu ya Simba, ikumbukwe kuwa Simba bado si kampuni, ila ni klabu ya kucheza mpira, hivyo kabla ya mabadiliko ilikuwa ni lazima iwe na viongozi kwa matakwa ya Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Hakuna klabu ya soka inayoruhusiwa kucheza mpira bila ya kuwa na viongozi, hivyo Simba waliona wasisubiri kwanza, bali wapate viongozi waendelee kuongoza wakati mchakato unaendelea.

Ikumbukwe kuwa mashabiki wengi wa soka Tanzania wamechoshwa na soka la ubabaishaji na wanachotaka ni kuona klabu hizi zikiendeshwa kwa mfumo ambao Simba inataka kuelekea.

Klabu zote nchini, ikiwamo hata Yanga kwa sasa darasa lao la mfano ni Simba. Wote wanaiangalia. Itakapofanikiwa na kuingia kwenye mfumo, basi klabu zote zitafuata njia hiyo, tena wao hawatochukua muda mrefu kwa sababu njia yote imeshawekwa na mtangulizi.

Lakini kama wapo watu wanataka kufanya mchakato huo uharibike kwa makusudi yao binafsi, basi wajue hawaikomoi au kuiangusha Simba, bali wanaliangusha soka la Tanzania.

Mchakato wa Simba ukifelishwa, labda kwa sababu tu za kukomoana, au Usimba na Uyanga, basi hata Yanga na klabu zingine hazitofanya mabadiliko na soka litarudi kule kule.

Uwapo wa watu wanaojitokeza kuweka kama Mo Dewji, ndiyo umeisababisha hata Yanga kuchangamka na kumpata GSM, badala ya kuendeleza bakuli lao, hivyo kumekuwa na upinzani mkali kwa sasa ambao unainua zaidi soka la Tanzania.

Kwa sasa Ligi ya Tanzania ndiyo inayotazamwa sana Afrika Mashariki na Kati kutokana na kukusanya wachezaji kutoka ukanda wote huo. Na hiyo yote ni kwa sababu ya watu wachache tu walioamua kutaka kuwekeza kwenye soka, Said Salim Bakharesa, Mo na GSM.

Wachezaji kama Clatous Chama, Luis Miquissone, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Prince Dube, Meddie Kagere ni baadhi ya nyota wa kigeni wenye thamani kubwa, wanaofanya ligi ya Tanzania iangaliwe sana Afrika Mashariki na Kati, hivyo wakitumiwa vema wataiingizia Tanzania mapato makubwa kuliko inavyodhaniwa.

Hata wachezaji wa Kitanzania, kutokana na kucheza na wachezaji hao kila wiki, viwango vyao vimeimarika kiasi cha Taifa Stars kuweza kusimama dakika 90 ugenini dhidi ya Tunisia na kufungwa bao 1-0 tu na kutoka sare bao 1-1 hapa nchini, kitu ambacho huko nyuma kabla ya kuingia kina Mo na kusajili wachezaji wa gharama kutoka nje, Stars ilikuwa ikifungwa idadi kubwa ya mabao.

Inabidi sasa kuwekwe mazingira mazuri ya kuhakikisha matajiri waliojitokeza wanabaki kuwafanya wale ambao wanaonekana kusita, kujiingiza kwenye soka.

Kuna matajiri wengi nchini Tanzania, lakini wamekuwa hawataki kujiingiza kwenye soka kutokana na kutokuwapo kwa mazingira na mifumo mizuri ya uwekezaji kwenye tasnia hiyo.

Hawa waliopo wanaonekana tu wana roho ngumu kutokana na wenyewe kuwa wanamichezo au wapenzi na mashabiki wa soka kindakindaki.

Ikumbukwe kuwa duniani kote sasa soka ni biashara, hivyo baadhi ya nchi wanaweka mifumo yake vizuri kwa ajili ya michezo, ikiwamo soka na wameshaondokana na kudhani kuwa soka ni burudani, afya, na sehemu ya kukutania marafiki pekee.