Uzoaji taka bado tatizo Mwananyamala

07Aug 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uzoaji taka bado tatizo Mwananyamala

HIVI sasa duniani ni miaka mingi imeshapita, elimu kuhusu umuhimu na usalama wa mazingira ni jambo muhimu sana.

Ni muhimu kwa maana kwamba, inatujengea mazingira ya usalama kiafya na mengi yanayoambatana nayo.

Ukitaka kulijua hilo kwa kina, angalia hata hapa nyumbani kwetu, wajibu wa jukumu hilo ajenda ya mazingira iko chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Kimantiki, pia nakubaliana na kwa maana zote za usemi ‘mazingira ni uhai.’ Katika moja ya mambo ambayo ni kipaumbele cha sekta hiyo ni usafi wa kuhakikisha hakuna adha ya taka katika maeneo tunayoishi. Nani analibishia hilo?

Lakini inaopokuja katika utekelezaji wake, jibu linaanza kuwa gumu kiasi, kwa sisi tunaoishi hasa mijini ambako kuna ugumu wa kupata maeneo sahihi ya kutosha kukusanya na kuharibu kwa kuchoma moto taka na mambo kama hayo.

Uongozi wa serikali zetu za mitaa uliyaona hayo na kuunda mifumo ya kuyakabili, kuwa na namna au nyenzo kama magari au trekta yanayokusanya, kuzoa na kwenda kutupa taka hizo. Hiyo si mji mmoja au mwingine, bali kote duniani iko hivyo.

Mifumo hiyo ya kukusanya taka hupitia mamlaka za mitaa, ambazo huku kwetu inakuwahi katika sura ya ama mamlaka za miji, manispaa, jiji au wilaya, inayokusanya na kutenga maeneo maalum ya kutupa taka hizo.

Nirejee katika eneo la Mwananyamala Kisiwani ambakao nina ushuhuda wake. Utaratibu ulioko mahali hapo ni kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, kwamba kuna magari ya kampuni binfasi zilizopewa kandarasi ya kuzoa taka na zingine mali ya halmashauri hiyo.

Watu wanagharamia, chini ya usimamizi wa viongozi wa serikali ya mitaa hadi ngazi ya chini kwa mabalozi wanaokusanya malipo kutoka kwa kila mkazi, hapo nikimaanisha mwenye nyumba hadi mpangaji katika nyumba wastani wa shilingi 1,000 kwa kila mwezi kutoka kwa kila mmoja.

Hapo kuna siku maalum zilizotengwa magari kupita katika eneo maalum kunakoelekezwa kukusanya taka ambazo wazoaji wenye vyombo vya usafiri hupita kukusanya taka hizo.

Malalamiko yetu katika sura kuu hapa, ni hasa pale watarajiwa wa kukusanya taka wenye jukumu au kandarasi hiyo hawajitokezi kwa wakati uliopangwa, ilhali huduma yao inakuwa imeshalipiwa.

Huwa tukienda kuuliza kwa viongozi wetu tulio nao jirani, tunapata majibu ambayo ni wazi yako mbali na ukweli stahiki.

Zaidi ya hapo, nikirejea hoja ya watu hao kushindwa kuzoa taka kwa wakati, badala ya kuboresha mazingira, inachukua sura ya upande wa pili kwamba inachafua mazingira zaidi.

Mahali kunakoelekezwa uchafu kukusanywa ni penye makazi ya watu ambako, taka zinapovunda inakuwa balaa. Hali inakuwa mbaya zaidi na imekuwa kawaida wakazi hao jirani wanalalamika mno, pasipo kusikiwa dai au lalamiko lao, sasa huku ni kuboresha mazingira kweli?

Hali inakuwa mbaya pale mvua zinaponyesha, taka zinapovunda na kuzaa mabaya kuliko, harufu inatapakaa mno kila mahali.

Tunajua taka hizi huzolewa na kwenda kumwagwa katika dampo ya Pugu Kinyamwezi, kutokana na miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam, panapo nyenzo bora za usafiri wa kuzoa taka, inapafanya pasiwe mbali zaidi.

Hata kama kuna shida ya msongamano wa magari, basi kazi hii inaweza kufanyika usiku kwa tija zaidi, kuondoa kero hii. Inapaswa tufike mahali halmashauri zetu nchini na si Kinondoni pekee, kuweka maendeleo kutoka katika sura ya ufanisi wa vitendo.