Uzoaji takataka mitaani ni kero kuliko uchafu wenyewe

06Sep 2020
Adam Fungamwango
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Uzoaji takataka mitaani ni kero kuliko uchafu wenyewe

HIVI sasa kila sehemu ina utaratibu wake kwenye masuala ya ulinzi na uzoaji takataka. Taratibu na kanuni hizo zinasimamiwa na serikali za mitaa kwenda kwenye kata na halmashauri nchini kote.

Kuna sehemu watoa huduma hizo kama vile takatata, wanatoza pesa kwa nyumba, huku wengine wakitoza kila chumba. Kuna watu wamekuwa wakipita kwenye makazi ya watu ukusanya fedha hizo kila mwezi.

Hii ni kwa sababu ya kuzuia wezi, lakini pia kuzuia utupaji holela wa taka ili kuzuia maambukizo ya magonjwa mbalimbali kama vile homa za matumbo na kipindupindu.

Jijiji Dar es Salaam, katika maeneo mbalimbali, kumekuwa na kero kubwa kuhusiana na uzoaji ya takataka, ambapo kumekuwa na ucheleshwaji mkubwa. Kuna wakati takataka zimekuwa zikionekana kukusanywa katika maeneo na kukaa hapo hata kwa wiki mbili kabla ya magari ya wazabuni wa kufanya kazi hiyo hayajafika kuzichukua.

Kinachofanyika ni kwamba wananchi hukusanya takataka kutoka kwenye makazi yao zikiwa ndani ya viroba na kuziweka maeneo waliyoelekezwa.

Hali hiyo imesababisha kero kubwa kwa sababu ya kukaa kwa muda mrefu kabla ya magari hayajafika , hivyo kuhatarisha afya za wakazi wa maeneo husika. Haijulikani ni kwa nini kumekuwa na ucheweshaji wa uzoaji, wakati wakazi hao wamekuwa wakitozwa pesa.

Kitachotakiwa kufanyika ni serikali za mitaa kupeleka pesa hizo kwa wenye magari ya kuzoa taka na kuifanya kazi hiyo mara moja.

Kuchelewa kwa magari kuzoa taka kwa baadhi ya maeneo yakiwamo Mwananyamala, Segerea na Tabata, kunaashiria kuwa kuna tatizo mahala. Je, pesa za kulipa malori ya takataka hazifiki kwa wakati? Kama siyo tatizo hasa ni nini? Ucheweshwaji huo umekuwa ukisababisha matatizo mbalimbali mitaani.

Kwanza kabisa, milima ya viroba ya takataka wakati mwingine unakuwa kando ya barabara, wakati mwingine kuzuia magari kupita hasa barabara zile za mitaani, hivyo kusababisha madereva kuteremka na kusogeza kwanza baadhi ya viroba ili kupita au kupishana.

Kero nyingine ni kwamba maeneo mengine ambako wanaelekezwa na serikali za mitaa ni kuweka nje ya nyumba za watu.

Baadhi wa wenye nyumba wa wapangaji wamekuwa wakilalamika hali hiyo kuwa inawafanya kulala kwa taabu kutokana na harufu ya takataka hizo kwani zinakaa muda mrefu bila kuchukuliwa na kusababisha funza kuanza kutoka kwenye viroba pindi mvua mvua zinaponyesha.

Hali hii inaondoa kabisa ile dhana ilivyojengwa mwanzo kuwa kuzoa taka ni kuleta usafi kwa jamii. Hali hiyo imekuwa kero kwani wakati mwingine inasababisha magonjwa ya kuambukiza.

Kuna baadhi ya wakazi wamekuwa wakidai kuwa kama kuna ucheleweshwaji wa kuzolewa takataka kwa sababu yoyote ile, basi takataka hizo zipelekwe na kuwekwa nje ya ofisi za serikali za mitaa, ili kama kutakuwa na ucheleweshaji, viongozi waone athari na huenda ikawafanya kukumbuka kusimamia magari kupita mitaani na kuchukua takataka kwa wakati.

Ni vyema serikali za mitaa zikachukua hatua kabla ya kusubiri mpaka magonjwa ya mlipuko yatokee ndipo hatua zichukuliwe. Ni bora kukinga kuliko kutibu.