Vifo hivi vitushitue kuwa makini utumiaji tumbaku

10Jun 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vifo hivi vitushitue kuwa makini utumiaji tumbaku

WAVUTAJI wa sigara, sasa ni wazi kwamba wanapaswa kufikiria upya starehe yao hiyo na ikiwezekana wachukue hatua ya kuachana nayo, kwa kutafuta mbadala ili kuepuka madhara ya kiafya wanayoweza kuyapata.

Hiyo ni kwa sababu inakadiriwa watu milioni sita, hufariki kila mwaka duniani, kutokana na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, zikiwamo sigara na shisha au asiye mvutaji kujikuta anavuta moshi kutoka kwa mvutaji

Inaelezwa katika mazingira hayo asilimia 28 ya watoto wanapoteza maisha, kati yao wanawake asilimia sita na wanaume asilimia 12. Inakadiriwa hadi kufikia mwaka 2030, vifo vitokanavyo na tumbaku vitaongezeka na kufika zaidi ya milioni nane kwa mwaka.

Licha ya watu kufariki dunia kwa kutumia tumbaku na kuvuta moshi kutoka kwa mtumiaji madhara yanayowapata waathirika ni pamoja na kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo saratani, magonjwa ya njia ya hewa.

Magonjwa mengine yanayotajwa, ni pamoja na mapafu na kisukari na yanayoathiri moyo, mishipa ya damu na kuongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu.

Hivi sasa nchini, kunatajwa wastani asilimia 14 ya Watanzania wanatumia tumbaku na kwamba idadi ya wanaoathirika kutokana na moshi wa tumbaku kutoka kwa wavutaji inaongezeka.

Kutokana na athari hizo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, anakiri tatizo na anahimiza serikali inaendelea kulipiga vita kupitia wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007.

Ni sera ambayo sehemu ya maudhui yake inalenga kuhudumia magonjwa yasiyoambukizwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO,) ambalo limekuwa likifanya jitihada mbalimbali za kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Ufafanuzi wake uko kwenye maadhimisho ya Siku Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku, kwamba hadi sasa serikali inaendelea kusisitiza kuacha utumiaji wa bidhaa za tumbaku iitwayo ‘shisha.’

Kwa kuwa ni wazi kwamba bidhaa hiyo ina madhara kwa afya za  watu, basi  kuna haja kila mmoja wetu kuanzia kwa wavutaji na wanaovutoshwa tumbaku kujiongeza ili waweze kulinda afya zao.

Hiyo inafanya umuhimu wa jamii kuongeza uelewa kwenye madhara yanayoweza kupatikana kutokana na matumizi ya tumbaku au kuwa karibu na mtu anayetumia kilevi hicho.

Jinsi mazingira ya uvutaji yalivyo nchini, baadhi ya watumiaji tumbaku wamekuwa wakivuta kwenye mikusanyiko ya watu, hata inawezekana watakuwa wameumiza wengine bila ya kujua au wanaovutisha nao bila kujua.

Elimu ni muhimu kwenye janga hilo, ambalo linatajwa kuchangia vifo milioni sita kwa mwaka, ili jamii iweze kuwa makini badala ya kuendelea kushuhudia watu wakivutishwa tumbaku bila kujua madhara yake.

Inasikitisha kusikia matumizi ya tumbaku yanaangamiza maisha ya wavutaji na wanaovutishwa, hivyo ipo haja ya kuelimisha umma wa Watanzania kuhusu madhara, pia kuepuka matangazo ya kuhamasisha uvutaji.

Katika pakti za sigara zimeandikwa tahadhari, ambayao ikiendana na elimu maradufu kwa umma, inaweza kusaidia kutimiza kaulimbiu ya  maadhimisho ya mwaka huu isemayo "dhamiria kuacha kutumia tumbaku na bidhaa zake."

Vilevile itapendeza iwapo ushauri wa wadau wa kupinga matumizi ya tumbaku utazingatiwa, ambao ni kutaka kutafuta mazao mengine mbadala wa zao hilo.

Karanga, chai, ufuta na alizeti ni miongoni mwa mazao ambayo yanaweza kuwa mbadala ya tumbaku, japo moja kati yao na yana soko kubwa la kuweza kuiingiza serikali fedha za kigeni.Ends