Vijana tuepuke kutelekeza watoto kwa babu na bibi

04Jan 2018
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vijana tuepuke kutelekeza watoto kwa babu na bibi

NADHANI nianze na swali, mnaotelekeza watoto kwa wazazi wenu bila ya kutoa misaada mnategemea nini?

Kumekuwapo na tabia sugu ya ajabu, inayofanywa na vijana kuzaa watoto na wanawapeleka vijijini kwa wazazi wao wakaishi, lakini hawakumbuki kupeleka gharama za matunzo.

 

Hivi huko mnapowapeleka watoto na kuwaachia wazazi wenu, wawalelee mnashindwa kuwapeleka matunzo nategemea nani awatunzie? 

Wazazi wametuleta duniani sisi na wakajinyima kwa kutupatia elimu, lengo ni kutuwezesha kupata ajira au uwezo mwingine halali wa kujishughulisha baadaye maisha, katika sura ya ukombozi kwao, pale wanapokuwa hawana nguvu za kuzalisha.

 

Katika suala la elimu sio kuwa wote wanaenda ngazi ya sekondari na vyuo vikuu, la hasha! Elimu yoyote anayoipata kijana inamwezesha kuajiriwa au kujiajiri. Ni moja ya mafanikio kwa wazazi.

 

Tukumbuke, wazazi wanapoona watoto wao wana kibarua, wanafarijika kwa kupatiwa misaada pale mwana anapokuwa na pesa.

 

Najua kuwa uwezo tunazidiana katika vipato, wapo wanaowajengea nyumba wazazi na wapo ambao hawakuwajengea, lakini kidogo wakipatacho, wanawakumbuka wazazi.

 

Wazazi hufarijika na chochote wanachokipata kutoka kwa mtoto na ndio maana unakuta hata wengine wanatamka; “nashukuru nakula matunda ya mwanangu.”

 

Sasa nazungumzia hili la baadhi ya vijana linalokosa aibu kwa kuzaa watoto mijini na kwenda kuwabwaga watoto wao vijijini kwa wazazi, bila ya kupeleka pesa za matumizi.

 

Wewe uliyezaa mjini, umeona maisha yamekushinda, huko kijiji ndio kuna vya bure hata ukaamua kumtupa huko mtoto wako?

 

Inaumiza sana. Wazazi wanawapenda wajukuu, lakini na sisi tuwapende waangalizi hao ambao tunawapelekea watoto wetu.

 

Kinachosikitisha unampeleka mtoto kijijini na huwasilishi fedha ya matumizi kwao, wewe unakaa mjini kuponda starehe unamwachia mzazi wako mizigo akulelee.

 

Hivi inakuingia akilini, wewe angekutupa usipate msaada, leo hii ungekuwa ukilaani kitendo hicho kuwa ulitelekezwa?

 

Sasa hao watoto mnaowatelekeza vijijini wakikua na kuwakana au kukataa kuwasaidia pale mnapokosa uwezo, mtasema wamelaaniwa au?

 

Tukumbuke kuwa starehe haziishi, ila zinabadilika na zitaendelea kuwapo.

 

Hao wazazi wenu mnaowatupia watoto vijijini na kutokomea kijiji nao wana changamoto za kimaisha, hata milo mitatu au miwili kwa siku kuipata kwao ni shida.

 

Hali hiyo inafanya kushindwa kuwapeleka shule, watoto wenu kutokana na kusoma fedha za kununua vifaa vya shule.

 

Pamoja na serikali kusema ‘elimu bure’ kuna vifaa ambavyo tunatakiwa sisi kama wazazi kununua.

 

Wapo baadhi ya hao tunaowaachia watoto, wameshindwa kununua na kusababisha watoto kukatiza masomo na kuishia kwenda kuangalia televisheni mitaani.

 

Hivi karibuni, mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo kijiji cha Nyangunguti, Mkuranga mmoja wa wanakijiji alisema taarifa za kijiji kikubwa ni watoto zaidi ya 30 wameacha shule kutokana na kukosa vifaa vya hule.

 

Ikaelezwa kuwa watoto hao wapo shule ya msingi na watano sekondari. Kilichowasababisha kuacha shule ni kutonunuliwa vifaa vya shule na wazazi wao.

 

Inaelezwa, watoto hao wazazi wao waliwatelekeza vijijini kwa bibi na babu, lakini nao hawana uwezo wa kuwasaidia, hivyo wameacha shule na sasa wanashinda katika mabanda ya televisheni.

 

Mbunge wa Mkuranga – Ulega, ametoa fedha Shilingi 100,000 ili watoto hao wanunuliwe vifaa vya shule, waendelee na masomo.

 

Sasa tujiulize, hizo pesa zikiisha hao watoto wataendelea tena kukaa nyumbani? Inatakiwa wazazi tuone aibu, hali ya maisha kwa sasa ni ngumu kila mtu anasimama na mtu wake, asitegemee mtu baki abebe mizigo wake.