Viongozi na waandishi Afrika wachukue hatua

04May 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Viongozi na waandishi Afrika wachukue hatua

RAIS Samia Suluhu Hassan, anahitimisha kilele cha Siku ya Uhuru wa Habari Duniani kwa Afrika, akiwaonya waandishi wa Afrika, kujitazama kwani wanairipoti vibaya Afrika kama vile ambavyo wanahabari wa kigeni wanavyoendeleza taarifa mbaya kuhusu bara hilo.

Anapowahutubia waandishi wa Afrika jijini Arusha jana, Rais anasema ni kama vyombo vya habari vya Afrika vinavisaidia vile vya kigeni kuendelea kuichafua Afrika, jambo ambalo anasema si jema kwa bara hilo.

Anapowageukia wanahabari wa Tanzania anasema kuna mengi mazuri ya kuripoti lakini kila wakati yanasahaulika na uandishi unakuwa wa matukio mabaya zaidi yanayodhalilisha badala ya kuleta matumaini na mwangaza wa maisha ya wasomaji na jamii inayoandikwa.

Anatoa mfano kuwa imekuwa ni kawaida watu kuimba wimbo wa umaskini miongoni mwa Waafrika kuwa wanaishi chini ya Dola moja kwa siku ambayo ni takribani shilingi 2,300.

Rais anasema nadharia hiyo hajaikubali na mara nyingi anaipinga wakati akikutana na wanaoitetea, akiwafahamisha kuwa wapo watu wanaoishi kwa kula matunda mbalimbali tena yanayozalishwa kwa kilimo kisichotumia kemikali, mbolea na viuatilifu vya viwanda, chakula ambacho kinauzwa ghali kwenye ‘supa maketi’ za Ulaya na Marekani, hivyo siyo kweli kuwa watu wanaishi chini ya Dola moja.

Anatoa mfano wa wafugaji kama Wamasai wanaoishi kwenye nyumba za asili ambao wana utajiri mkubwa wa mifugo ambayo pekee inadhihirisha kuwa si maskini kama inavyoelezwa.

Anawaambia wanahabari kuwa wabadilike na kuanza kuandika mengi mazuri ya Afrika na Tanzania na kulipenda bara lao.

Kwa hivyo anawahamasisha kujikita katika kuikabili dhana potofu kuhusu bara la Afrika na kukuza uandishi na utangazaji wa ripoti zenye uwiano na uhakika.

Ni vyema angalizo za Rais likafanyiwa kazi kuhusu kuripoti mabaya kuhusu Tanzania na hata Afrika. Ni kweli kuwa taarifa nyingi zikitafitiwa zinaonyesha upungufu zaidi. Kwa mfano miaka ya nyuma habari za wanawake kwenye vyombo vya habari vingi zilihusu udhalilishaji kama ubakaji, mimba, jinai na kwa ujumla taarifa mbaya wakati mwingine zikiambatana na picha za waathirika hao.

Hata hivyo, juhudi zilifanyika na kubadilisha sura hiyo na sasa ripoti za masuala ya kinamama zinawaonyesha wakiwa na mafanikio badala ya kubakia kuwa wadhalilishwaji.

Pamoja na nia njema ya Rais kuwahimiza wanahabari kuandika masuala ya maendeleo na mafanikio ukweli ni kwamba viongozi wa Afrika wanawajibu wa kuimarisha sekta ya habari ya umma, ili kuwa na mashirika ya habari ya umma, redio na televisheni za umma badala ya uandishi wa Afrika kutegemea kupata habari za Kiafrika kupitia mashirika ya kigeni ambayo nayo huiandika vibaya Afrika.

Ni wazi kuwa vyombo vya habari vya Afrika vinategemea habari za Afrika kutoka mashirika ya Reuters, au BBC yote ya Uingereza, AFP la Ufaransa, Xhnua la China ili kupata taarifa za nchi za Kiafrika.

Pengine kama kungekuwa na vyombo vya habari vya Afrika vyenye taarifa sahihi na zinazoelezea mema ya Afrika utegemezi wa mashiriki au vyombo vya kigeni ungepunguzwa.

Rais na viongozi wa Afrika wanapaswa kuelewa kuwa baadhi ya vyombo vya habari havina fedha hivyo kutegemea vyanzo vya nje, vikiwamo mashirika makubwa ya habari ili viendelee kuwepo hivyo ni lazima serikali zisaidie vyombo hivyo kwa kuvipa matangazo, kuweka mazingira wezeshi, kuondoa sheria mbovu na kandamizi ili kuviwezesha kufanikisha lengo la uandishi unaoleta mabadiliko na maendeleo badala ya ule wa kulalamika na kutangaza ubaya wa serikali zao.