Viongozi Yanga, GSM kwa nini mgombee fito?

06Apr 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Viongozi Yanga, GSM kwa nini mgombee fito?

NAJUA kwa sasa suala hili limemalizika, lakini ni lazima lisemwe, liwekwe sawa na kisha kutolewa ushauri ili lisijirudie tena.

Mara nyingi kuna mambo yanajitokeza na yanaonekana kumalizika, lakini baadaye yanaibuka tena kutokana na upande mmoja au pande zote kutofuata makubaliano yaliyowekwa kwa pande zote.

Viongozi wa Yanga hivi karibuni waliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kueleza kuwa tofauti zao na GSM zimemalizika na sasa wote wako kitu kimoja.

Hii ilitokana na kuibuka kwa sintofahamu kati ya baadhi ya viongozi wa Yanga na wadhamini wao GSM uliosababisha baadhi ya viongozi wa Kamati ya Utendaji ndani ya klabu hiyo kuenguliwa madarakani na wengine kujiuzulu.

Wimbi hili lilitokana na wanachama wengi wa Yanga kuwajia juu viongozi wao kuwa wanamzuia mdhamini wao, Kampuni ya GSM kufanya kazi yake kwa ufanisi na kuwataka wachukua hatua za kinidhamu kwa wote waliohusika, la sivyo viongozi wa ngazi ya juu wataubeba msalaba huo.

Wanachama na mashabiki wa Yanga walikuja juu baada ya Kampuni ya GSM kuandika barua ya kujitoa kwenye masuala yasiyo ya kimkataba wa udhamini wao ndani ya klabu hiyo.

GSM, imekuwa ikitoa mishahara kwa baadhi ya wachezaji na kusajili pia, kutoa posho na mambo mengine ambayo awali hayakuwa kwenye mkataba baina ya pande hizo mbili.

Wanachama na mashabiki wa Yanga, wakajua fika kuwa kama GSM wakijiweka kando kwenye masuala hayo, basi timu itarejea kule kule kwenye kusajili wachezaji wa kuungaunga, na hata mishahara ya wachezaji kuwa shida, huku yote hayo, mwisho wake hata ushindi kuupata kwa tabu.

Kilichoonekana hapo ni mgongano wa kimadaraka na si kitu kingine chochote kile na kwa vile tayari viongozi wa Yanga na GSM wameshapatana, inabidi sasa wawekeane mipaka kwenye ufanyaji kazi ambao vile vile uwe ni wa kushirikiana.

Kwa upande wao viongozi wa Yanga, waliona kitendo cha mdhamini wao kujichukulia jukumu wa kusajili mwenyewe bila wao kushirikishwa au wao kufanya kazi hiyo ni kama kuwadharau au kuwapoka madaraka yao.

Wanaona kuwa wao ndiyo wana mamlaka kikatiba kufanya kazi hizo za klabu na mdhamini afanye kazi zake zilizomo kwenye mkataba.

Tukienda kwa upande wa pili, tatizo ni kwamba viongozi wengi wa klabu za Kibongo hawaaminiki.

Nafikiri GSM iliona kama ikiwapa moja kwa moja pesa kwa ajili ya kusajili wachezaji, basi kuna baadhi ya viongozi watapiga panga kwa lugha ya kimichezo, lakini kwa ile ya kawaida ni kwamba mchezaji hazimfikii zote.

Sasa hapa kwa sababu wameshapatana na kuwa kitu kimoja kinachotakiwa ni kukaa na kuangalia ni utaratibu gani utatumika ili pande zote mbili zihusike kwa wakati mmoja kwenye masuala ya usajili na hata yale ambayo yapo nje kimkataba.

GSM na viongozi wa Yanga inabidi washirikishane kwa mambo yote ambayo yanataka kufanyika siyo mmoja wanamficha mwenzake, au kila upande unafanya mambo kivyake wakati wote lengo lao ni moja tu, kusukuma gurudumu la Yanga mbele.

Haileti picha nzuri, wote wanajenga nyumba moja, lakini wananyang'anyana fito. Kila mmoja afanye kazi yake. Viongozi wafanye kazi yao ya kuongoza klabu na GSM afanye kazi yake iliyo ndani ya mkataba.

Na chochote kile ambacho kiko nje ya mkataba na kina manufaa kwa Yanga, ni lazima GSM iwaite viongozi wa Yanga na kuwashirikisha na kufanya maamuzi kwa pamoja, ili kila mmoja ajione ni sehemu ya mafanikio. GSM waone pesa yao imetumika kama ilivyopangwa na haijachakachuliwa, huku viongozi nao wakipewa hadhi yao ya kusajili wachezaji kama ilivyo kawaida.

Haya yakizingatiwa, basi pande zote zitafanya kazi bila migongano, lakini yakipuuzwa, ipo siku isiyo na jina, mambo yanaweza kuvurugika tena na hali kuwa mbaya zaidi.