Visawe, vitawe na vitate ni nini?

06Aug 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Visawe, vitawe na vitate ni nini?

VISAWE ni maneno yenye maana zinazokaribiana. Kwa mfano, ‘mtoto’ na ‘mwana’ humaanisha kitu kimoja. Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21 (Uk. wa 577), visawe hutumika ili kuwasilisha dhana ileile iliyokusudiwa bila kubadilisha maana.

Hivyo Visawe hupamba lugha ama katika mazungumzo au katika uandishi wa aina mbalimbali.

Mifano ya visawe: Afya: siha, zihi, rai, nguvu, uzima. Aibu: haya, tahayuri, soni. Alama: doa, ishara, dalili, taashira. Anza: takadamu, amiri, tangulia. Apiza: laani, duia. Arbuni: kishanzu, advansi. Athari: dosari, doa, kasoro.

Bahili: mchoyo. Baradhuli: zuzu, zuge, bwege, juha, jura, jinga. Baraste: barabara, tariki. Busara: hekima, akili, tabasuri. Chelewa: kawia, limatia, faitika, taahari, ahirika. Cheo: mamlaka, dhima, madaraka, wadhifa. Daawa: kesi, mashtaka. Daktari: tabibu, mhazigi, mganga. Duni: dhalili, hafifu, nyonge.

Fadhili: wema, hisani, ukarimu. Fikiri: waza, dhani, tafakari. Fuvu: bufuu, fuu. Kapera: mseja, mhuni. Kasoro: hitilafu, walakini, doa, taksiri. Kera: udhi, kirihi. Kibahaluli: kibatari, koroboi. Kimetameta: kimulimuli. Kuwadi: kijumbe, gambera, mtalaleshi, kibirikizi.

Laghai: danganya, nyenga, ongopa. Matata: chachawizo, ghasia, fujo, sokomoko, ugomvi, kimondo. Mauzauza: kiinimacho, mizungu, mazingaombwe. Mnadi: dalali. Mnyama: hayawani. Mpagazi: hamali, mchukuzi. Mpelelezi: jasusi, kachero, mdadisi. Msichana: banati, binti, mwari. Mtu: mja, adinasi, mwanadamu, mahuluki. Mvulana: ghulamu, janadume, barobaro. Mwizi: pwagu, pwaguzi, mdokozi. Nasa: kamata, nata, gwia. Ndoa: nikahi, harusi.

Rafiki: sahibu, somo. Rika: umri, hirimu, umri unaolingana. Shabihi: fanana, landana. Shamba: konde, mgunda. Simanzi: majonzi, jitimai, ukiwa, huzuni. Stadi: bingwa, farsi, mweledi, gwiji, mtaalamu. Taabika: sumbuka, hangaika, dhikika. Taadhima: heshima, adabu, tasfida.

Uchawi: juju, sihiri, ulozi. Ugali: sima. Ugonjwa: maradhi, uwele. Ukuta: kiambaza. Uliza: saili, hoji. Wajihi: sura, uso. Weweseka: hohosa, babaika, kiakia, hangaika, riaria. Wia: dai, kitendo cha kutoka mahali fulani, kitendo cha jambo kuwa zito kutokea: imeniwia vigumu kuja. Wia radhi: kitendo cha mtu kuomba msamaha; alimwambia amwie radhi, akamsamehe.

Maneno yaliyo kwenye vitawe na vitate yataelezwa kwenye matoleo yajayo. Hapana shaka ufafanuzi wa maneno haya yatawasaidia sana waandishi na wasomaji wanaotumia maneno ya vijiweni/mitaani yaliyo kinyume cha ufasaha wa lugha ya Kiswahili kama ilivyo hapa chini:

“Stars, Harambee hainaga” ni kichwa cha habari ya gazeti la michezo. Kichwa hicho kina makosa mawili: Kiswahili hakina neno ‘hainaga’ ingawa siku hizi neno hilo hutumiwa sana mitaani. Kichwa cha habari yenyewe hakikukamilika! Hakielezi Stars, Harambee ‘hazina’ kitu gani!

Neno ‘…ga’ limezoeleka sana mkoani Mwanza: ‘nakwendaga’ badala ya huenda, hula, hulala, huimba, husema (mara kwa mara) badala ya nakwendaga, nakulaga, nalalaga, naimbaga, nasemaga maneno ambayo si Kiswahili sahihi. Hali ilivyo sasa nadhani kuna wakati tutasema ‘fyombo fyangu’ (Wanyakyusa) badala ya vyombo vyangu; ‘ndisi mbifu,’ ‘ukali’ (Wachaga) badala ya ndizi mbivu, ugali.

Aidha kuna maneno yanayotumiwa tofauti na maana yake halisi. Kwa mfano siku hizi pilipilimboga zaitwa ‘hoho’ au ‘pilipilihoho!’ Pilipilimboga ni pilipili kubwa yenye rangi ya kijani, manjano au nyekundu isiyowasha, aghalabu hutumika kwenye kachumbari au kiungo kwenye upishi. ‘Hoho’ au ‘pilipilihoho’ ni ndogo nyembamba, nyekundu inapoiva na huwasha sana. Kwa ukali wake, huitwa pilipili kichaa. Husaidia kutibu kideri, ugonjwa wa kuku wa kuhara na kukohoa.

“Stars, Congo kwa viatu hatari” ni kichwa cha habari kwenye moja ya magazeti yetu ya michezo. ‘Kiatu’ ni kitu kinachovaliwa miguuni ambacho hutengenezwa kwa ngozi, plastiki n.k. na wingi wake ni ‘viatu.’

Hapa “Stars, Congo kwa viatu hatari” haieleweki ila mpaka usome habari yenyewe ndio utagundua kuwa timu za Taifa Stars (Tanzania) na DR Congo ndizo zilizocheza rafu nyingi kuliko timu zingine zilizoshiriki michuano ya AFCON 2019.

Kichwa kingine kwenye gazeti hilohilo: “Couple matata inayopiga pesa.” Neno ‘couple’ si Kiswahili bali ni Kiingereza na maana yake ni vitu au watu wawili wanaohusiana kama vile mtu na mkewe, wachumba au maharusi. ‘Matata’ ni hali ya kugombana inayozuka miongoni mwa watu; ukorofi, mtu mwenye tabia ya ugomvi.

‘Piga’ ni kitendo cha kuadhibu kwa kugonga mwili kwa kitu kinachoumiza; kitendo cha kugonga kitu kwa kitu kingine kwa makusudi. ‘Pesa’ ni fedha. Sasa tusome kichwa kilichoandikwa: “Couple matata inayopiga pesa.”  Ni wasomaji wangapi waungwana wanaoelewa?

Magazeti yetu ya michezo huandika mambo ya ajabu ajabu sana. “Diamond amkana Tanasha buana!” Yaelekea neno la mwisho ‘limepasishwa’ kuwa badala ya neno halisi (bwana) huku wengine wakiandika ‘bana!’

Mshangao mwingine kwenye gazeti hilo ni baada ya kusoma kichwa cha habari husika yenye paragrafu 8 na mwisho wa habari hiyo kukiwa na picha ya Guardiola, kocha wa mabingwa wa Uingereza kwa mara ya pili mfululizo. Kichwa cha habari kimeandikwa kwa herufi kubwa: “GUARDIOLA ASEMA ANARUDI BARCELONA”

Ingawa kichwa cha habari hiyo kimemtaja Guardiola kusema anarudi Barcelona na picha yake kuwekwa mwisho wa habari hiyo akiwa kajikunyata, hakuna paragrafu yoyote kati ya 8 iliyoandikwa Guardiola anarudi Barcelona!

Aliyeandika kichwa hicho alikuwa na fikra gani? Wanaodurusu habari (proof readers) hawakuona kiroja hicho? Au siku hizi habari ikiandikwa na waandishi hakuna wanaozipitia kuhakikisha usahihi (hali ya jambo au kazi kutokuwa na kasoro au kosa) wake?

“Elimu bila amali ni kama nta bila asali.” Elimu isiyo na matendo ni kama nta isiyo na asali. Methali hii yaweza kutumiwa kumpigia mfano mtu aliyeelimika sana lakini akawa hana faida kwa watu au kwa jamii yake.

Methali: Werevu mwingi mbele kiza.

[email protected]

0784 334 096