Visawe, Vitawe na Vitate ni nini? -2

13Aug 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Visawe, Vitawe na Vitate ni nini? -2

TOLEO lililopita, tulieleza kwa kirefu baadhi ya maneno yenye maana zinazokaribiana. Mara hii twawaleteeni maana ya ‘vitawe’ yaani maneno yenye maana zaidi ya moja. Sasa endelea …

Umoja wa vitawe ni kitawe. Vitawe huchukua umbo au mofolojia –sarufi- yaani tawi la isimu linalohusika na uchambuzi na uchanganuzi wa kanuni na mifumo inayohusu upangaji wa maneno katika lugha moja lakini katika muktadha wa kimatumizi huenda kitawe kikawa na maana tofauti.

Katika matumizi ya vitawe, mzungumzaji au mwandishi ni lazima awe makini ili kuondoa utata katika sentensi au usemi wake. Ifuatayo ni mifano ya maana ya vitawe:

Chungu: kifaa cha mfinyanzi cha kupikia; aina ya mdudu mweusi; kuwa na maumivu; patikana kwa wingi. Fuma: dunga kwa mkuki au mshale; suka sweta, fulana n.k. Goma: ngoma kubwa; susia, kataa au kaidi amri. Guni: chombo cha seremala cha kukwangulia ubao au cha kupimia pembe za miraba iliyo sawa; shairi la Kiswahili lililokosa kutosheleza kanuni moja au zaidi ya ushairi wa Kiswahili.

Harija: fedha zinazotumika katika shughuli za biashara au matumizi ya nyumbani; hoja nyingi za maneno zisizokwisha. Hema: tweta, pumua kwa nguvu; kibanda cha turubali. Jaa: furika hadi pomoni; jalala, mahali pa kutupa takataka. Kaa: kipande cha kuni kilichoungua; keti; aina ya mnyama wa majini. Kama: mfano, jinsi, mshabaha; shika chuchu za mnyama na kutoa maziwa.

Kamba: uzi mnene; aina ya samaki wa baharini. Katika: vunjika, kwenye, ndani ya. Kigae: kifaa cha kuezeka paa la nyumba kilichotengenezwa kwa udongo au saruji; kipande kidogo cha chombo kilichovunjika; kigereng’enza (kipande cha chungu au mtungi uliovunjika). Kinga: zuia madhara fulani yasimfike mtu au mahali; jambo au dawa ya kujiepusha na madhara; kipande cha ukuni chenye moto au kilichoungua.

Kipepeo: kitu kinachopepea ili kuleta upepo au ubaridi; samaki mpana mwenye umbo la duara, rangi za mchanganyiko na mapezi ya nyuma mapana; mdudu mwenye umbo jembamba na mbawa pana zenye rangi mbalimbali na hupendelea kutua kwenye maua. Kuba: dari ya nyumba iliyojengwa mfano wa tao au bakuli lililofudikizwa; kaburi lililojengewa ukuta mfano wa chumba. Kuna: tumia mbuzi kusugua nazi; kuwako, kuwa huku na huku; sugua panapowasha.

Mbuzi: mnyama mdogo wa nyumbani anayefugwa kwa ajili ya nyama au maziwa; chombo cha kukunia nazi. Meza: kifaa cha mbao, chuma au plastiki cha kuandalia chakula au kuandikia; pitisha chakula kooni hadi tumboni.

Mwanamgambo: askari wa akiba aliyepata mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya ulinzi wa taifa lake lakini asiye mwajiriwa wa jeshi, raia anayejitolea kufanya kazi ya ulinzi; mpiganaji wa kundi haramu hususan la waasi. Mwari: msichana anayewekwa ndani kwa kutawishwa; mgonjwa aliyetengwa na kuwekwa ndani ili apate matibabu bila ya kuonekana na watu; bwana au bibi harusi wakati wa fungate (kipindi ambacho maharusi hukaa ndani na kuhudumiwa).

Nyanya: bibi, mama mzaa baba au mama; tunda la mnyanya ambalo hutumika kama kiungo cha mboga au kutengenezea kachumbari. Nyoka: tambazi mrefu mwembamba ambaye hana miguu, mwenye rangi mbalimbali anayetambaa kwa kunyiririka.

Paa: aina ya mnyama pori wa jamii ya mbuzi; kisusi cha nyumba; ruka kwenda angani; ambua magamba ya samaki; koka moto. Pea: aina ya tunda; kifaru; kaukiwa na sauti au potelewa na sauti; komaa, kuwa  pevu. Paka: mnyana mdogo wa nyumbani anayekula panya; tia rangi, eneza rangi kwa kitu. Panda: kwea; manati; makutano ya njia au matawi ya mti ama vidole; tia mbegu au mche ardhini; atika. Rai: bembeleza; nguvu, siha, uzima; maoni, nasaha, ushauri; lisha chakula.

Shuka: kipande cha nguo, leso au kitambaa; teremka bei au gharama; teremka kutoka mahali palipo juu kama mti, ukuta, ngazi n.k. Sijida: alama inayotokeza kwenye paji la uso kutokana na kuguswa, kwa mfano kwenye mkeka au mswala wakati wa kuswali; tendo la kuinamisha uso na kuugusisha kwenye mkeka au mswala unaposwali.

Sita: nambari au tarakimu iliyo kati ya tano na saba; babaika, kuwa na wasiwasi, kutokuwa na hakika. Somo: mtu wa jina moja na mwingine; rafiki; kungwi, mwalimu wa unyagoni. Tai: aina ya ndege alaye mizoga; aina ya vazi au kipande cha kitambaa kivaliwacho kwenye ukosi wa shati au blauzi. Tema: kata; kutupa mate au chakula kutoka kinywani. Tembo: ndovu; pombe.

Uhuni: tabia ya kuzurura mitaani, kuwasumbua watu na kufanya vitendo vibaya; tabia ya kukaa bila mke au mume. Varanga: maneno ya kutia fujo; ingilia kwa ghafla mazungumzo aghalabu yasiyokuhusu. Vua: toa nguo kutoka mwilini; opoa samaki kutoka majini; okoa kutoka hatarini.

Wamba: tandaza na funga kitu kama vile ngozi kwenye ngoma au kamba kwenye kitanda; ishiwa na fedha, kuwa katika shida ya fedha za matumizi; enea kila mahali, zagaa. Yamini: mkono wa kulia; tendo au maneno ya kuapa. Ziada: kitu kilichoongezwa; kiasi kinachobaki baada ya matumizi. Ziara: tendo la kwenda mahali fulani kwa sababu maalumu, kwa mfano kutembelea au kufanya mazungumzo fulani; kaburi. Toleo lijalo tutawaleteeni maana ya neno ‘Vitate.’

Nafasi ndogo iliyobaki tumalizie na jinsi waandishi wanavyochafua lugha ya Kiswahili: “Zahera ni fulu kicheko huko” ni kichwa cha habari kwenye gazeti la michezo. ‘Fulu’ si Kiswahili. Mwandishi angeandika: “Zahera ni kicheko tu” bila neno ‘fulu’.

Methali: Dira ya binadamu ni kichwa

[email protected]

0784  334 096