Vita hii iunganishe wanasiasa nchini

25Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vita hii iunganishe wanasiasa nchini

KISWAHILI kina methali kadhaa zenye maana sawa kama 'umoja ni nguvu utengano ni udhafu, jiwe moja haliinjiki chungu na ndege wanaofanana huruka pamoja’ ambazo zinahimiza umoja.

Methali hizi nimezilinganisha na wito ambao umetolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwa wanasiasa na wadau wa siasa, kwamba waache itikadi za vyama waungane kutoa elimu kuhusu virusi vya corona.

Wanasiasa wanatakiwa kuweka pembeni itikadi zao za kisiasa na kutumia ushawishi kuwaleta Watanzania pamoja kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo ambao unaoendelea kukatiza maisha ya watu.

Kwamba bila kufanya hivyo, ugonjwa utaendelea kusambaa na athari zake zitaonekana kijamii kisiasa na kiuchumi, kwa maana hiyo vyama na wadau wote wa siasa hawana budi kuwa kitu kimoja.

Anawataka waunge mkono miongozo iliyotolewa na serikali ili kupambana na maambukizi ya ugonjwa huo, ambao tayari umeingia nchini, hivyo vyama vya siasa viendelee kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachama na wafuasi wao kutekeleza kwa vitendo maelekezo ambayo yameshatolewa.

Umoja katika kukabiliana na tatizo la virusi vya corona ni wa muhimu na lifanye Watanzania kuwa kitu kimoja bila kujali itikadi zao za kisiasa na kusaidiana kuelimisha wengine jinsi ya kuliepuka.

Dhana ya umoja imejengwa katika kuungana, kushikamana na kushirikiana au kufanya mambo kwa nia moja hata kuwa kitu kimoja, kwani kadiri umoja unavyoimarika ndivyo nafasi kubwa ya kufanikiwa huonekana.

Kwa maana hiyo, kilichosemwa na Jaji Mutungi ni kama jukumu la wanasiasa wote kwani ni vyema Watanzania wakaacha chuki na itikadi za kisiasa na kuwa wamoja kwa kutambua kwamba umoja ni nguvu.

Mambo ya kuwafanya Watanzania wachukiane hadi washindwe kushirikiana yasipewe nafasi, badala yake umoja utawale katika vita hii ya virusi vya corona kwa kutoa elimu, ili hatimaye viishe nchini.

Jaji Mutungi anawakumbusha wanasiasa kuwa ugonjwa huo ni hatari kama wataalamu wa afya wanavyosema, athari zake zinahusu kuondoa uhai, hivyo kama taifa bila kujali itikadi za kisiasa, ni muhimu kushikamana katika kukabiliana nao.

Umoja au ushirikiano wa vyama vya siasa usiishie kuungana kwa lengo la kukikabilia chama tawala katika uchaguzi tu, bali hata kwenye mambo ya msingi kama hayo ya kupambana na virusi vya corona.

Kinachotakiwa ni vyama kujishughulisha kwa dhati na masuala muhimu ya taifa, yenye umuhimu kwa wananchi, badala ya masuala ya kibinafsi zaidi ambayo yanaweza kujenga utengano badala ya umoja.

Siamini kama nchi ilirejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, bali umoja ambao ni msingi mkubwa wa ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Hivyo wito unapotolewa wa kuacha itikadi za kisiasa na kuungana kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu madhara ya virusi vya corona, wanasiasa na wadau wa siasa wote waone umuhimu wa wito huo.

Penye wengi, pana mengi na Tanzania kuna vyama takribani 20 vya siasa na vipo vyenye ushawishi mkubwa kwa wananchi, vyote vijitose kutoa elimu ili kusaidia Watanzania kuepuka ugonjwa.

Ikumbukwe kuwa shughuli zenye mkusanyiko wa watu wengi imezuiwa kwa muda ili kukabiliana na ugonjwa huo, hivyo wakati hatua hizo zikiendelea kuchukuliwa, wanasiasa nao waungane na serikali katika vita hiyo.

Mtindo wa kubezana ambao umeanza kujitokeza kwa wanasiasa, usipewe nafasi kwani unaweza kuchangia kuwagawa na hivyo kusababisha wito wa Jaji Mutungi usizae matunda.

Kila Mtanzania kwa nafasi yake anatakiwa kuelimisha au kuelimishwa ili ajue jinsi ya kujikinga na virusi vya ugonjwa huo, kwani hiyo siyo kazi ya mtu fulani au chama fulani, bali ni jukumu la wote.

Ni muhimu kuzingatia kwamba dhana ya kuwa "umoja ni nguvu utengano ni udhahifu" ina nafasi kubwa katika kufanikisha jambo liwe la siasa au kutoa elimu wakati huu dunia inapokabiliana na virusi vya corona.

Hivyo kila mwanachama wa chama cha siasa awiwe na atumie muda wake, akili yake, nguvu zake na hekima yake kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika kutoa elimu inayomwezesha Mtanzania kuwa salama.