Vitambulisho vya BVR, NIDA ni mzigo

03Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vitambulisho vya BVR, NIDA ni mzigo

MIAKA zaidi ya miwili iliyopita, serikali ilianzisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kuipa jukumu la kukusanya taarifa kwa lengo la kutambua watu wanaoishi nchini kwa kushirikiana na vyombo husika na kutoa vitambulisho kwa raia wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Mamlaka hiyo ilipewa jukumu la kusimamia utendaji kazi kwa kuzingatia utawala bora na kutunza daftari la taifa la usajili na utambuzi wa taarifa za wahusika kwa maendeleo ya taifa.
Serikali ilichukua hatua hiyo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa utaratibu huo umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika nchi duniani, ambazo ziliamua kuutumia.
Baada ya utaratibu huu kuanza, wananchi walijitokeza kwa wingi kujiandikisha na kutoa taarifa zao sahihi na kisha baadhi ya wakafanikiwa kupata vitambulisho hivyo, huku wengine wakiendelea kuvisotea hadi sasa bila kuvipata.
Hii inatokana na changamoto mbalimbali ndani ya NIDA ambazo zilisababisha watu kushinda vituoni kuvipata huku wengine wakikata tamaa na kuamua kurudi nyumbani.
Haya yote yalitokea jijini Dar es Salaam na hadi sasa wapo watu ambao hawana vitambulisho hivyo vya taifa huku mikoa mingine NIDA haijafika kuandikishaa Watanzania kwa ajili ya vitambulisho hivyo.
Kazi ya kutoa kutoa vitambulisho ilisimama mwaka jana kutokana na kuwapo kwa kazi nyingine ambayo inafanana na ya NIDA ambayo ni ya kuandikisha wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR).
Mfumo huo ulipigiwa debe na serikali pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), unadaiwa kutumia Sh. Bilioni 149 na wananchi walikuwa wakihamasishwa kujitokeza kwa wingi.
Kama ilivyokuwa kwa NIDA, hata kwenye BVR mambo yalikuwa ni yale yale, wananchi wanajitokeza kwa wingi wanashinda vituoni bila kuandikishwa kwa sababu ya ubovu wa mashine na changamoto nyingine nyingi.
Mara mashine zishindwe kutambua vidole vya watu, mara hili mara lile, mara wengine wazuiwe kujiandikisha na kusababisha baadhi yao kukata tamaa na kuamua kuachana na vitambulisho hivyo vya kupigia kura.
Cha kushangaza ni kwamba karibu maswali yote ambayo wananchi walikuwa wakiulizwa kwenye vitambulisho vya taifa ndio yale yale ambayo waliulizwa na NEC.
Kushindwa kuona utofauti ya maswali ya NIDA na NEC ulisababisha baadhi ya watu kujiuliza kwamba kulikuwa na haja gani ya kuwapo kwa vitambulisho vya taifa na vya mpigakura?
Binafsi ninakubali kwamba ipo haja ya kujiuliza maswali mengi hasa baada ya kuwapo kwa taarifa za upotevu wa fedha ndani ya NIDA uliosababisha mkurugenzi wake mkuu, Dickson Maimu, na maofisa wengine waandamizi kusimamishwa kazi na kuchunguzwa.
Uteuzi wa Maimu, ulitenguliwa na Rais John Magufuli kutokana na kuwapo kwa malalamiko kuhusiana na wananchi kukosa vitambulisho vya taifa huku Sh. bilioni 179.6 zikiwa zimetumika.
Sasa bosi huyo amepisha uchunguzi ili kuangalia vitambulisho vya taifa kama vinaendana na fedha iliyotumika Sh. bilioni 179.6, lengo likiwa ni kubaini kama kuna ufisadi uliofanywa na watu kwa maslahi yao binafsi.
Kwa mazingira haya sidhani kulikuwa na umuhimu wowote wa utoaji wa kitambulisho cha taifa ama kuendelea na mchakato huo hasa kwa kuzingatia kwamba yale yaliyomo kwenye BVR ndio hayo hayo ya NIDA.
Ninasema hivyo kwa sababu sioni umuhimu wa kuendelea kuteketeza fedha nyingi za umma huku wananchi wakikosa huduma muhimu, hivyo NIDA na BVR zitazamwe upya.
Kitambulisho cha taifa kina umuhimu wake na kingefaa kutumika katika kupigia kurwa kwa sababu kina maelezo ya kutosha ya mhusika, hivyo kusingekuwa na vya BVR.
Mtanzania kuwa na kitambulisho cha NIDA na BVR ninaona ni kujiongezea mzigo wa matumizi ya fedha, kutokana na ukweli kwamba vingeweza kutumika hata kupigia kura badala ya kuongeza vingine.
Ikumbukwe kuwa wapo Watanzania ambao hadi sasa hawana vitambulisho vya NIDA wala BVR, kutokana na kile nilichoeleza kuwa ni changamoto zilizojitokeza katika mchakato wa uandikishaji, hivyo sioni sababu za kulazimisha kutoa vyote viwili.
Kutumika kwa Sh. bilioni 179.6 huku kukiwawapo kwa malalamiko juu ya wananchi kukosa vitambulisho vya taifa ni ishara tosha kwamba kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kupunguza mzigo huu kwa kuachana kimojawapo kati ya BVR ama NIDA.