Vitiligo maradhi yanayobabua midomo, macho, ngozi

05Jun 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Vitiligo maradhi yanayobabua midomo, macho, ngozi

VITILIGO ni ugonjwa unaosababisha kupotea kwa sehemu ya juu ya rangi ya ngozi.

Hubabua midomo, macho, ngozi na mikono.

Maradhi haya yanaathiri kiasi au kiwango chochote cha ngozi.

Aidha hujitokeza sehemu ya ndani ya midomo na hata machoni.

Katika hali ya kawaida, rangi ya ngozi ya mwili hutokana na kiwango cha chembechembe zinazojulikana kama melanin.

Ugonjwa huu wa vitiligo hutokea pale chembe hai zinazotengeneza melanin zinapokufa au kuacha kufanya kazi. Huathiri watu wote japo hali hii huonekana kwa haraka zaidi kwa watu weusi. Ugonjwa huu si hatari au kutishia uhai japo husababisha msongo wa mawazo na mtu kujihisi vibaya au kujiona ana upungufu.

Hata hivyo, matibabu ya ugonjwa wa vitiligo huimarisha muonekano wa ngozi kuwa mzuri japo ugonjwa halisi hauwezi kupona na kutoweka.

Dalili za Vitiligo

Mojawapo ni kupotea kwa rangi halisi na kuota mabaka kwenye ngozi. Tatizo huanzia kujitokeza kwenye sehemu za mwili zinazopigwa na jua zaidi kama mikono, miguu, viganja, uso na midomo hasa ‘lipsi’.

Dalili zake ni ngozi kupoteza rangi halisi, kuwa na weupe au rangi ya kijivu (gray) sehemu ya ngozi ya kichwa, kope za macho au nyusi. Kupotea kwa rangi ya ngozi ya sehemu ya ndani ya mdomo au pua. Kubadlika kwa rangi ndani ya jicho. Pia kuwa na mabaka makwapani, kitovuni na sehemu za siri.

Vitiligo huanza katika umri wowote lakini mara nyingi ugonjwa huonekana kabla ya kufika miaka 20.
Kulingana na aina ya vitiligo, mabaka huweza kutokea katika viwango vifuatavyo, sehemu nyingi mwilini.

Hii ni aina ambayo huwapata watu wengi zaidi na hujulikana kama vitiligo iliyosambaa. Ipo nyingine ya upande mmoja wa mwili, hutokea katika umri mdogo na huendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja halafu hukoma.

Sehemu moja au chache za mwili ya vitiligo aina hii hutokea eneo moja tu la mwili. Hata hivyo, ni vigumu kujua kiwango cha kusambaa kwa hali ya kupoteza rangi ya ngozi. Wakati mwingine mabaka huweza kupona bila hata ya kutumia dawa au matibabu yoyote.

Aidha mara nyingi hali ya kupoteza rangi huendelea na husambaa maeneo zaidi ya mwili na mara chache sana ngozi hurejea katika hali ya awali.

Chanzo

Ugonjwa wa vitiligo hutokea pale chembe hai zinazozalisha melanin zinapokufa au kuacha kufanya kazi. Melanini huipa ngozi, nywele na macho rangi yake ya asili. Madaktari hawajaweza kufahamu sababu ya kufa au kushindwa kufanya kazi kwa chembe hai hizi lakini hali hii huweza kuhusishwa na mfumo wa kinga ya mwili kushambulia na kuharibu kimakosa chembe hai hizi ambazo huzalisha melanin.Unaweza kurithi, kugusana na kemikali za viwandani au msongo wa mawazo
Matatizo ya vitiligo

Watu wenye ugonjwa huu huwa katika hatari kubwa ya kushambuliwa na matatatizo ya kisaikolojia na msongo wa mawazo. Huhisi kuungua zaidi na jua pamoja na saratani ya ngozi. Wana matatizio ya macho. Kadhalika kushindwa kusikia kikamilifu.

Pia hupata madhara yaletwayo na utumiaji wa madawa ya kutibu ugonjwa huu kama kukauka sana kwa ngozi pamoja na muwasho.

Matibabu

Yapo matibabu ya aina nyingi na ambayo husaidia katika kurejesha rangi ya awali ya pamoja na ubora wa ngozi japo matokeo ya matibabu hayo hutofautiana na ni vigumu kutabiri ufanisi. Badhi ya matibabu huweza kuwa na madhara makubwa kwa hiyo daktari wako huanza kwa kukushauri utumie dawa nyepesi za kujaribu kuboresha muonekano wa ngozi kama ‘make-up’.

Iwapo mgonjwa na daktari watakubaliana kuanza matibabu makubwa ya madawa basi uponyaji huweza kutumia miezi kadhaa kuonekana na wakati mwingine kutumia aiana nyingi za matibabu.

Lakini mpaka sasa hakuna dawa zinazoweza kusaidia kuzuia vitiligo kuendelea kutokea yaani kupoteza kwa chembe zinazosababisha rangi halisi ya ngozi lakini zipo dawa ambazo huweza kuboresha muonekano wa ngozi ukawa mzuri. Dawa ambayo hutumika kwa hali ya kawaida ni krimu.

Zipo aina ya krimu ambazo husaidia kurejesha rangi ya ngozi ya awali hasa kama ulianza matumizi yake mapema baada ya kuona tatizo la vitiligo. Hata hivyo, matokeo ya matumizi ya krimu hayawezi kuonekana mapema kwani huhitaji miezi kadhaa. Hata hivyo matumizi ya krimu huwa na madhara ya pembeni kama ngozi kuwa nyembamba au muonekano wa mistari mistari kwenye ngozi.

Mgonjwa anapaswa kumwona daktari mara tu unapoona hali ya kupoteza rangi ya ngozi, nywele au macho. Ugonjwa wa vitiligo hauna tiba lakini matibabu husaidia kuzuia au kupunguza hali ya ngozi kupoteza rangi yake.

Kwa hiyo tafuta daktari mwenye kufahamu zaidi kuhusu hali hii mfano bingwa wa magonjwa ya ngozi na uzungumze naye.