Vituo vya daladala nchini vizingatie usalama wa abiria

29Jan 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vituo vya daladala nchini vizingatie usalama wa abiria

MIJI mikubwa ya Tanzania, ikiwamo Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam inakua kwa kasi siku hadi siku.
Kasi ya ukuaji wake inajiotofautisha kabisa na jhaloi ilivyokuwa ukilinganishwa na miaka 50 iliyopita.

Vituo vya daladala katika barabara kuu za maeneo tofauti ya miji hasa katikati ya miji, jiji yaashiria umuhimu wa ujenzi wa vituo ndani ama pembezoni mwa barabara
Ka namna yoyote ile, ujenzi huo uzingatie msongamano wa magari na watu ili kuhakikisha kuwa unatatua matatizo ya usafii ya wahusika .
Kwa mfano, ukichukulia Jiji la Dar es Salaam ambalo lina watu wapatao milioni tano, husababisha kuwepo na mikusanyiko mikubwa katika vituo hivyo hata kuonekana kuwa ni jambo la kawaida na wakati mwingine huwa ni kero.

Baadhi ya vituo vya daladala jijini Dar es Salaam katika barabara kuu kama vile Kigogo Njiapanda, Tazara, Mwenge, ITV, Darajani- Ubungo, Buguruni na Chama vipo karibu na taa za kuongozea magari au karibu na makutano ya barabara yaani njia panda hata kusababisha foleni.
Vituo hivyo huwa na abiria wengi hasa majira ya asubuhi na jioni. Abiria husubiri usafiri wa daladala ili kwenda au kurudi watokapo kazini.
Hali hiyo husababisha daladala nyingi kupaki ovyo bila mpangilio vituoni kwani vituo vinakuwa ni vidogo na havitoshi kuhimili hali halisi ilivyo.

Hii yawezekana inatokana na udogo wa kituo ambacho hakitoshi hata gari nne kusimama kwa wakati mmoja, kwa ajili ya kushusha au kubeba abiria ikiwa ni kitendo cha dakika chache tu.
Kitendo hicho cha daladala kusimama kwa dakika kadhaa, kushusha ama kubeba abiria kinasababisha foleni barabarani.
Kazi ya ziada huwa kwa askari wa usalama barabarani (trafiki), kukaa vituoni ili kuwasimamia madereva wa daladala wanaopaki magari ovyo ama mamlaka za barabara kupanga mawe makubwa mwanzoni mwa kituo ili daladala zikapaki mbele zaidi.
Hali hii inaweza kushuhudiwa kama baaadhi yake nilivyovitaja vinaleta kero kwa abiria na wamiliki wa magari binafsi hata kusababisha foleni, kutokana na daladala kupaki barabarani ili kushusha au kubeba abiria.
Hii inatokana na hali halisi ya wenye magari kushurutishwa na kupakia abiria ili watumie sekunde chache tu kufanya kitendo hicho, bila kujali ama kuzingatia hali ya mtu kwa umri,wake mathalani mtoto, mzee, mjamzito au mama mwenye mtoto,mgonjwa na mwenye ulemavu wa aina yeyote.

Wanachokifanya makondakta wa daladala hizo ni kukwepa mkono wa sheria kwa kupakia au kushusha abiria barabarani kutokana na udogo wa kituo kilicho karibu , barabara kuu au kwemye makutano.
Mamlaka husika,Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), wazingatie ujenzi wa vituo hivyo pamoja na kuzingatia ujenzi mpya wa barabara unaoendelea katika majiji na miji mikubwa nchini.
Ujenzi wa vituo hivyo kuzingatia usalama wa vituo vinavyoingia ndani, kwa mfano kile cha Buguruni Rozana ,Makumbusho na Mawasiliano ama Simu 2000 kama kinavyofahamika.
Vituo hivi vina ukubwa wa wastani kulingana na mahitaji ama sehemu husika. Hii imeepusha foleni na msongamano unaosababishwa na wingi wa daladala katika vituo vingi.
Ujenzi wa mzunguko katika makutano ya barabara yaani 'round about' wengine huita Keep Left kwa lugha ya kiingereza, ni muhimu. Hii itasaidia kupunguza foleni katika maeneo hayo, kutokana na ukweli kuwa kitakachozingatiwa ni sheria za barabarani na madereva wote.
Nazishauri mamlaka husika zisimamie vituo hivi kikamilifu ili visigeuzwe maeneo ya biashara ndogondogo na kuvuruga malengo mazima.