Vituo vya TV za kurusha mechi viongezwe kupunguza corona

11May 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vituo vya TV za kurusha mechi viongezwe kupunguza corona

BAADA ya sasa kuwapo kwa uwezekano wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuendelea na kuumalizia msimu wa 2019/20 ambao umekumbwa na changamoto kubwa ya ugonjwa wa COVID-19, maarufu kama corona, kumekuwa na mipango na mikakati mbalimbali ili kuona inamalizika kwa usalama na amani.

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) imesema huenda ligi ikarejea tena Juni mwaka huu, lakini ikichezwa kwa mtindo ule ule wa nyumbani na ugenini, ingawa baadhi ya klabu zimeonyesha kupinga kutokana na kudai kukabiliwa na ukata, lakini mechi zilizosalia kwa kiasi kikubwa zitachezwa bila mashabiki uwanjani.

Na hii ni kutokana na kwamba pamoja na ligi inarejea, bado janga hilo lipo, lakini maisha ni lazima yaendelee na watu waendelee kuchapa kazi.

Hebu fikiria, wakati ule mashabiki wanaruhusiwa tu kwenda viwanjani, lakini kwenye vibanda umiza watu wanajazana kuangalia mechi mbalimbali za ligi, je, wakati huu ambako haruhusiwi shabiki yeyote kuingia uwanjani, zaidi ya wachezaji, viongozi, makocha, madaktari, wahudumu, walinzi na askari tu?

Ni kwamba wale mashabiki wote waliokuwa na tabia za kwenda viwanjani, sasa nao wataongeza idadi ya wale watakaojazana kwenye vibanda umiza.

Si huko tu, hata kwenye hoteli na baa mbalimbali, zitakuwa na shughuli kubwa ya kupokea wateja wengi wanaokwenda kutazama mechi.

Hii itasababisha watu wengi kuwa kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa corona kwenye maeneo ya msongamano wa watu wanaoangalia mpira.

Tukumbuke kuwa waangaliaji mpira si sawa na watu waliokusanyika kwenye mikusanyiko mingine, mara nyingi muda mwingi wanaongea, wanabishana, wanapigana vijembe, wanashikana na kushangilia kwa nguvu, wakirukaruka, hivyo ni watu ambao wako kwenye hatari zaidi.

Kwa hali hiyo, itakuwa ni kazi bure kuwakataza watu wasiingie uwanjani, lakini wanaachwa kwenye maeneo mengine wakusanyike.
Hata hivyo, ni televisheni moja tu ndiyo iliyoingia mkataba wa kuonyesha mechi hizo, ambapo wafanyabiashara hununua ving'amuzi vyao kwa ajili ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu.

Sina tatizo na hilo kwa sababu ni kweli wana haki kisheria, lakini kwa maoni yangu ni kwamba kutokana na janga hili kila kitu kinaweza kubadilika kwa kipindi hiki ili tu kulinda afya za watu na kuwafanya waendelee kujenga taifa, kufanya kazi na kulipa kodi.

Mimi nadhani kwa kipindi hiki, kwa mechi zilizobaki, Shirikisho la Soka nchini (TFF) na kampuni ya Televisheni ya Azam iliyonunua haki za kurusha mechi za Ligi Kuu wakae chini na kuzungumza ikiwezekana kuuza haki hiyo kwa vituo vingi zaidi vya televisheni kwa makubaliano maalum ya kibiashara ili nazo zijiunge nayo kwa ajili ya kuonyesha mechi hizo, hatua ambayo itapunguza msongamano wa mashabiki kwenye maeneo zinapoonyeshwa mechi.

Tumeshawahi kuona huko nyuma kwenye sherehe za kitaifa, Rais akihutubia, au misiba ya watu mbalimbali mashuhuri, televisheni zote zimeungana na televisheni moja tu kwa ajili ya kuonyesha tukio hilo.

Kwa hili pia inawezekana kufanyika hivyo lengo likiwa ni moja tu, kuepusha msongamano kwenye maeneo mbalimbali ya kuonyesha soka.

Wigo unapokuwa mpana, na televisheni kadhaa ikiwamo hata ya taifa, zikijitokeza kuonyesha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizobaki, basi hakutokuwa na misongamano mikubwa kwa sababu wengine watabaki wakiangalia majumbani mwao.

Najua kuna baadhi ya mashabiki wao hawawezi kuangalia nyumbani kwa sababu kuna utulivu, badala yake wanataka sehemu za kubishana, lakini kwa kiasi kikubwa kutakuwa hakuna misongamano na hata wamiliki wanaweza kumudu kuchukua hatua za kuwanawisha kwa sabuni na dawa, kuliko umati mkubwa ukijazana.

Wakati mwingine watu wanajazana sana kwenye vibanda umiza kwa sababu ya uchache wa maeneo ya kuonyesha mipira, hivyo televisheni kubwa nchini Tanzania zikionyesha itapunguza msongamano mabandani.

Nadhani Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, ikishiriakiana na TFF, TPLB na Azam TV yenye haki ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, wanaweza kukaa na kuliweka sawa hili ili mechi ziendelee kuchezwa na kuonwa kwa mapana zaidi huku afya za Watanzania zikiwa zimezingatiwa.