Viwanja vya Karume, Gwambina vilipitishwaje?

21Sep 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Viwanja vya Karume, Gwambina vilipitishwaje?

BAADA tu ya mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TBLB), ilitangaza kuvifungia viwanja vya Karume mjini Musoma, Mara na wa Gwambina uliopo Misungwi jijini, Mwanza kutokana na kutokidhi baadhi ya vigezo.

Na hii ni baada ya watu wengi waliokuwa wakiangalia mechi hizo kwenye televisheni kushangaa na kutoridhishwa mwonekano wa viwanja hivyo.

Ukiangalia kwenye picha za televisheni, mechi zilizokuwa zinachezwa kwenye viwanja hivyo, hali ya uwanja pamoja na wachezaji jinsi walivyokuwa wakicheza, ilitengeneza mazingira fulani yanayochekesha, kushangaza na kusikitisha kwa wakati mmoja.

Uwanja wa Gwambina ndiyo ulioanza kufungiwa, mapema tu baada ya mechi kati ya Gwambina FC dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Septemba 11, mwaka huu, mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.

Mechi hiyo iliyoonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni, ilionekana kuwashangaza wengi na mitandao ya kijamii 'ikachafuka' kwa mshangao kutoka kwa mashabiki na picha mbalimbali.

Nadhani hii ndiyo moja kati ya sababu iliyoifanya Bodi ya Ligi 'kuutia kufuli' uwanja huo.
Taarifa ya haraka ya bodi hiyo ikatoka ya kuufungia Uwanja wa Gwambina kutokana na sehemu yake ya kuchezea kutokuwa na hali nzuri, kinyume na kanuni, na pia kuitaka klabu ya Gwambina kuchagua viwanja vya CCM Kirumba au Nyamagana kwa ajili ya kuchezea ligi.

Siku mbili baadaye wasimamizi hao wa soka nchini wakaufungia Uwanja wa Karume, lakini tayari timu ya Biashara ikiwa imeshacheza mechi mbili, dhidi ya Gwambia FC mechi ya ufunguzi na kushinda bao 1-0, lakini dhidi ya Mwadui, ikishinda pia bao 1-0.

Taarifa ya Bodi ya Ligi ilisema Uwanja wa Karume umefungiwa kwa sababu ya ubovu wa eneo la kuchezea, na vyumba vya kubadilishia nguo kutokidhi vigezo.

Ukiangalia hii pia ilitokana na mechi zote hizo mbili kuonekana kwenye televisheni na mashabiki wa soka kuanza kulalamika.

Ingawa viwanja vingi vya mikoani si vizuri sana, lakini hivi vilivyofungiwa vilionekana vibovu zaidi.

Hapa najiuliza kama viwanja hivi visingeonekana kwenye televisheni vingefungiwa?
Nadhani uwezekano wa kuendelea kutumika ungekuwa mkubwa kwa sababu tayari vilikuwa vimeshaanza kutumika na kufungiwa ilitokana tu na watu wengi huhoji uhalali wa viwanja hivyo kupitishwa.

Kingine cha kujiuliza ni kwa nini Kamati ya Ukaguzi ilipitisha viwanja hivyo? Je, wakaguzi walikwenda kukagua kiwanja kwa kiwanja, au walipewa taarifa tu kuwa vipo sawa, ama walipelekewa picha ya viwanja kwa njia ya mtandao?

Pamoja na kuipongeza Bodi ya Ligi kufanya haraka kuamua jambo hili, lakini pia imetia doa kwa Kamati ya Ukaguzi wa viwanja na kuonekana haikufanya kazi yake sawasawa.

Inawezekana kamati ilikuwa inaamini Uwanja wa Gwambina uko vizuri kama ulivyokuwa ukionekana siku za mwanzo baada ya ujenzi, kwa hivyo walionekana kufanya kazi kimazoea.

Hapa kuna cha kujifunza kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi na Kamati zake kuwa zisifanye kazi kimazoea, badala yake zifanye kwa kufuata misingi, kwani kama kamati ile ingefanya ukaguzi wa kina, sidhani kama Gwambina na Biashara zingeanza kucheza mechi zao kwenye viwanja hivyo.

Na wengi wanajiuliza kama mechi zile zisingekuwa zinaonekana kwenye televisheni, basi mechi zingeendelea kuchezwa kwenye viwanja hivyo, labda pale tu siku Simba, Yanga na Azam zingekwenda kucheza ndipo kila mmoja wangeshtuka, lakini wakati huo baadhi ya timu tayari zimeshaumia kucheza kwenye viwanja vibovu.