Vyama vinadhibitije janga wapigakura kutaka rushwa?

01Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vyama vinadhibitije janga wapigakura kutaka rushwa?

MWEZI Julai barani Afrika ni wakati wa kupambana na rushwa, kila mwaka Julai 11 ni Siku ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.

Rushwa inatajwa kuwa ni chanzo cha uharibifu, udhalimu, uovu na ndiyo mzizi mkuu wa umaskini barani Afrika na mara nyingi imekuwa ikilelewa na kulindwa na viongozi wengi wa bara hili.

Kwa ujumla mara nyingi wataalamu wa kiuchumi na kisiasa barani Afrika wanaeleza kuwa viongozi wengi wa bara hili ni matunda ya rushwa kwa vile michakato ya uchaguzi inatawaliwa na kuwahonga wanaoteua, kupendekeza na wapigakura. Yote haya yanasababisha uongozi unaolinda maslahi binafsi, wazembe, wabadhirifu, madikteta na mnyororo mzima wa kudumisha na kuendeleza umaskini.

Rushwa ndiyo iliyohujumu na kuteketeza rasilimali za Afrika na kuitumbukiza katika umaskini usiokwisha, ujinga, maradhi na hali duni.

Tanzania inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa viongozi wa kisiasa hawaendelei kuwa matunda ya rushwa, msimamo huu ukisimamiwa na CCM na serikali.

Wakati huu CCM imetangaza kuwa kupiga vita rushwa ndiyo ajenda kuu na kwamba haitaruhusu viongozi wawe wabunge na madiwani na watendaji wengine wa chama wapatikane kwa njia ya rushwa. Kwa hiyo ili kuunga mkono juhudi za Afrika na serikali kutokomeza rushwa wapigakura wasiwe chanzo cha kutaka rushwa.

Ni ukweli kuwa wapo wapigakura wanaotoa shinikizo kwa kauli na kwa vitendo vyao kuwa wanategemea wafanyiwe jambo maalumu iwe kupewa hongo, nguo, vyakula na chochote ili wapate hamasa ya kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombea.
Hali hii inashuhudiwa wakati wa kuonyesha nia ya kuteuliwa na chama cha siasa ili kugombea ubunge. Ndiyo kipindi cha kukabaliana na wagombea wanaoonyesha nia wakitakiwa kutoa mlungula.

Wapigakura hutaka kupewa chochote cha ziada na kama hawatapewa pesa huona kama mgombea hana nia ya kupata dhamana anayoitafuta na huachwa kama msindikizaji wa wale `wanaojitoa mhanga’ kuwapatia ‘soda’ au ‘chai’ wapigakura.

Ni wazi wagombea wana kazi ya ziada kuvuka kiunzi cha kutakiwa kuwahonga wapigakura. Kama nchi ni ukweli usiopingika kuwa kuna janga la mpigakura kudai chake mapema akiamini kuwa mgombea anakwenda kufaidika pekee yake akiwa mbunge na wanaamini kuwa mbunge au kiongozi wa umma ni kuula na kuondokana na umaskini.

Lakini pia rushwa ya uchaguzi inayotolewa nje ya kipindi cha kampeni za uchaguzi inayolenga kuwavuta wapigakura. Hapa kuna misaada kama pesa, vifaa na hata wakati mwingine kusaidia familia zenye wahitaji.

Yote haya yanachochea wapigakura kutaka misaada ambayo wakati mwingine hutafsiriwa kama hongo ya uchaguzi nje ya kipindi rasmi cha kufanya kampeni na kwa kiasi huwafanya wananchi kutaka kupewa kitu kidogo.

Viongozi wamewazoesha wapigakura kuwapa mlungula kipindi kabla ya kutangazwa kampeni za uchaguzi kwa kufanya mambo ya kimaendeleo kwa kutumia raslimali zao au za umma kwenye majimbo yao. Hii ni rushwa kwani wananchi hupokea baiskeli, pikipiki, mabati, dawa na hata mbegu na mbolea kabla ya uchaguzi ili kuwaandaa kumchagua mhusika kuwa mbunge au diwani wao.

Hayo yote yamefanyika na inachukuliwa kama chai ya uchaguzi, lakini sasa si wakati wa kuendeleza tena jambo hili. Vyama vya siasa vijiulize ni nini kinawasukuma wapigakura kudai rushwa kwa wagombea wao?

Jawabu ni kwamba wapigakura huamua kuomba na kuchukua chao mapema kiwe pesa, sukari, kanga, sabuni, chakula au pombe, baada ya kugundua kuwa viongozi wanapochaguliwa huendeleza ubadhirifu na ufisadi. Kwa hiyo kwa vile viongozi kuanzia sasa wawe wabunge, madiwani na watendaji wengine wa serikali wamepatikana na watapatikana kwa njia halali bila mlungula wananchi hao wataacha mwenendo huo wa kuomba na kutaka rushwa wanapochagua viongozi.