Waamuzi Bongo walindeni wachezaji

15Jan 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waamuzi Bongo walindeni wachezaji

KWA siku za karibuni kumeonekana kuna aina fulani ya uchezaji wa kihuni katika soka la Tanzania ambao unaonekana kama unaanza kuhalalishwa na baadhi ya waamuzi.

Soka hili baadhi yetu tulikuwa tukiliona miaka ya nyuma kwenye miaka ya 1980, mabeki walipokuwa wakicheza kikatili, makipa wakiruka na miguu, lakini pia kulikuwa na uhuni mwingine kwenye mchezo wa soka ambao ulisababisha hata baadhi ya wazazi kuwakataza watoto wao kuingia katika mchezo huo.

Ulionekana kama vile ni mchezo wa watu wenye nguvu kama vile raga, lakini rafu zilikithiri na sheria hazikuwa ngumu sana kwa wachezaji kiasi kwamba ili kucheza soka ni lazima uwe mbabe hivi.

Baada ya soka kugeuka sasa kuwa biashara, makampuni yakawekeza fedha nyingi, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilibadilisha sheria nyingi na kuuweka mchezo huo kuwa na burudani zaidi badala ya ubabe na uhuni.

Zamani beki alikuwa na uwezo wa kukurukia miguu miwili sehemu yoyote ya mwili, na labda ikatoka kadi ya njano tu, kipa aliruka na silaha ambayo ni mguu kuweka mbele, kwa sababu tu yeye mwenyewe hakuwa analindwa, kwani hata akiguswa na kusukumwa kwa kutumia mwili wa mchezaji mwingine haikuhesabika ni faulo.

Ndiyo maana kwenye kona, kuna mchezaji kazi yake ilikuwa ni kumsukuma kipa na mmoja kupiga kichwa.

Lakini huyo atakayekwenda kumsukuma kipa ni lazima awe mbabe kweli kweli kwa sababu makipa wenyewe wa zamani walikuwa ni wababe, na watukutu na si rahisi sana kufanya hivyo.

Mabeki waliwachezea mastraika rafu za hovyo, ndiyo maana kwanza kabisa ikawekwa sheria kuwa akiwa mtu wa mwisho akicheza rafu ni kadi nyekundu, na mchezaji yoyote atakayemkwatua mwenzake kwa nyuma, wakati tayari ameshapitwa ni kadi nyekundu pia.

FIFA walitengeneza sheria kuwa rafu zitakazoachwa ni zile za kimpira, lakini yoyote ile inayoonekana kuhatarisha maisha ya mchezaji mwenzake, au 'karia' yake ya kucheza soka moja kwa moja ni kadi nyekundu.

Kwenye Ligi mbalimbali za Ulaya na hata baadhi ya nchi za Afrika, ikiwamo hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, waamuzi wamejitahidi sana kuzingatia hilo.

Cha ajabu hapa nchini, waamuzi wamekuwa bado wanachezesha soka la miaka ya 1970 hadi 1980. Katika Ligi Kuu Tanzania Bara na hata Kombe la Mapinduzi tumeona baadhi ya rafu mbaya, za kihuni ambazo waamuzi wameonekana kuogopa kutolea uamuzi.

Ifike wakati waamuzi wa Tanzania waache wachezaji wanaotaka kucheza soka, kuonyesha ufundi na burudani kwa mashabiki wapewe uhuru wa kufanya hivyo na ambao wanaona soka ni mchezo wa kihuni, kazi yao ni kutaka kuumiza wengine wapewe adhabu ya kutolewa nje.

Sikatai kuwa soka linahitaji nguvu na kupambana, hiyo inaeleweka, lakini yoyote anayependa soka na aliyecheza anajua jinsi gani ya kutumia nguvu kwenye soka na kucheza rafu ya kuhatarisha maisha ya mchezaji mwenzako. Waamuzi wa Ulaya hawa huwa hawakopeshi, rafu moja tu ya kutaka kumuumiza mwenzako ni kadi nyekundu moja kwa moja.

Hapa nchini waamuzi wamewafanya wachezaji kama ng'ombe, na kuacha wachezewe rafu za kikatili na kutisha, huku wakitoa kadi chache za njano kwa sababu ya kinachoonekana woga tu.

Mchezaji mwenye uwezo anatakiwa kunyanga'anywa mpira na mchezaji mwenye uwezo pia. Kwa sababu yeye ni mchezaji, anatakiwa pia atumie uwezo wake na nguvu zinazoruhusiwa kwenye soka na si rafu za kupigana miguu ya tumbo, kichwani, mbavuni kama wacheza karate na kung'fu, huku kukiwa hakuna uamuzi wa maana ya kuwaadhibu unaofanyika.

Kama waamuzi wataendelea kulea aina hii ya uchezaji wa kihuni wa baadhi ya wachezaji ulioanza kuzoeleka, kuna uwezekano ipo siku tutapoteza wachezaji kwa kupata vilema vya maisha au kupoteza maisha kwa sababu tu ya udhaifu wa waamuzi kuchukua hatua. Mwamuzi anapochukua hatua, wachezaji huogopa kufanya hivyo kwa kuhofia kupewa kadi nyekundu, lakini anapoachia, basi anawapa uhuru kufanya wanavyotaka.