Waamuzi wabovu nchini wanakimbiza wadhamini

06Jul 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waamuzi wabovu nchini wanakimbiza wadhamini

TAYARI Shirikisho la Soka Nchini (TFF), limetangaza kuwafungia waamuzi watatu waliochezesha mechi ya Ligi Kuu Bara, kati ya Yanga dhidi ya Azam FC, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam Juni 21, mwaka huu, timu hizo zikitoka sare ya bila kufungana.

Taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa rasmi wa mtandao ya kijamii wa TFF ni kwamba mwamuzi wa kati, Elly Sasii pamoja na wasaidizi wake, Sudi Lila na Mbaraka Haule wamefungiwa kuchezesha soka kwa muda wa miezi mitatu kwa kutoumudu mchezo huo.

Siku chache baadaye baada ya mechi hiyo, mwamuzi mwingine, Shomari Lawi, aliingia kwenye midomo ya mashabiki wa soka, pamoja na vyombo vya habari, baada ya kutomudu mchezo wa robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA, kati ya Yanga dhidi ya Kagera Sugar.

Kwenye mechi hiyo pia kulikuwa na 'madudu' mengi ambayo yalionekana, mwamuzi huyo kutoka Kigoma, akawa ndiyo gumzo kubwa kuliko mechi yenyewe.

Kwanza kabisa nitoe pongezi kwa TFF na Bodi ya Ligi kwa kutoa adhabu hiyo kwa waamuzi wanaovurunda.

Lakini hapa sijajua kama adhabu hii ni kwa sababu tu Azam iliandika barua, au hata kama isingeandika, waamuzi hao wangeadhibiwa?

Bado mpaka sasa hatujajua hatima ya Lawi na wenzake. Na kingine ninachojiuliza ni kwamba miezi mitatu waliofungiwa kina Sasii inajumlishwa na ile ambayo ligi itakuwa imemalizika?

Nasema hivyo kwa sababu zimebaki mechi chache tu msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara umalizike, na inawezekana kukaa mwezi mmoja au miwili hivi bila ya kuwa na ligi, kabla ya kuanza msimu mwingine.

TFF na Bodi ya Ligi bado hawajafafanua kama miezi ambayo haina ligi inahesabika au la. Kama inahesabika sawa, lakini kama haihesabiki ina maana inawezekana waamuzi hao wakamaliza adhabu zao na kukaa wiki kadhaa tu kabla ya adhabu yao kumalizika.

Hapa sidhani kama adhabu hii itakuwa ni adhabu au mapumziko ya kawaida.

Kwa siku za karibuni, waamuzi tena wameshaanza kurejea kwenye hali ile ambayo ilisababisha malalamiko sana kwenye Ligi Kuu Bara.

Nakumbuka baadhi ya utetezi wao ulikuwa kutolipwa stahiki zao, lakini hivi karibuni TFF iliwalipa malimbikizo yao yote na kila mmoja akadhani kuwa watakuwa makini kwa sababu awali walikuwa na msongo wa mawazo.

Haiko hivyo. Wapo baadhi ya waamuzi ambao wameendelea kuchezesha vema na kupongezwa kwa kazi nzuri. Lakini baadhi yao mambo yamekuwa ni yale yale, wakiwamo Sasi, Lawi na wengine wanaopangwa katika mechi zisizotumia macho 'mengi'.

Tukisema ni makosa ya kibinadamu ni sawa, lakini cha kujiuliza ni kwa nini makosa yao yanakuwa yakizipendelea timu kubwa tu?

Tukisema hawajui nayo pia si kweli. Hawa hawa kuchezesha mechi nyingi na kuwa makini, lakini sasa cha kushangaza wachezeshe mechi za wakubwa.

Hapa kuna tatizo ambalo TFF na Bodi wanatakiwa kukaa na kuliangalia kwa makini.

Vinginevyo miaka nenda rudi tutakuwa tukilalamika kuwa soka la Tanzania ni la timu mbili tu, Simba na Yanga.

Mashabiki watakuwa wakilalamika kuwa Ligi Kuu haina ushindani. Lakini ukiangalia kwa jicho la tatu ni kwamba Ligi Kuu Tanzania Bara na hata michuano mingine kama Kombe la FA kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa na ushindani mkubwa, lakini tatizo baadhi ya waamuzi wameonekana hawataki soka lijicheze lenyewe na aliyekuwa amejipanga sawa na mwenye uwezo siku hiyo ashinde mechi.

Baadhi ya waamuzi wameonekana kama kukariri kuwa ni lazima timu fulani zishinde hata kama hazina uwezo.

Hii ndiyo inaleta tatizo. Hii inasababisha soka la Tanzania haliaminiki. Wenzetu Kenya na Uganda wameshatoka huko. Sisi inaonekana bado baadhi ya waamuzi wetu wanaamini ni lazima Simba na Yanga washinde mechi hata kama siku hiyo hawakuwa na uwezo au wamezidiwa mbinu. Hawataki wakifungwe ili wakakae chini na kutafakari wapi wamekosea ili wajirekebishe kuelekea mechi zinazofuata.

Kumekuwa na maswali mengi kwa wachambuzi wa soka nchini ni kwa nini Ligi Kuu na mashindano mengine yanakosa wadhamini. Wakati mwingine hawataki kujitokeza kwa sababu kama hizi. Wanaona kabisa kuwa ushindani si wa haki.

Timu hasa wa mikoani wakati mwingine, pamoja na matatizo ya fedha na mishahara ya wachezaji wao, lakini zimekuwa zikijituma na kupambana, zikileta upinzani mkali zinapopambana na timu kubwa zenye uwezo wa kipesa na wachezaji wa hali ya juu, lakini wamekuwa wakiangushwa na waamuzi.

Hii haikatishi tamaa timu za mikoani zinazopambana tu, wachezaji na viongozi wake, lakini inawakimbiza wadhamini ambao wanaona kabisa wanakwenda kuwekeza sehemu yenye soka ambalo, waamuzi wanalazimisha timu gani ishinde hata kama haina uwezo na timu gani ifungwe hata kama ina uwezo.

Matokeo yake tunashuhudia aibu na maamuzi ya ajabu viwanjani, yanayofanywa na baadhi ya waamuzi wetu nchini.