Waamuzi walindeni wachezaji au mpaka wavunjane miguu?

21Nov 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waamuzi walindeni wachezaji au mpaka wavunjane miguu?

WAKATI kukiwa na mashaka juu ya uwezo wa uchezeshaji wa baadhi ya waamuzi hasa kwenye matukio ambayo yanatoa ushindi kwa timu zingine, kuna sehemu ambayo watu ni kama hawaioni au kuizungumzia sana.

Naona wachambuzi na watangazaji wengi huwa wanakuja juu pale waamuzi wanapofanya makosa ambayo yanasababisha timu inyimwe bao au ipate kimakosa matokeo.

Kuna eneo ambalo limefumbiwa macho nalo ni waamuzi kulinda afya za wachezaji. Kwa siku za karibuni nimeshuhudia mechi nyingi ambazo baadhi ya wachezaji wako huru kucheza rafu ambazo si za kiuanamichezo zinazoweza kugharimu maisha ya mwenzao kisoka.

Nimeona wachezaji wa sasa wa Ligi Kuu wanacheza soka kama lile la mtaani, la kurukiana miguu tena kwa makusudi na hatua zinazochukuliwa ni ndogo kulingana na kosa lenyewe.

Ni kama vile wachezaji wamekuwa hawawaogopi tena waamuzi uwanjani na hii ni hatari sana kwa mustakabali wa soka la Tanzania. 

Wanatawala mechi, wanafanya wanavyotaka, wanacheza wanavyotaka. Nadhani hii inatokana na waamuzi kuonekana kuwa waoga wanapochezesha mechi hizo, labda wakihofia watakosea, au kusakamwa kwenye vipindi vya michezo na hivyo kujikuta wakishindwa kutoa maamuzi ambayo ni sahihi.

Siku hizi ni nadra sana kukuta mchezaji anapewa kadi nyekundu ya moja kwa moja. Badala yake wengi ni kadi mbili za njano, tena ni baada ya mchezaji huyo kucheza rafu hatarishi zaidi ya nne.

Nimesema rafu hatarishi, sisemi zile ambazo za kimpira, kumzuia mtu kwenda kufunga au kuleta hatari langoni, ila ni zile ambazo nia ni kumuumiza mwenzake.

Unakuta mchezaji anacheza rafu mbaya za kutaka kumvunja mwenzake, lakini eti mwamuzi wanamhesabia na kumuonyesha ishara kuwa hiyo ni ya mwisho.

Ukweli ni kwamba rafu moja mbaya inaweza kumfanya mchezaji akatolewa moja kwa moja kwa kadi nyekundu na tumeona kwenye nchi ambazo soka kwao ni biashara, na ni maisha ya wachezaji, hivyo hawakubali mchezaji aonekane kuwa ni hatarishi kwa maisha ya soka ya mwenzake.

Kuna rafu mbaya nyingi zinaonekana kwenye baadhi ya mechi za Ligi Kuu ambazo zimefumbiwa macho na waamuzi na wasaidizi wao.

Na hii inatokea hasa kwa wachezaji wa timu ndogo, ambao wanaona kama ili kumzuia mchezaji staa au wa timu kubwa ni lazima umchezee rafu zisizokuwa za kimchezo, kuwakanyaga kwa makusudi, kuwapandishia miguu, kuwapiga viwiko na kadhalika.

Mfano kumpiga mtu kiwiko ni kadi nyekundu ya moja kwa moja na tuliona hilo hata hapa nchini zamani, ikitokea rafu hiyo hata mashabiki hamuulizani, lakini kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa unaweza kukuta mchezaji anampiga mwenzake kiwiko, lakini anaonyeshwa kadi ya njano tu. Hii imewafanya wachezaji wenye uwezo na vipaji kuwa waoga kwa sababu hawalindwi na waamuzi waliogeuka waoga.

Imewafanya pia wachezaji wa timu zinazoitwa au kujiita ndogo kujiona wana haki ya kucheza rafu dhidi ya wachezaji wakubwa.

Kibaya zaidi ikitokea wachezaji wa timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam wakicheza rafu hata ya bahati mbaya, itaonyeshwa na kusambazwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii na wachambuzi watashinikiza afungiwe. Lakini mchezaji huyo anakuwa amechezewa rafu mbaya nyingi kwenye mechi moja lakini haionyeshwi.

Imefika wakati waamuzi waache kuwafanya wachezaji kama wanyama, wao pia ni binadamu hivyo watendewe haki kwa kuwaadhibu wale ambao wanataka kuufanya mchezo wa soka kuwa wa kihuni.

Tusisubiri mpaka mchezaji avunjwe mguu ndipo tuibuke tuanze kuongea na kuandika, au wenye mamlaka kuanza kuchukua hatua.