Waamuzi watende haki mechi Simba, Yanga

15Feb 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waamuzi watende haki mechi Simba, Yanga

NCHI inatarajia 'kusimama' kwa dakika 90 Jumamosi ijayo kupisha mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Ni mechi inayogusa hisia wa Tanzania wengi ndani na nje kutokana na sababu za kihistoria.
Klabu hizi ndizo zenye wanachama, mashabiki na wafuasi wengi kuliko zingine.

Inasadikiwa kuwa kila timu inaweza kuwa na wafuasi wasiopungua milioni 20.
Hata wale wanaooneka kuwa hawapendi au kujihusisha na mambo ya soka, lakini ukimbana sana, utagundua kuwa ni mfuasi kati wa moja kati ya timu hizi mbili.

Timu hizo zitakuwa uwanjani kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza Yanga kuifunga Simba mabao 2-0.

Kwa miaka ya karibuni tumeona kuwa tatizo kubwa la wanachama na mashabiki wa timu hizi kuzimia uwanjani, au wakati mwingine kupoteza maisha iwe uwanjani, au sehemu yoyote ile wanapofuatilia matangazo ya mechi au kuyatanzama kwenye luninga.

Kutokana na haya yote niliyoyaeleza kuna, umuhimu mkubwa kwa wale watakaopewa dhamana ya kuwa mahakimu kwenye mechi hiyo kuchezesha kwa haki, uadilifu na kufuata sheria zote 17.

Lengo hapa ni kupunguza mihemko ili mshindi apatikane kwa haki na si kwa kulazimisha.
Pamoja na umati wa mashabiki wanaofurika uwanja wa Taifa, lakini timu yoyote ile inayofungwa kihalali hukubali matokeo na kurejea nyumbani kwa amani, wakiwaacha wenzao wakishangilia.

Mfano mwaka 2012, Simba iliifunga Yanga mabao 5-0, lakini mashabiki wake walikubali matokeo kutokana na kwamba waamuzi walichezesha kwa kufuata sheria zote.

Hata hivyo, kuna baadhi ya mechi kati ya timu hizo mbili kumekuwa na maamuzi ambayo yanatia shaka.
Sitaki kwenda mbali sana, mechi iliyopita kati ya timu hizo mbili mwamuzi Israel Nkongo, pamoja na ukogwe wake hakulitendea haki pambano hilo kutokana na baadhi ya maamuzi yake.

Sina maana kwamba alikuwa akiibeba timu moja kati ya hizo mbili, la hasha ila aliachia kwa makusudi au kwa kutokuwa makini baadhi ya rafu ninazoziita za kipuuzi za wachezaji wa timu zote mbili bila kuchukua hatua yoyote.

Kuna matukio ya wachezaji kupigana viwiko, kichwa, lakini mwamuzi hakuchukua hatua yoyote ile.
Alionekana kutoa kadi za njano kwenye rafu za kimchezo, lakini kutotoa kadi zozote kwenye rafu ambazo si za kiungwana.
Moja kati ya majukumu ya mwamuzi pamoja na kuchezesha kwa kufuata sheria ni kuwafanya wachezaji wanaotaka kutoa burudani uwanjani wawe huru ili kufurahisha mashabiki na watu wote ambao wamelipa kiingilio kwa ajili hiyo.

Hata hivyo, kuna baadhi ya waamuzi wameshindwa kuwalinda wachezaji wa aina hiyo mbele ya wachezaji wakorofi, watukutu ambao wanaotumia mbinu chafu kuwazuia wenzao.

Matokeo yake wachezaji wanaingia woga kutokana na kwamba hawalindwi na waamuzi pamoja na kuchezewa rafu, hivyo na wao kuanza kucheza soka la kubutua kiasi cha kusababisha ladha yote ya mchezo kupotea.

Pia visasi vinaanza na kuifanya mechi nzima sasa kugeuka kuwa ya kibabe badala yake burudani.
Kitu cha kushangaza kwenye mechi kati ya timu hizi mbili unaweza kuona wachezaji wenyewe wametulia na kucheza soka bila tatizo, lakini waamuzi tena wa wenye beji ya FIFA wao ndiyo wanaonekana kuwa presha zaidi.

Natoa rai kwa waamuzi watakaochezesha mechi baina ya timu hizo Jumamosi kujua wana jukumu la si kutupatia mshindi halali, lakini pia kutoa maamuzi sahihi pale tatizo linapotokea.

Waamuzi wengi hasa kwenye mechi hizi kubwa wana tatizo la kutotoa adhabu kwa rafu kubwa upande mmoja, baadaye upande mwingine ukirudishia wanaacha kwa sababu waliacha ile ya kwanza ya wapinzani wao.
Hapo ndipo maamuzi ya utata yanapoanza kushamiri uwanjani.

Haipendezi kuona watu wanazirai au kupoteza maisha uwanjani chanzo kikiwa waamuzi.
Iwe hivyo kutokana na mwenendo wa mechi au matokeo tu basi kama itatokea ingawa hatuombei hilo.
Kila la kheri waamuzi watakaochezesha pambanao hilo.