Waandishi tuache kushabikia vilabu

09Sep 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waandishi tuache kushabikia vilabu

‘UMBEA’ ni tabia ya kutoa habari bila ya kutumwa au kuulizwa; udaku, udakuzi; tabia ya kufuatilia au kusikiliza habari za watu wengine bila kutumwa.

‘Uchochezi’ ni tabia ya mtu kutia fitina baina ya watu ili wazozane; uchonganishi; chokochoko. Pia ni tabia ya kuwaambia watu uongo ili wapate kugombana, kutukanana au kupigana.

Soma hii: “Ngoma, Tambwe mmoja kutimka.” Lengo kumpisha mkali wa hat trick ni yule aliyekinukisha Ligi
ya Mabingwa Afrika.

Hiki ni kichwa cha habari katika ukurasa wa mbele wa gazeti la michezo kikipambwa na picha moja kubwa ya mchezaji ambaye bado hajasajiliwa na Yanga. Ubavu wake wa kuume kuna picha mbili ndogo ya Tambwe juu na chini yake ni picha ya Ngoma wakiwa katika tabasamu.

Ukurasa wa pili wa gazeti hilo, habari hiyo imeandikwa kwa kirefu ikitumia paragrafu 13. Hata hivyo ni paragrafu moja tu ya mwisho ndiyo unakuta maelezo yanayowahusu Ngoma na Tambwe. Paragrafu nyingine 12 zaeleza sifa za mchezaji Sabelo Ndzinisa wa Mbabane Swallows FC ya Swaziland anayetakiwa na Yanga.

Paragrafu inayowahusu Ngoma na Tambwe imeandikwa: “Lakini iwapo atatua Jangwani, ni wazi kuwa kati ya Donald Ngoma na Amisi Tambwe, mmoja wao atalazimika kufungashwa virago ili kutoa nafasi kwa mshambuliaji huyo (Ndzinisa) kusajiliwa na mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara.” Huko juu nimeanza kueleza kwa kirefu maana ya ‘umbea’ na ‘uchochezi’ ili wasomaji waamue kama gazeti husika lilivyoandika ni umbea au uchochezi.

Ndzinisa hawezi kusajiliwa kwa sababu hajamaliza mkataba wake na Mbabane Swallows.

Aidha, Yanga haiwezi kumsajili sasa kwani hata kama ataonekana kuifaa klabu hiyo, itabidi isubiri mpaka mkataba wake na Mbabane Swallows utakapomalizika.

Wakati huo pia dirisha dogo la usajili nchini litakuwa limefunguliwa, hivyo kuiwezesha Yanga kusajili.
Haijawekwa bayana na viongozi wa Yanga kwamba kati ya Ngoma na Tambwe mmoja wao atafungashiwa virago kama ilivyoelezwa na gazeti hilo!

Haya, gazeti lingine la michezo likaandika kwenye ukurasa wake wa mbele: “Kwa Chirwa, Ngoma na Ajib zilipendwa.” Kisha paragrafu ya kwanza ikaandikwa ifuatavyo:

“Kurejea kwa Obrey Chirwa katika kikosi cha Yanga kunamaanisha kwamba kombinesheni ya Ibrahim Ajibu
na Donald Ngoma imegeuka kuwa zilipendwa.

“Kwa uhalisia ulivyo, Chirwa atawatenganisha mastaa hao kiuchezaji hasa kutokana na matokeo ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Lipuli, lakini wanaweza kuwamo kwenye kikosi cha kwanza kwa nafasi tofauti.” Wakati mwingine waandishi wa habari za michezo huandika kwa ushabiki, kuwatia wasiwasi wachezaji au kuleta kutoelewana baina ya wachezaji au na benchi lao la ufundi.

Hebu fikiri mchezaji anapoandikwa bila kificho kuwa mchezaji fulani akisajiliwa, mwingine aliyeko ataachwa, atakuwa na ari ya kucheza? Hebu ona hii:

“Mchezaji fulani akisajiliwa, kocha atapata taabu kupanga safu yake ya ushambuliaji/ulinzi
kwani wote wana viwango sawa.” Kwa kuandika hivyo, ni kuwatia hamasa wachezaji kujibidisha zaidi kila mmoja kutaka kuwa bora kuliko wenzake, badala ya kuwakatisha tamaa.

Vilevile waandishi wanapaswa kuwauliza wahusika, yaani walimu (makocha) kwa sababu ndio wanaojua umahiri na udhaifu wa wachezaji wao. Kumwuliza mtu asiye na utaalamu wa kandanda, viongozi au msemaji wa
klabu si sahihi.

Mambo yanayohusu klabu aulizwe Katibu Mkuu maana yeye ndiye mtendaji mkuu wa klabu si Mwenyekiti wala Mweka Fedha.

Hushangazwa na baadhi ya waandishi wanapowauliza wasemaji wa vilabu kuhusu mechi ijayo kama watashinda au la!
Wasemaji wa vilabu si makocha wa timu tena hawawezi kusema watashindwa, bali watatoa maneno mengi ya kujitapa na kujiaminisha kuwa lazima watashinda! Nadhani wengi tulimsikia Muro wa Yanga na Manara wa Simba walivyokuwa wakiitana majina ya ‘wa mchangani,’ ‘wa matopeni’ na ‘wa kimataifa.’

Mfano wa karibuni ni Bwire, Msemaji wa timu ya JKT Ruvu lakini mwishowe timu yake ilifungwa mabao 7-0 ilipokutana na Simba kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Wahenga watwambia “Kila mlango una ufunguo wake.” Kwa kawaida kila mlango huwa na ufunguo wake maalum. Methali hii yatufunza kuwa si vizuri kufananisha mambo au hata watu kwa kuwa kila jambo au mtu huwa na sifa zake au uwezo wake tofauti na mwenzake. Huwezi kuvifananisha vipawa vya watu wawili.

Ni muhimu tuandike habari bila kutia chumvi.

Tuondokane na ushabiki, tuache chuki kwa vilabu tusivyovipenda, na tuwaulize watu wanaostahiki tukiwaepuka wale wasemao “usiandike jina langu kwa kuwa mimi si msemaji wa klabu!”

Kama wajua wewe si msemaji wa klabu ni sababu zipi zinakufanya utoe taarifa ilhali pilipili ziko shamba?
[email protected]

0715/0784 33 40 96