Waandishi wanapotosha Kiswahili

08Nov 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Waandishi wanapotosha Kiswahili

UANDISHI au uandikaji ni shughuli inayohusu masuala ya kuandika kama vile habari, makala au kitabu. Maneno ni matamshi, yaani namna mtu anavyosema.

Kitamkwa ni sauti inayowakilishwa kwa herufi. Kwa hiyo kitamkwa kimoja tu katika neno kinapotamkwa au kuandikwa visivyo huweza kuleta maana tofauti.

‘Hafla’ na ‘ghafla’ ni maneno mawili yenye maana tofauti. ‘Hafla’ ni shughuli inayofanywa kusherehekea jambo maalumu. ‘Ghafla’ ni neno linaloeleza utokeaji wa jambo bila kutazamiwa.

Twapaswa kuwa makini katika uandishi. ‘Sukari’ iitwe hivyo badala ya ‘tamu!’ Nani asiyejua sukari ni tamu? Au ‘limau’ kuitwa ‘ugwadu.’ Kuna matunda ya aina tofauti yenye ugwadu.

Matumizi ya maneno yasiyo kwenye msamiati wa Kiswahili huwafanya wasomaji kutoelewa maudhui (wazo kuu linaloelezwa katika maandishi au katika kusema). Kuchanganya lugha ni kuwakanganya (duwaza mtu asijue la kufanya) wasomaji kutoelewa kilichoandikwa!

Katika makala zangu (Kiswahili, michezo, siasa, maradhi n.k.) hutumia maneno ya Kiswahili yasiyotumika sana na kuyatolea maana yake. Hufanya hivyo kuwaonesha wasomaji kuwa kuna maneno mengi ya Kiswahili yasiyotumiwa na badala yake hutumiwa maneno ya mitaani yasiyoeleweka au kuchanganya Kiswahili na Kingereza!

‘Inahuu?’ Neno hili lilikuwa kichwa cha habari ukurasa wa kwanza na wa tatu kwenye gazeti la michezo. “Inahuu? Mwacheni bebi wangu Tambwe.”

‘Bebi’ ni neno lililotoholewa kutoka Kiingereza, (baby). Maana yake ni mtoto mchanga; mdogo katika familia au kikundi. ‘baby carriage’ ni gari la mtoto; ‘baby talk’ lugha ya kitoto.

‘Bebi’ ni neno linalotumiwa siku hizi na wapenzi wanapodanganyana. Mwanamke humwita mwanamume ‘bebi’ au mwanamume humwita hivyo mwanamke. Badala ya kuambiana hivyo, waitane ‘laazizi’ yaani rafiki wa kike au wa kiume; mwandani, mpenzi. Maana ya ‘azizi’ ni kitu cha thamani.

“Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Property International inayodili na masuala kuthaminisha ardhi, Salehe Omary …”

Neno ‘inayodili’ pia limetoholewa kutoka Kingereza yaani ‘deal.’ Ni neno linaloweza kutumika kwa namna tofauti lakini kwa muktadha huu, lina maana ya ‘shughulikia,’ ‘jihusisha,’ ‘ongelea,’ ‘husu.’

Sentensi ya mwandishi ingekuwa: “Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Property International inayothamini ardhi, Salehe Omary …”

“… kuna watu walikanyagana, wengine walizimia kwa hofu, wengine wakataka kugongwa na magari.” Maana moja ya ‘taka’ ni kuwa na haja ya kitu au jambo fulani, tamani kitu; hitaji.

Lugha ya Kiswahili ina methali nyingi zinazotokana na neno ‘taka.’ Mtaka cha mvunguni sharti ainame, mtaka nyingi nasaba hupata mingi misiba, mtaka unda haneni, mtaka yote kwa pupa hukosa yote, mtaka vingi kwa pupa hana mwisho mwema n.k.

Hebu tujiulize: Kuna watu ‘waliotaka’ kugongwa na magari? Kwa nini ‘walitaka’ wagongwe? Hawapendi kuishi? Kama ‘walitaka kugongwa na magari, basi wana kesi ya kkujibu kwa kujaribu kujiua!

Mwandishi angeandika: “… kuna waliokanyagana, waliozimia kwa hofu na walionusurika (kitendo cha kuokoka kutoka kwenye hatari) kugongwa na magari walipokuwa wakikimbia vurugu.”

Deni si jukumu wala jukumu si deni kama alivyoandika mwandishi wa gazeti moja la michezo. Kwa kuwa maelezo yake yana maneno 76 katika sentensi moja, nitatumia sehemu tu.

“ … na fedha nyingine zote zitapewa umuhimu wa nafasi ya kwanza katika matumizi ya kukamilisha majukumu ya zamani ya klabu hiyo ambayo yalijilimbikiza na hayakuwa yamelipwa.”

Jukumu (nomino) li/ya (ma) ni dhima aliyonayo mtu juu ya jambo fulani. Kwa mujibu wa sentensi ya mwandishi, ‘majukumu’ hayalipwi bali kinacholipwa ni deni/madeni. Sentensi yake inathibitisha hilo ilipoandikwa “ … yalijilimbikiza na hayakuwa yamelipwa.”

Kichwa cha habari cha gazeti hilohilo kiliandikwa: “Yanga SC ‘itabugi’ ikimtimua Pluijm.” Neno ‘bugi’ lina maana mbili. i) ulozi unaofanywa na wezi wa kufungua milango ya nyumba kimazingaombwe au kuroga walio kwenye nyumba kulala usingizi mzito; ii) ngoma ichezwayo Uswahilini na Wakwere.

Sehemu ya tahariri ya gazeti hili iliandikwa: “Nipashe inachukua fulsa hii kuwakumbusha mashabiki na wanachama wa klabu hizi kushangilia timu zao kwa amani bila kuwapo kwa vitendo vyovyote vitakavyochochea uvunjifu wa amani na uhalibifu wa mali za uwanja huo uliojengwa kwa pesa nyingi.”

Kwa ufupi hakuna neno ‘fulsa’ wala ‘uhalibifu’ bali ni ‘fursa’ na ‘uharibifu.’ Hakuna wanaodurusu habari/makala kabla ya kuchapishwa? Kama wapo, macho yao huingia kiwi (hali ya kutoona vyema kutokana na kutazama kitu kinachong’aa sana)?
Methali: Asiyeuliza hana ajifunzalo.
[email protected]
0715/0715 33 40 96