Waandishi wanawake wanasahaulika kiajira

21Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waandishi wanawake wanasahaulika kiajira

UANDISHI wa habari ni moja ya fani muhimu kwenye jamii kwani ni daraja linalounganisha na kufikisha taarifa kutoka kwa watoaji na kuwapelekea wananchi.

Jukumu hilo ni nyeti kutokana na ulazima wa binadamu kuhabarika na taarifa muhimu na za mara kwa mara katika mazingira na dunia anayoishi.

Dhana hii ya upashanaji habari ni ya karne nyingi kwa vile ilianza kwa kutumia michoro na picha zilizochorwa mapangoni na hata kwenye mawe ili kufikisha ujumbe kwa jamii ama kundi fulani.

Na hilo lilidumu kwa miongo mingi kutoka kizazi kimoja hadi vingine hadi ujio wa sayansi na teknolojia ulioboresha mawasiliano kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Kutokana na umuhimu huo ndiyo maana miaka ya hivi karibuni kumekuwa mabadiliko makubwa katika tasnia ya uandishi na usambazaji wa habari yanayoletwa na TEHAMA.

Yote hayo yamechangia kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanaume na wanawake kwenye tasnia hiyo. Na wote hao wamejikita katika kutafuta maarifa na taaluma ili kuifikishia jamii taarifa sahihi na kwa wakati kwa kutumia ujuzi walioupata madarasani na teknolojia wezeshi.

Katika safari ya kutafuta taaluma hii ya uandishi wa habari, kumezuka changamoto kubwa ya upatikanaji wa ajira rasmi kwa wahitimu hasa kwa wanawake.

Mathalani, baadhi wameijikuta wakiingizwa kwenye mahangaiko makubwa ili wapate ajira mahali fulani walipo patamani.

Hili limechangia kushusha morali yao ya kuthamini kile walichojifunza wakiwa darasani na umuhimu wake kwa jamii.

Lakini, wanawake wanazidi kukata tamaa kwa vile wengi hawaaminiki katika tasnia hiyo na kuwaona kama watu wa ajabu hasa wakishika kamera na kazi nyingine ambazo zimezoeleka kuwa ni za wanaume. Kimazoea wanawake walikuwa wakihusishwa na usomaji wa habari na siyo vitengo vingine.

Na hili mara nyingi limekuwa likiathiri taaluma yao kwasababu ya kupangiwa nini cha kufanya na kile cha kutokugusa.

Zaidi waandishi wa habari wa kike wamejikuta wakiathirika na ukosefu wa ajira na kuangukia kwenye kufanya majukumu mengine ambazo si za taaluma hiyo.

Mbali na hayo ukosefu wa ajira kwa wasichana waandishi umefanya fani hiyo kuathirika kwa kukosa wanafunzi wapya, kwani wengi wao wamekuwa wakikataa kujiunga kwa kisingizo cha kuepuka kusota bila ajira kama ilivyo kwa watangulizi wao.

Hali hii pia inachangia waandishi kutothaminiwa wala kupewa kipaumbele kama zilivo kazi nyingine, na upatikanaji wake wa ajira kuwa mgumu hususani kwa wanawake na kutokana na imani zilizojengeka katika jamii kuwa uandishi wa habari soko lake la ajira limekuwa dogo likilinganishwa na sekta nyingine.

Wanahabari waathirika wanaiomba serikali na asasi binafsi, kupanua wigo wa ajira ili wasichana waandishi waongezeke kwenye fani hii muhimu.

Pia taasisi nyingine za fedha ziwe tayari kuweka mazingira bora ya kutoa mikopo nafuu kwa vijana na hasa waandishi wa habari wa kike ili kuwawezesha kuanzisha kampuni zao binafsi na kujiajiri kusaidia kujikwamua na pia kuajiri wengine.

Ni raia yangu kwa waandishi wanafunzi walio kwenye mafunzo au wanaotarajia kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kujiepusha na tabia zinazoharibu maadili yao na kujidhalilisha ili kuweka mazingira ya kuajiriwa baadae.

Ninalisitiza hili kwasababu chanzo cha kushamiri tatizo la ukosefu wa ajira kwa waandishi wengi wa kike ni matokeo ya kujifunga katika mienendo isiyo ya kimaadili na kusababisha wasiajirike.

Naamini kwa kupitia makala hii, wahusika wote wataliangalia kwa jicho la karibu tatizo hili la ukosefu wa ajira kwa waandishi wa habari wa kike na kuja na muarobaini wa kulimaliza.