Waathirika mnaotibiwa  msirudie kula mihadarati

28Jun 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waathirika mnaotibiwa  msirudie kula mihadarati

MATUMIZI ya dawa za kulevya yamekuwa yakipingwa kwa nguvu zote, kutokana na kwamba yana athari kubwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo kiafya, kiuchumi na hata kijamii.

Ili kuhakikisha jamii inaepuka janga hilo, serikali kwa kushirikiana na wadau wa mapambano dhidi ya dawa hizo, imekuwa ikifanya kila njia, ambayo itasaidia kukomesha matumizi na biashara hiyo nchini.

Taarifa za serikali zinasema kwa sasa matumizi ya dawa hizo yamepungua kwa asilimia 90, na pia Tanzania ni ya kwanza katika nchi za Afrika za Kusini mwa Jangwa la Sahara kuanzisha vituo vya matibabu kwa waathirika wa dawa hizo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ndiye anakaririwa na vyombo vya habari akisema hayo wakati akifungua mkutano wa 28 wa wakuu wa vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya, kutoka nchi 54 za Afrika.

Mkutano huo ulifanyika Septemba mwaka jana, jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu alieleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya nchini yameathiri sekta mbalimbali ikiwamo ya afya, uchumi na jamii.

Anaongeza kwamba uchunguzi unabainisha kuwa kati ya asilimia 10 hadi 50 ya watumiaji wa dawa za kulevya wana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), na kushauri nchi za Afrika kuweka mkakati imara wa kudhibiti dawa hizo.

Nikirejea kwenye hoja ni kwamba, jana ilikuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya, ambayo hufanyika kila mwaka Juni 26.

Maadhimisho ya mwaka huu yana kaulimbiu isemayo: "Waathirika wa dawa za kulevya wana haki ya kupata huduma ya afya", kwa maana kwamba kila mwathirika anaweza kwenda katika kituo cha matibabu na kupatiwa huduma.

Kimsingi ni kwamba serikali imefanya juhudi kubwa katika kukomesha matumizi na biashara ya kulevya nchini, kinachotakiwa sasa ni wauzaji wa dawa hizo kufanya biashara nyingine halali.

Kwa upande wa watumiaji, nao watambue kuwa dawa hizo ni hatari kwa afya zao hivyo wajitenge nazo ili kuepuka madhara mengine ya kiafya, ambayo wanaweza kuyapata yakiwamo ya ugonjwa wa akili.

Serikali imeanzisha vituo vya matibabu kwa waathirika wa dawa hizo, wahusika wavitumie inavyotakiwa badala ya kwenda kupewa huduma  ya afya na kisha wanarudi mitaani na kuendelea kutumia dawa za kulevya.

Hivyo ni vyema wanaofanya hivyo watambue kuwa kwenda kupata huduma  vituoni na kurudia matumizi ya dawa za kulevya ni sawa na kushindwa kutumia haki inayotajwa katika kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu.

Pamoja na juhudi za serikali na wadau wengine kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya vinakoma nchini, inasemekana baadhi ya watumiaji wabuni mbinu nyingine baada ya kuona wamebanwa.

Inaelezwa kuwa baada ya kuona wamebanwa, sasa baadhi ya watumiaji, hasa vijana wanatumia sumu ya kuua panya na kuitumia kama dawa ya kulevya kwa kuichanganya na dawa nyengine haramu za kulevya kama bhangi na kuvuta.

Hiyo inatokana na kwamba sumu ya panya inapatikana kirahisi katika maduka ya bidhaa za nyumbani na sokoni, na huuzwa kwa bei ndogo, hivyo watumiaji baada ya kubanwa wakaamua kugeukia huko.

Watumiaji na wale wanaojiandaa kujiingiza katika matumizi hayo watambue kuwa dawa za kulevya, ni janga linalotishia maisha ya vijana na kuathiri nguvukazi ya taiafa ambayo ni vijana.

Walioathirika na dawa hizo wanajikuta wakipoteza dira ya maisha na taifa kukosa mchango wao unaouhitaji sana na wanakuwa watu wa kutegemea badala ya kujitegemea.

Badala ya vijana kujikita katika shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wao wameamua kujiingiza katika utumiaji na uuzaji wa dawa ya kulevya na mwisho wa siku wahusika pia wanajiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Aidha, wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya Duniani, jamii na taasisi zisizo za kiserikali, kila upande ushiriki kikamilifu katika vita ya dawa za kulevya.

Watumiaji wa dawa za kulevya wapo mitaani, wanajulikana, wasaidiwe ili waunge mkono juhudi za serikali za kupambana na dawa hizo kwa kwenda vituo vya matibabu, na wauzaji watajwe wachukuliwe hatua za kisheria.