Wachambuzi wajitafakari kumpeleka Ajibu Simba B

23Mar 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wachambuzi wajitafakari kumpeleka Ajibu Simba B

KWA muda wa wiki nzima nilikuwa nasikia vipindi vya michezo kwenye redio mbalimbali nchini. Moja kati ya mada zilizokuwa zinavutia na zilizovutia wasikiliza wengi ni mchezaji wa Simba, Ibrahim Ajibu kudaiwa kupelekwa kikosi cha pili cha timu hiyo.

Baadhi ya wachambuzi walikuwa wakielezea jinsi mchezaji huyo alivyoshuka kiwango baada ya kurejea Simba kutoka Yanga. Lakini wapo waliosema kuwa Ajibu ni mvivu wa mazoezi, hivyo ni lazima kiwango chake kiteremke, hivyo si ajabu kupelekwa kikosi cha pili.

Kwangu binafsi haikuwa habari mpya kwa Ajibu kuwa mvivu wa mazoezi, au kutojituma. Hili nilikuwa nalisikia tangu mchezaji huyo yupo Simba, kabla hajaelekea klabu ya Yanga.

Pamoja na hayo bado alikuwa akicheza soka la aina ile ile, siku anaweza kucheza vizuri, siku nyingine akaamka vibaya. Huyo ndiyo Ajibu ninayemjua mimi.

Hajawahi kucheza kwa asilimia zote msimu mzima kama walivyo wachezaji wengine kama kina Meddie Kagere, Kevin Yondani, na wengineo. Watoto wa mjini wanasema maji kupwa maji kujaa. Na tayari hata mashabiki wa soka wamemzoea hivyo. Hakuna jipya. Nikajiuliza ni kwa nini mada hii ipo?

Kumbe kuna gazeti moja la michezo liliandika kwenye kichwa chake cha habari kuwa 'Ajibu apelekwa Simba B.' Wachambuzi wakawa wanawauliza mashabiki ni kwa nini na wao wanadhani kimesababisha Ajibu kupelekwa huko?

Kabla hata kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck na viongozi wa klabu hioyo hawajakanusha taarifa hiyo, mimi tayari nilikuwa nimeshalisaka gazeti hilo na kusoma.

Nilichoshangaa ni kwamba kilichoandikwa humo ni tofauti na kile ambacho baadhi ya wachambuzi wa soka walichowekea mada kwenye vipindi vyao.

Kumbe chini ya kichwa kile cha habari kumeandikwa kuwa Kocha Sven alikuwa ameandaa mechi ya kirafiki kati ya kikosi cha Simba ambayo wachezaji wake hawapati sana namba kama vile kina Ajibu, Gerson Fraga, Haruna Shamte, Rashid Juma na wengine wacheze dhidi ya Simba B.

Lengo la kocha ni kuwafanya wachezaji ambao hawapati namba kwenye kikosi cha kwanza na wao kutokaa muda mrefu bila kucheza. Nikawa sasa nimeelewa maana ya ile habari kuwa 'Ajibu amepelekwa Simba B.'

Sasa nikawa najiuliza, hivi kweli wachambuzi wetu walipata muda wa kupitia habari ile kabla ya kuweka mada hiyo?

Kwa vyovyote vile, wachambuzi wetu wanaonekana kuwa waliweka mada kwa kusoma tu kichwa cha habari, bila kutafuta kwanza gazeti na kusoma kilichoandikwa ndani. Si vizuri na wala si haki kuweka mada kwenye vipindi kwa vitu vya kudhani au ambavyo havijafuatiliwa vizuri.

Hii ni kwa sababu wengi waliokuwa wakifuatilia mada hizo, walidhani ni kweli Ajibu anapelekwa Simba B, kumbe anakwenda kucheza dhidi ya Simba B, akiwa na kikosi cha wachezaji wanaokaa benchi.

Baadhi walimponda Ajibu kwa kuonekana kuwa ameshuka kiwango hadi kusababisha hayo na wengine kumlaumu kocha Sven kwani hawakuamini kwamba mchezaji huyo ameshuka kwa kiwango kikubwa namba hiyo hadi kupelekwa huko, kwa kitu ambacho si cha kweli.

Binafsi kama nilivyosema hapo awali kuwa sikuwa na shaka na kilichozungumzwa juu ya uvivu wa Ajibu na baadhi ya mambo mengine yanayozungumzwa juu yake, kwa sababu yanaeleweka.

Nilichokuwa ninashangaa ni kule kusema kuwa amepelekwa kikosi cha pili, wakati ukweli siyo huo. Hapa baadhi ya wachambuzi wetu walikuwa wamewapiga wasikilizaji wao 'changa la macho.'

Nawakumbusha tu wachambuzi kama wanataka kuweka mada yoyote ambayo wanaitoa kwenye gazeti, basi walitafute na wasome neno kwa neno kabla ya kupeleka kwa wasikilizaji, badala ya kuweka mada kwa kuangalia kichwa cha habari tu.