Wachezaji kuweni makini na mikataba ya usajili

13Jun 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wachezaji kuweni makini na mikataba ya usajili

WIKI iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kalenda ya usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara na Ligi Daraja la Pili.

Kalenda hiyo ni mwongozo kwa viongozi wa klabu na wachezaji ambao wanasajiliwa kwa ajili ya kuzitumikia timu mbalimbali zinazoshiriki ligi hizo mbili.

Ligi Kuu ambayo inatoa wawakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika na michuano ya Kombe la Shirikisho wakati Ligi Daraja la Kwanza mbali na kupandisha nyota mbalimbali wanaosajiliwa na klabu za Ligi Kuu, pia inasaidia kutoa wachezaji kwa ajili ya timu za taifa.

Kutangazwa kwa kalenda hiyo, sio tu kwa ajili ya kutimiza wajibu wake, bali ni maalum kwa ajili ya viongozi na wachezaji kufanya mchakato wa usajili kisasa.

Usajili unapofanyika kisasa, unasaidia kutoa nafasi kwa wachezaji na klabu kufahamu hatima yake katika msimu unaofuata. Kubwa ikiwa ni kujipanga kuwa na vikosi imara kwa ajili ya kupambana na si kuwa wasindikizaji wa baadhi ya timu.

Klabu inapofanikiwa kuwa makini kwenye mchakato huu wa awali, hapana shaka kwamba, itakuwa na msimu mzuri na itaonyesha ushindani katika kila mchezo.

Moja ya mambo muhimu ambayo wachezaji na klabu zinatakiwa kuzingatia ni kuhakikisha kila upande uafanya uamuzi sahihi katika kutangaza wachezaji inaowaacha.

Kipengele hiki kilionekana kusumbua wachezaji zaidi, hasa pale klabu inapowatangaza kuwaacha, huku muda wa usajili ukiwa umemalizika.

TFF iliamua kuweka kipindi hiki hasa kwa kuzingatia masilahi ya wachezaji ambao mara kwa mara wamejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuachwa dakika za mwisho.

Baadhi ya wachezaji waliachwa katika mazingira kama ya kuwakomoa kwa vile hawakuwaeleza mapema kama watawaacha.

Pia wachezaji wengine huachwa katika dakika za lala salama kutokana na klabu kupata mchezaji mwenye kiwango cha juu, hivyo thamani ya nyota huyo wa zamani kupotea.

Ni vizuri klabu zikafanya usajili kwa kutuata taratibu husika zinazoongozwa na kalenda ya TFF.
"Ukisema cha nini, mwenzio anasema atakipata lini", viongozi jaribuni kuwa na uamuzi wa busara na wakati mwingine chukueni uhusika wa wachezaji katika mioyo yenu.

Na wachezaji, si dhambi kuamua kuvunja mwenyewe mkataba na klabu pale unapobaini kuwa kipaji chako kinaweza kufa au hupati kile ulichotarajia. Tumeshuhudia baadhi ya nyota wakikubaliana na baadhi ya timu kuvunja mikataba yao kwa busara badala ya kung'ang'ania kile kisichowezekana.

Mbali na kusajili, pia TFF imeelekeza muda wa timu kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa mwaka 2016/17.
Baadhi ya timu zilizoshiriki msimu uliopita, mojawapo imeshuka daraja, kocha wake aliwahi kueleza kuwa hakupata nafasi ya kucheza mechi hata moja ya kirafiki. Jambo hili halikuwa sahihi, timu haiwezi kutoa ushindani wakati ligi inapoanza.