Wachezaji wa Kibongo mnakwama wapi?

20Jun 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wachezaji wa Kibongo mnakwama wapi?

KWA misimu kadhaa sasa kila ukija wakati wa dirisha la usajili wa wachezaji, neema inaangukia zaidi kwa wachezaji kutoka nje ya nchi na si wazawa.

Klabu kubwa kama Simba, Yanga na Azam zinakuwa zikipigana vikumbo kusaka wachezaji wa kigeni kwenye mataifa mbalimbali.

Siku hizi utakuta klabu hizo zikipigana vikumbo kwenda kusajili mpaka wachezaji kutoka Rwanda, na Burundi ambapo kwa miaka ya 1980, ilikuwa si tu ni aghalabu, ila haiwezekani.

Ni kwamba wakati huo Tanzania ilikuwa na wachezaji wengi wenye vipaji kuliko Rwanda na Burundi. Wachezaji wa Tanzania walishindana kwa ubora na wachezaji wa Zambia, Kenya, Uganda, Malawi, Nigeria, Guinea, Zaire (sasa DRC) na Ghana.

Kadri misimu inavyozidi kusonga mbele, binafsi nilianza kuhisi kuna kitu kitatokea mbele ya safari na kweli kimeanza na huko tunakokwenda misimu ijayo itakuwa ni hatari zaidi.

Nilianza kuona taratibu klabu kubwa na zenye uwezo kipesa kama Simba, Yanga na Azam zinakuwa zikiangalia zaidi wachezaji wa kigeni na si wa Kitanzania kwa jili ya kuunda timu zao.

Inavyoonekana zimeshaona ili ziwe na msingi mzuri ni lazima zisajili wachezaji wa kigeni, na baadaye kusajili wazawa kama vile kuongezea, au kutimiza idadi inayotakiwa ya wachezaji kuanzia 25 hadi 30.

Nadhani wakati mwingine kuna timu zinasajili wachezaji wa Kitanzania kwa sababu tu ni lazima wasajiliwe, yaani kuna idadi ya mwisho iliyowekwa ya wachezaji wa kigeni, la sivyo kama wangeruhusiwa basi ama wangesajili wote wageni, au wazawa wasiozidi watano tu.

Huko nyuma klabu za Simba na Yanga zilikuwa zikigombea wachezaji wazawa hapa hapa nchini, lakini sasa zimegeuka, zinagombea wageni.

Kumbuka zilivyokuwa zikiwagombea kina Malimi Busungu, Said Bahanuzi, Ramadhani Singano, Kelvin Yondani, na wengineo, lakini kadri misimu ilivyozidi kusonga mbele hali ikazidi kubadilika.

Mfano mzuri msimu huu, Yanga imetangaza kuwa itasajili wachezaji wasiozidi au kupungua wanne wa kigeni tu basi.

Ina maana kwenye usajili msimu huu wa Yanga wachezaji wa Kibongo hakuna mwenye nafasi ya kusajiliwa. Pamoja na jitihada zao zote za kucheza soka kwenye klabu mbalimbali ili waonekane, lakini nafasi hakuna.

Kwa sasa nafasi ipo za Simba na Azam tu kwenye klabu zenye pesa nzuri, ambako hata huko nako nina uhakika kuna nafasi chache sana za wazawa. Kama hali ikiendelea hivi, kuna msimu unaweza kukuta Simba, Yanga na Azam zote hazitosajili mchezaji yeyote wa Kibongo.

Viongozi wa klabu hizi wanafanya makusudi? Hapana, ni kwa sababu wanaona hakuna wachezaji wa viwango ambavyo wanavihitaji kwenye timu zao.

Pamoja na kudaiwa kuwa ligi imekuwa ngumu na wachezaji wamejituma sana msimu huu, lakini bado hakuna viwango vya wachezaji wengi wa Kitanzania ambavyo vingeshawishi klabu hizi kushtuka.

Hata huyo George Mpole ambaye amekuwa na msimu mzuri, bado ni kama vile klabu hizo zina mashaka naye, kwani wachezaji wa Kibongo wameonekana ni kama maji kubwa na kujaa, msimu huu anaweza kucheza hivi na msimu ujao vile.

Nasikia Simba wanamnyemelea, na hii ni kwa sababu tu msimu huu wataondoka mastraika wengi kutokana na kuonekana kushuka viwango, vinginevyo hata huko asingepata nafasi.

Yanga ilifanya usajili kipindi cha dirisha dogo kwa kuwachukuwa, Denis Nkane kutoka Biashara United na Chrispin Ngushi, kutoka Mbeya Kwanza waliokuwa wanafanya vema, lakini mpaka sasa hakuna maajabu makubwa waliyofanya, cha maana wakiwa huko. Mchezaji pekee ambaye ameonyesha mafanikio ni Salum Aboubakar 'Sure Boy'.

Hii inaonyesha kuwa bado wachezaji wa Kitanzania wana safari ndefu sana na inabidi wajiulize wanakwama wapi?

Yupo shabiki mmoja alisema Taifa Stars haifanyi vema kwa sababu Ligi Kuu ya Tanzania ina wachezaji wengi wageni. Mwenzake akamjibu mbona timu ya Algeria nayo haina wachezaji wa Ligi Kuu ya Algeria? Swali lake likafa hapo hapo. Ina maana Algeria ilitumia wachezaji wengi kutoka nje ya nchi.

Hivyo, ufumbuzi wa ubishi wao ukawa wachezaji wa Kitanzania nao watoke waende wakacheze soka nje ya nchi. Nasikitika kusema kama hapa kwenyewe Tanzania wengi wao si mhimili katika klabu zao hasa kubwa, unadhani kweli wengi wao wanaweza kucheza kwa mafanikio nje ya nchi?

Wanaweza kuwaweka nje wazawa na huko na kucheza wao kama wanavyofanywa huku? Wachezaji wa Kitanzania ukiwatazama wana vipaji vikubwa sana, lakini kuna sehemu wanakosea. Ni wavivu wa mazoezi, hawajali, hawana mwendelezo, hawaifanyi soka kama ni kazi kama zingine za ofisini, na si wavumilivu.

Haya ni machache tu yanayowafanya wachezaji wa Kitanzania leo hii kuwa wa kujazia tu nafasi kwenye timu. Kibaya zaidi tunaona sasa hata klabu ndogo za Coastal Union, Biashara United, Geita Gold, Mtibwa Sugar na zingine zimeanza kushusha wachezaji wa kigeni ambao wameonekana kujitofautisha na wazawa hata huko. Hii nayo ni kengele ya hatari kwao, wasipojirekebisha utafika wakati hata huko kupata namba kwao itaanza kuwa shida.