Wafugaji wetu wabadilike waendeshe ufugaji wa tija

05Sep 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Wafugaji wetu wabadilike waendeshe ufugaji wa tija

MIGOGORO ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima ni moja ya changamoto kubwa ambayo imeikabili nchi kwa muda sasa kutokana na jinsi ambavyo imekuwa ikiibuka kila mara huku na kule na kusababisha maafa kati ya makundi hayo mawili.

Kimsingi si jambo geni kusikia yameibuka mapigano kati ya makundi hayo mawili na hasa kwenye mikoa ya Morogoro, Arusha, Manyara, Tanga na mingine kadhaa licha ya kuwapo kwa jitihada za kuimaliza changamoto hii.

Lakini sasa angalau hali imetulia kidogo kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kumaliza tatizo hilo, ambalo kimsingi lilikuwa linaitia doa nchi hii inayosifika kwa amani.

Wakati huu ambao hali imetulia ingekuwa ni vyema sasa zitafutwe mbinu zitakazomaliza migogoro hii moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wafugaji kuachana na mtindo wa kufuga mifugo mingi na badala yake wafuge katika kiwango kitakachowaletea tija.

Hilo likifanyika ninaamini wafugaji pia wataachana na mtindo wa kuhamahama kwenda kutafuta malisho na maji kutokana na wingi wa mifugo, hasa ng'ombe ambao umekuwa ukisababisha ugomvi kati yao na wakulima wakidaiwa kulisha kwenye mashamba ya wakulima.

Kwa mtazamo wangu wafugaji walio wengi ni kama vile wachungaji kwa namna wasivyofaidika na wingi wa mifugo yao, hivyo ni vyema wakaachana na aina hiyo ya ufugaji, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Huu ni wakati wa kuwaelimisha wafugaji waimarishe maeneo yao, ili yawe vyanzo vya malisho ya mifugo yao kwa kuyawekea miundombinu ya mifugo kama vile malambo, majosho na visima ili kukabiliana na changamoto mbalimbali kama za upungufu wa maji na malisho.

Waelimishwe kupunguza wingi wa mifugo, ili waweze kubaki na michache, ambayo wanaweza kuimudu, kwani katika mazingira hayo itakuwa ni rahisi kwao kutulia sehemu moja badala ya kuhangaika kufuata malisho na maji sehemu nyingine.

Binafsi ninaamini kwamba haimsaidii mfugaji kuwa na mifugo mingi, ambayo wakati mwingine hufa hovyo kwa sababu ya njaa au katika kadhia za mapigano ya kugombea ardhi kati yao na wakulima.

Ng’ombe wakiwa wachache na pia wakawekewa miundombinu yote inayohitajika kwa ajili ya mifugo itawasaidia wao kuachana na mtindo wa wa kuhama ovyo ambao umekuwa kama jadi yao.

Hatua ya kupunguza wingi wa mifugo itasaidia pia kulinda mazingira.

Ikumbukwe kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye wingi wa mifugo ya asili, lakini cha kushangaza wafugaji wengi wanaishi maisha ya kimaskini kana kwamba hawana mali.

Ripoti ya ufugaji katika Ofisi ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa zaidi ya kaya milioni 2.3 zinategemea ufugaji kama njia kuu ya kujiongezea kipato, lakini cha ajabu mifugo imeshindwa kubadilisha maisha ya kaya hizo.

Na badala yake zimeendelea kuwa kaya za wafugaji tu, mfumo ambao kwa kweli unapaswa ubadilishwe, ili ziwe kaya za kisasa kwa kubakiwa na mifugo michache, ambayo wanaweza kuihudumia kikamilifu na hata kuchangia kwenye pato la taifa.

Ripoti ya NBS inaonyesha kuwa Tanzania ina zaidi ya ng'ombe ya milioni 21.3, mbuzi milioni 15. 2, nguruwe 1.6 na kondoo milioni 5.7, lakini bahati mbaya vyote hivyo inasemekana havijakidhi mahitaji ya soko la nyama na maziwa.

Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kinakiri kwamba ukosefu wa maeneo rasmi ya malisho, migogoro kati yao wafugaji na wakulima ni moja ya changamoto kubwa inayolikabili kundi hili.

Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu wa CCWT, Magembe Makoye amekuwa akizunguka mikoa mbalimbali na kuhamasisha wafugaji kupunguza wingi wa mifugo, ili kubaki na michache na kuwataka wasione fahari kuwa na mifugo mingi isiowanufaisha.

Lakini lingine la kuelimishwa ni katika kuwafahamisha watu wote wakiwamo wafugaji juu ya umuhimu wa rasilimali ardhi.

Kwamba ardhi ni rasilimali inayohitajika kwa maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi na pia kwa ajili ya binadamu na mifugo yao, hivyo isimamiwe kikamilifu, ili kuhakikisha migogoro inakomeshwa moja kwa moja.

Ninaamini Tanzania bila migogoro ya ardhi inawezekana iwapo wafugaji watabadilika na kupunguza wingi wa mifugo na pia iwapo maeneo ya makundi hayo yataainishwa, ili wahusika wasiendelee kuathiriwa na migogoro ya ardhi.