Wagombea wote upinzani Shinyanga kuenguliwa kunavyozidisha maswali

22Sep 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wagombea wote upinzani Shinyanga kuenguliwa kunavyozidisha maswali

UCHAGUZI mdogo wa diwani wa kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao baada ya kifo cha David Nkulila, umeanza kwa vimbwanga vya washiriki wote wa upinzani kuangukia pua, kwa maelezo kuwa hawakikidhi vigezo.

Diwani Nkulila, aliyekuwa pia Meya wa Manispaa ya Shinyanga, alifariki dunia Agosti mwaka huu na sasa uchaguzi wa kuziba pengo lake utafanyika Oktoba 9 na ndivyo mchakato unavyoanza.

Waliojitokeza, lakini wakaenguliwa na kumbakiza mgombea wa CCM pekee Victor Mmanywa, wanatoka vyama vya Demokrasia Makini, ADC, SAU, NLD, UMD, CCK, CHAUMMA, NRA, DP na ACT-Wazalendo.

Kuenguliwa kwa wagombea 10 kutoka vyama vya upinzani, kuwania nafasi hiyo kunatokana na kile kinachoelezwa na msimamizi wa uchaguzi huo kuwa ni kutokidhi vigezo vya kugombea udiwani kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 9, mwaka huu.

Hayo yanafanyika Shinyanga, wakati Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa ameshatoa maelekezo kwamba ni muhimu sheria zikazingatiwa ili zisitumike kuwanyima watu haki kwa madai kuwa wanashindwa kuandika au kokosea majina yao.

Rais alisema mtu anapokosea kuandika baadhi ya herufi za jina lake au za chama chake, kisiwe kigezo na kwamba mipango ingewekwa vizuri ili asiengulie, lakini akawataka wagombea nao kuwa makini wanapojaza fomu.

Ni wakati akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 iliyowasilishwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kutoa wito huo ili kwamba wagombea waweze kuchukuana kwenye kinyang'anyiro, badala ya kuwapo malalamiko ambayo wakati mwingine si ya lazima.

Rais aliwataka wagombea kuwa makini wanapojaza fomu ili wasiache nafasi ambayo itawafanya wapinzani wao kuitumia kuwaengua katika kinyang'anyiro.

Alichosema kilitakiwa kuwa somo hata kwa wanasiasa waliojitokeza kuwania udiwani wa Kata ya Ndembezi, ili kwamba makosa yasijirudie kama ambavyo yamekuwa yakifanyika katika uchaguzi mbalimbali.

Kwa mfano, sababu ya kuenguliwa mgombea wa ACT-Wazalendo aliyekuwa ameteuliwa rasmi na kupewa barua ya uteuzi imeelezwa kuwa hakujaza fomu namba 8 (c) na namba 10 (c) na kuzirudisha NEC kwa wakati.

Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa chama hicho Shinyanga Mjini, Omary Gindu, anasema mgombea wao alikuwa tayari amepewa barua ya uteuzi, lakini wa CCM akamwekea pingamizi, Mvano Idd, ambaye atakata rufani, ili jina lake lirejeshwe kwenye kinyang'anyiro.

Mapingamizi kama hayo yalitokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ambayo huenda yangekuwa fundisho kwa wagombea ili wawe makini katika ujazaji wa fomu za kuwania udiwani au ubunge.

Lakini kama ni makosa ambayo aliyagusia Rais Samia na kutaka yarekebishwe, ingependeza wasimamizi wakasaidia kuwarekebisha wagombea kwenye kasoro hizo za kawaida, ili hatimaye wapate nafasi ya kushiriki kwenye kinyang'anyiro.

Hatua hiyo, inaweza kusaidia kuleta hamasa katika uchaguzi badala ya watu kupita bila kupingwa, hali ambayo wakati mwingine inaweza kusababisha wagombea na kudhani hawana nafasi ya kuchaguliwa.

Mbali na hilo, hata kelele za mara kwa mara za wapinzani ambazo zinajitokeza wakati wa uchaguzi kudai kuenguliwa, kunyimwa fomu au kutopokelewa fomu zao, zinaweza kutapungua.

Pamoja na hayo, upinzani utakuwa umekosa hoja ambazo huelekezwa kwa wasimamizi wa uchaguzi kuwa mamia ya wagombea wao huenguliwa ili kuwapa ushindi wa 'mezani' wagombea wa CCM.