Wajasiriamali mboga mjali afya za wateja wenu jamani!

20Nov 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wajasiriamali mboga mjali afya za wateja wenu jamani!

NI msimu wa mvua. Kila mahali hasa kwa wakazi wa mikoa ya Pwani kuna msamiati mvua, ukizidi kupanuka katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Ni mvua na hata simulizi ya mafuriko, huku barabara zimeharibika, kule kilio cha madaraja, ili mradi majanga tu.

Wadau wakuu wa hali ya hewa wiki iliyopita, wanatudokeza kwamba na tusishangae, likawapo kwa wiki zaidi. Mafuriko hayo yanatokana na maendelezo ya mvua zinaendelea kuonyesha hivi sasa.

Kuna tahadhari zinazotolewa kwa kila mtu anao wajibu wa kuchukuwa hatua za kujihami hata kupata shida zitokanazo na athari zake. Hapo ni mimi na wewe ndio tunaotakiwa kuchukua hatua na kamwe sio mtu mwingine kwa niaba yako. Kuwa sehemu tu mapambano.

Jamii kutokana na mvua zinazonyesha, watu wanatakiwa kuzingatia masuala ya usafi na kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.

Hapo niseme kuna baadhi ya watu wasiowapenda wenzao au kutowatakia neema katika kipindi hiki cha mvua wanakitumia kutapisha ‘chemba’ za vyoo vyao na kuzuia tafrani ya kiafya, huku wakijua wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria na hata kijamii.

Kanuni na sheria zote tunazifahamu na mamlaka zetu, hadi ngazi ya serikali za mitaa zinahimiza hilo. Sasa, kulikoni mtu anaona ni bora kutafuta watu wamzibulie ili awapatie pesa kidogo, badala ya kukodi gari la kutoa huduma ya kunyonya vyoo.

Hivi sasa, mtu anayefanya hivyo ajue hamtendei haki jirani yake na umma unaonzunguka na hata tafsiri na zaidi ya hapo.

Ukija kwa wenzetu wanaouza matunda, mboga na bidhaa za aina mbalimbali, nao wanajua vizuri kipindi hiki na namna wanavyotakiwa kuchukua tahadhari za kiafya.

Hapo unakuta mvua inanyesha, ikimpa ishara kwmba anahitaji kuhifadhi bidhaa zake kwa ubora. Tujiulize wanalitenda hilo? La hasha, hata kidogo!

Umma huo wa wajasiriamali wanaotulisha, wengi wanashindwa kabisa kutekeleza kigezo hicho muhimu katika ujasiriamali.

Ni jambo linalofanyika,wakiwa waelewa wazuri wa dhana kama maradhi ya tumbo, kuhara, kichocho na hata kilio cha kipindupindu.

Unakuta mtu anajua umuhimu wa kumjali mteja na kufanya hivyo, lakini hajengi mazingira rafiki katika namna ya kuuza, kama vile kuziosha.

Ukija kwenye vitafunwa, hapo ni kazi haviosheki na vilevile vimeachwa katika namna hatarishi. Wauzaji wanawaza pesa tu, ndio wanaowakimbilia.

Ndani ya mvua hizi, ndio wakati sahihi kwa wafanyabiashara kubuni mbinu sahihi za kujihami.
Bila kufanya hivyo, ni kujimaliza na mvua ni kitu kilicho endelevu, hakikwepeki, bali cha kupambana nacho.

Kinachotakiwa kikuu ni kujiongeza kama mvua itanyesha nini kinatakiwa kufanyika na sio kuendelea kutoa huduma katika maeneo na namna isiyofaa.

Jijini Dar es |Salaam, eneo la Mabibo, kuna soko la ndizi, biashara ikiwa imeshamiri na kuna matope mengi yamejaa mahali hapo.

Mahali hapo kuna mengi zaidi ya mikungu ya ndizi imejaa kwenye matope, sambamba na bidhaa nyinginezo.