Wajasiriamali ni sawa biashara, vipi usafi nao?

15Sep 2020
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wajasiriamali ni sawa biashara, vipi usafi nao?

KATIKA maeneo yenye mikusanyiko ndiko kuliko na fursa nyingi kuanzia za kibiashara hadi za kisiasa, ndiyo maana wajasiriamali wengi wanapatikana maeneo ya sokoni, vituo vya mabasi vya mijini na majijini, njiapanda, kando ya barabara, viwanja vya michezo, shuleni na hata ufukweni.

Wafanyabiashara hawa ambao ni wajasiriamali wadogo, huuza vyakula, vinywaji, mavazi na bidhaa za nyumbani, ambao pamoja na serikali kuwapa vibali kama vitambulisho vya kufanya biashara maeneo haya, kuna changamoto ya usafi na utunzaji wa mazingira yanayozunguka kazi zao.

Kwenye vituo vya daladala, mfano Makumbusho, Gongo la Mboto na Mbezi vilivyoko Dar es Salaam, utashuhudia taka na uchafu na kinachoonekana ni sawa na kusema kuwa hawajali wala kuzingatia usafi ila wanasaka pesa kwanza.

Pia, maeneo ya soko Tandika, Kariakoo, Manzese, Tandale na Buguruni hali ya uchafu ni hiyo hiyo na kwa ujumla masoko hayo hayapendezi machoni. Mtu ni afya, kuzitunza afya za wateja na unayeuza bidhaa ni kitu muhimu.

Ingekuwa ni bora fursa iendane na wajibu, sababu nafasi wamepewa wajasiriamali hawa ambao kundi kubwa ni vijana, siku hizi Kiswahili cha mjini wanasema 'kujiongeza', jiongezeni kwenye usafi.

Wafanyabiashara mjiongeze katika maeneo yenu kwa kila mmoja kuwa na ndoo au kapu la kutunza takataka zinazotokana na bidhaa mnazouza, si sawa hata kidogo uzalishe uchafu kwenye biashara zako kila dakika usubiri watu waje kukufagilia.

Kuna ambao watasema tunalipa ushuru. Ni sawa ushuru unalipwa, lakini akija mfanya usafi akute pa kuanzia, ikiwezekana taka zimetunzwa mahali fulani azikusanye na kumalizia kufagia.

Ni sawa na ukilipia ushuru, uache eneo chafu au mazingira machafu. Mbona katika vyoo vya kulipia utalipia ushuru wa Sh. 300 hadi 500 lakini baada ya kutumia choo iwe haja ndogo au kubwa utamwagia maji? Ni wachache wasio na uelewa wakaacha choo kichafu na kumfanya anayekuja nyuma yake arudi nyuma kama ameona chatu chooni.

Vivyo hivyo, hata wanaokuja kufanya usafi katika maeneo yenu ya biashara iwe soko au vituo vya daladala ni watu kama wengine, ambao wanahitaji kukuta utaratibu uliowekwa na wewe mzalisha uchafu kisha zikabebwa na gari taka hadi dampo.

Kituo pekee cha mfano wa kuigwa ni Simu 2000 au maarufu Mawasiliano kilichoko Dar es Salaam, kutokana na kupiga marufuku biashara katika kituo hicho.

Ni vyema wajasiriamali, wafanyabiashara kuweni rafiki wa mazingira kwa kuwa wasafi na pia wekeni vyombo vya kuhifadhia taka ngumu na si kuzitupa ovyo mitaroni barabarani.

Hii inawachanganya wafagizi wa barabara, ambao hutumia matoroli, ufagio na koleo, ili kuzoa mchanga akishafagia, huchanganyikiwa anakutana na maganda ya miwa, ndizi au chupa za maji yote hufanyakazi kuwa ngumu zaidi, kwani analazimika kuzoa mchanga na taka ngumu.

Wafanyabiashara hiyo ndiyo ajira isiyo rasmi, lakini inatambulika kwa kuziwezesha familia zenu kupata mahitaji na ni maendeleo pia kwa nchi, lakini kumbukeni mtu ni afya na maofisa afya na wajumbe wa kamati za afya na mazingira kwenye sehemu zao waongeze usimamizi, ufuatiliaji na kuchukua hatua kwa vile kama hamtaziba ufa mtajenga ukuta.

Kuna kipindi zilianza kampeni za kuwa na utaratibu wa kutumia sheria ndogo ndogo utakaowezesha kuwatoza faini wanaochafua mazingira ikiwa ni pamoja na kutupa taka ovyo na wanaojisaidia haja ndogo. Wakosaji wangelipishwa Sh. 50,000 papo kwa papo, mikakati hiyo iliishia wapi? Kama inawezekana kuna sababu ya kuangalia upya suala la tozo za papo kwa papo.