Wajenzi wa mabondeni, nini haki na wajibu wako kisheria?

18May 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Wajenzi wa mabondeni, nini haki na wajibu wako kisheria?

MVUA zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali na atahri zake zimeonekana. Mionzi ya Sheria leo inajikita kujibu swali la msingi hapo juu.

Ni vyema  kuanza  kuyajua makundi ya ardhi yanayotambulika kisheria.

Kwa ajili ya usimamizi na utawala wa ardhi, Sheria ya Ardhi nchini Tanzania, (The Land Act Cap. 113), ya mwaka 1999 inaigawa ardhi katika makundi matatu:  Ardhi ya jumla; Ardhi ya Vijiji'; na Ardhi ya Hifadhi.

Ardhi ya jumla, ni ambayo haiangukii miliki ya vijiji au hifadhi. Hii ni miongoni mwa ardhi inayosimamiwa na Sheria ya Ardhi ya 1999 na kiutendaji inasimamiwa moja kwa moja na serikali.

 

Ardhi ya Vijiji: Ni maeneo yaliyo ndani ya kijiji kinachotambulika kisheria na inasimamiwa na serikali ya vijiji. Hii ni pamoja na ardhi iliyo ndani ya mipaka ya vijiji, ambayo imesajiliwa chini ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Local Government Act) 1982; 'ardhi iliyo chini ya vijiji vilivyoanzishwa chini ya Sheria ya Makazi (Village Settlement Act) 1965'.

Pia, kuna ardhi iliyotengwa kama kijiji, kwa lengo maalum na kuwekewa mipaka kwa kufuata sheria zilizowekwa; ardhi yoyote ambayo mipaka yake imekubaliwa na Serikali ya Vijiji husika, hasa pale ardhi hiyo ilikuwa na mgogoro.

Pia, katika kundi hilo la wamiliki ardhi, wanaingia wanakijiji wanaoimiliki kwa muda wa miaka 12 au zaidi kabla ya kupitishwa Sheria mpya ya Ardhi mwaka 1999'.

 

Ardhi ya Hifadhi: Ni iliyotengwa kwa madhumuni maalum. Hii ni pamoja na Hifadhi ya Misitu inayotambulika kisheria; mbuga za wanyamapori; hifadhi za majini, ikihusisha bahari, mito, mabwawa makubwa na maziwa'; 'hifadhi za barabara; maeneo ya wazi ya kupumzikia, burudani, michezo na starehe; na, ardhi hatari.

Mifano ya hai ni mabondeni, penye miteremko mikali, kingo za mto, maziwa na bahari, sehemu zilizotengwa kutupa taka, mito na miamba baharini.

Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, kupitia Kifungu cha 6(1) (d)] na Sheria ya Ardhi ya Vijiji; Kifungu cha 6(1)-(11)], zote kwa ujumla wake zina tamko kuhusu ardhi hatari.

Inaitafsiri: “Ardhi Hatari' ni ambayo si salama kwa maisha ya ama binadamu au viumbe vingine, au utumiaji wake unaleta uharibifu wa mazingira.”

Kabla ya haijatangazwa kuwa ‘Ardhi Hatari’' kama Sheria Kuu ya Ardhi inabainisha, wanaomiliki ardhi hiyo wapewe nafasi kutoa maelezo, yatakayozingatiwa katika kufikia maamuzi.

 

Baada ya uamuzi wa kuitangaza sehemu yoyote ya ardhi kuwa ‘Ardhi Hatari, wamiliki wote kisheria hulipwa fidia kulingana na sheria inavyoelekeza kwa wakati huo, pia inatangazwa katika Gazeti la Serikali, ili kuufahamisha umma wa Watanzania.

Tamko la Sheria Rasmi

Kifungu cha 57(1) cha Sheria elekezi ya mazingira kinasema, hakuna atakayeruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu za kudumu ndani ya mita 60, ambazo kwa asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira au utunzaji bahari au kingo za mto, bwawa,  na miamba ya asili ya ziwa.

 

Hiyo ni sawa na kusema, serikali kwa kupitia mamlaka zake zenye dhamana, moja kwa moja, inawajibika kuhakikisha raia wake wanaendeleza makazi na ikiwemo kuendesha shughuli zao za kila siku katika mahali salama na halali kwa mlengwa huo.

 

Sheria ya Usimamizi wa Mazingiraya Mwaka 2004), inatamka kuwa Waziri mwenye dhamana, anaweza kuweka miongozo ya kuendesha shughuli za binadamu ndani ya maeneo husika.

 

Hivyo basi, kwa ujumla wake kinachosisitizwa ni kwamba mtu ataruhusiwa kuendeleza makazi katika ardhi isiyokuwa hatarishi tu na siyo kinyume na mazingira hayo. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Mwaka, 1999.

Pia, Sheria ya Mipango Miji, inatamka mtu hataruhusiwa kuliendeleza eneo lolote lililopimwa kwa mujibu wa sheria, bila ya kwanza kupatiwa kibali maalum toka kwa mamlaka husika, kwa kuzingatia masharti yanayoambatana na kibali husika.

 

Ni utaratibu unaojitokeza katika Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999.

Muhimu

Sheria inaenda mbali zaidi kwa kutoa mwanya kwa raia kuiomba mahakama kutoa ‘’amri ya hafueni’’ pale atakapotakuwa na mamlaka yenye dhamana kuondoka katika eneo, kutokana na sababu za kisheria.

Haki hiyo ni imo chini ya Sheria Elekezi ya Mmasuala ya Ardhi.

Angalizo ni kwamba, kwa Kifungu chake kidogo cha 9 (a)-(c): Maombi haya ya kuiomba Mahakama kutoa ‘amri ya afuheni’ kamwe hayatachukuliwa kwamba mwombaji hana haki ya msingi juu ya eneo lake.

 

Mfano hai,  rejea hatua ya Mahakama Kuu katika mwaka 2016, kukubali kupokea, kusikiliza na kutolea maamuzi Ombi la Wakazi wa Mabonde ya Kinondoni, waliopipinga hatua ya serikali kuvunja nyumba zao kwa lazima na kuwataka kuhama bila ya fidia.

Hitimisho

Kimsingi, fidia ya ardhi ni stahili ambayo mmiliki wake anapaswa kulipwa, pale tu ardhi yake inapotwaliwa. Yaweza kuwa kwa matumizi ya serikali, binafsi au hata kwa ya aina nyingine yoyote ile, ambayo kwa tafsiri itakuwa ni ‘kwa manufaa ya umma.’

 

Kwa kuwa basi, mmiliki halali wa ardhi ndiye pekee kisheria ana haki ya kudai fidia, anaweza kuwa mtu binafsi, kampuni, shirika au taasisi ya aina yoyote, , kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji.

 

Atakayestahili fidia, anatajwa ni yule tu ambaye hajaendeleza makazi au kufanya ujenzi katika eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya shughuli za kijamii na aliyeendeleza makazi kwa kuzingatia vigezo na masharti yanayoambatanishwa katika hatimiliki ya ardhi aliyopatiwa na mamlaka yenye dhamana.

 

Hivyo basi, kutokana na hicho kilichotangulia kuelezewa, kwa wale wote waliojenga katika maeneo yasiyostahili kisheria watakuwa hawana haki yoyote wala shauri la madai msingi, dhidi ya serikali.

Sheria Elekezi ya Masuala ya Ardhi, Kinamtaka mnunuzi wa ardhi kuwa makini sana ya kujiridhisha, au maarufu (buyer beware).

 

Pia, kwa wapangaji, katika nyumba au majengo ya biashara, ambayo ujenzi wake haukuzingatia vigezo na masharti, nao wako hatarini kupoteza haki zao. Naomba kuwasilisha!