Wakala wapandishao nauli stendi ya Ubungo wasifumbiwe macho

19Nov 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakala wapandishao nauli stendi ya Ubungo wasifumbiwe macho

UNAPOFIKA katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo, jijini Dar es Salaam na unaingia katika stendi hiyo, utakutana na kinadada na kinakaka wanakukimbilia kwa kasi wakikuuliza ‘safari ya wapi na wapi unakoenda?’.

Hao ni wakala wa kampuni za mabasi, wakiwasaidia kutafuta abiria wa mabasi mbalimbali.Sina shida sana na hao wakala, bali mtihani wangu uko katika namna kazi hiyo inavyofanyika.

Cha kushangaza, unakuta wakala ana tiketi na mpiga debe pia ana tiketi zake. Riziki inatafutwa katika mtindo huo wa maisha, mwisho wa siku kila mtu anatoka na chake alicholenga kimaslahi.

Hatukatai mtu kutafuta riziki. Ni kweli wapo watu ambao hawajui hata mabasi ya kampuni yanapaki wapi na pale yakofikia, wapo wapo tu!

Kituko nilichokiona katika stendi hiyo ya Ubungo, haina siku nyingi, bali kadhaa zilizopita, nikiwa katika safiri ya kwenda Dodoma. Usafiri ulikuwa unasumbua kutoka Dar es Salaam kwenda jijini Dodoma.

Inawezekana ni zao la kisichokuwa kinaendelea bungeni, maana ni ndani ya msimu mmoja, wabunge wateule walikuwa wanaenda kuapishwa, huku wengine wakitumia usafiri wa mabasi. Gari nyingi zilikuwa zimejaa.

Pamoja na kujaa kwa gari hizo, lakini kuna magari ambayo nauli zake zilikuwa zinachanganya abiria hasa mnapomuonyesha tiketi kwa kondakta.

Ni gari moja, kulikuwapo tiketii tiketi zilizouzwa, nikishuhudia wastani wa Sh. 17,000, wengine Sh. 22,000 wapo wa Sh. 23,000 na na hata Sh. 25,000.

Sasa ninaingia katika kujiuliza, inakuwaje katika gari moja kunakuwapo nauli tofauti katika gari ambalo hata vitk vya nani ni sawa katika mfumo maarufu wa ‘two by two,’

Hata hivyo, inapotokea abiria anamuita kondakta akidai ufafanuzi wake, anajibu kwa kujiamini kabisa kwamba nauli sahihi ni shilingi 17,000 na ziada zingine anayejua ni mpiga debe aliyekatisha tiketi hiyo

Nikimrejea kondakta huyo, ni kwamba mpigadebe halipwi chochote, wakala nao wanajilipa. Sasa tunajiuliza, huyo mpigadebe anakuwa na nguvu gani kuliko wenye kampuni, hata wakafanya baadhi ya mambo kupitiliza?

Mtu akiangalia kwa kina kampuni zingine hazitumii wapiga debe na biashara inafanyika bila tatizo.

Ukiangalia kampuni  zinazotoza nauli kubwa, nazo ndizo zinazotoa huduma za ziada safarini kama soda, maji, juisi na zinakuwa hata na maeneo ya kuchaji simu. Safari inakuwa ya raha na starehe.

Pia, kuna cha ziada kwamba mtu akifuatilia nauli na mwenendo wa kampuni za mabasi zenye nauli kubwa, ni ngumu kukuta malalamiko ya aina hiyo kutozwa nauli tofauti.

Magari ambayo unakuta nauli zake hazieleweki, ndizo hazina hata huduma za maboresho ndani ya safari, simulizi za soda na juisi.