Wakati umepita wa kila kitu kufanywa na serikali

15May 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakati umepita wa kila kitu kufanywa na serikali

MOJA ya mada zinazovuta mjadala mkubwa sehemu yoyote ile na katika kada mbalimbali za kimaisha, huwa ni ya maendeleo.

Ukianzisha mada ya kwa nini kwa mfano kanda fulani imeendelea ama mkoa, wilaya, tarafa, kata, mtaa, kijiji, kitongoji na hata mtu binafsi, utakumbana na hoja zenye mtazamo tofauti juu ya mada hiyo.

Si ajabu kukumbana na mitizamo isiyokubaliana juu ya vigezo vya maendeleo ya nchi zilizoendelea, zinazoinukia na hata jamii au mtu aliyeendelea.

Aidha, kuna mitazamo tofauti juu ya nani anayeleta maendeleo ya mtu ama watu katika jamii au maeneo yao.

Na ndiyo maana ya kusikia watu wakiilalamikia serikali kutojenga daraja, kutuchonga barabara, kutoleta kariveti kwenye mtaro ama hata kwa nini haijakata miti inayohifadhi vibaka katika maeneo yao.

Kwamba kila changamoto ya maendeleo, hata iwe ndogo kiasi gani iliyo kwenye uwezo wa wananchi, bado kuna watu katika baadhi ya maeneo watabaki wakisubiri serikali itatue changamoto hiyo.

Binafsi mtazamo huo sikubaliani nao, nikiongozwa na dhana kuwa, maendeleo ya watu huletwa na wao wenyewe kwa ushirikiano na serikali.

Ninajua kwamba, serikali ina wajibu na majukumu yake ya kufanya katika dhana nzima ya kuchangia maendeleo ya watu wake.

Na baadhi ya majukumu  na wajibu wa serikali katika hilo ni pamoja na kudumisha amani kupitia sheria na amri zake mbalimbali na kulinda maisha na mali za watu wake.

Lakini pia kukuza demokrasia, haki za binadamu, kuzalisha ajira, kukuza maendeleo ya kiuchumi na kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.

Huduma kama zile za kujenga miundombinu, hospitali, mabomba ya maji, umeme, elimu na zingine zenye mchango mkubwa wa kuboresha kiwango cha maisha ya wananchi.

Hivyo ni kweli kuwa serikali ina wajibu na majukumu ya kufanya kwa watu wake katika hiyo dhana nzima ya kuleta maendeleo.

Lakini, ambacho sikubaliani nacho ni kitendo cha wananchi kuiachia serikali kila kitu, hata kwa vitu ambavyo kimsingi viko kwenye uwezo wao.

Mara nyingi nimesoma malalamiko katika vyombo vya habari, nimesikia redioni na hata kuona kwenye televisheni wananchi wakiilalamikia serikali kwa changamoto ambazo wangeweza kuzitatua kwa kutumia rasilimali zao.

Kwamba wananchi wameshindwa ‘kujiongeza’ hata katika suala la kununua koki ya maji ili bomba liendelee kuwahudumia kwa muda mrefu, badala yake wanasubiri serikali ilete koki, ili waendelee kupata maji.

Unakuta wananchi wanailalamikia serikali kutowajengea kivuko ama daraja dogo la mbao au miti kwenye bonde dogo linalopitisha maji wakati wa masika, na hivyo kusababisha watoto wao wasiende shule, wakati wangeweza ‘kujiongeza’ kidogo tu na kutatua changamoto hiyo.

Nimesikia malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali kwamba imeshindwa kudhibiti utoro wa wanafunzi wanaozagaa katika mitaa yao wakati walipaswa kuwa shuleni, kana kwamba hilo hawawezi kulidhibiti, wakisubiri serikali ije isaidie kupiga doria.

Muungwana hakubaliani na hili asilani la kuacha kutatua baadhi ya changamoto kwa msingi wa kuisubiri serikali izitatue, wakati wananchi wenyewe wangeweza kuzitatua mapema iwapo ‘wangejiongeza’

Tuna maeneo hapa nchini ambayo yaliona umuhimu wa ‘kujiongeza’ muda mrefu kwa kutoitegemea serikali, na sasa yamepiga hatua kubwa sana za kimaendeleo.

Maeneo hayo hayakufungwa na upofu wa kuitegemea serikali kwa kila kitu na hata kwa changamoto zilizo chini ya uwezo wao.

Maeneo hayo yamepiga hatua kubwa za za kimaendeleo katika nyanja nyingi kama vile elimu, afya, maji na miundombinu kutokana na kulibaini hilo mapema.

Muungwana anatoa rai kwamba, sasa si muda wa wananchi kusubiri kila kitu kifanywe na serikali, na badala yake wahamasishane wao wenyewe kutatua changamoto za kimaendeleo zilizo chini ya uwezo wao.