Wakongwe wanawatesa chipukizi Ligi Kuu Bara

14Jan 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakongwe wanawatesa chipukizi Ligi Kuu Bara

NILIWAHI kuandika kwenye moja ya makala zangu kuwa itafika wakati sasa wachezaji wa zamani wataanza kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na wachezaji vijana au chipukizi kushindwa kuwastaafisha, naona tayari imeshaanza kutokea.

Baada ya Haruna Moshi 'Boban' kusajiliwa na Yanga, nilisema kuwa kwa hali ya kawaida, kama wachezaji vijana wangekuwa wanacheza kwa kujituma kwa uwezo wao wote, basi sidhani kama kiungo huyu angethubutu si kujiunga na Yanga, bali hata kurejea tu Ligi Kuu.

Huu ni mwaka wa 16 Boban anacheza soka la kiushindani, akianzia timu ya Moro United mwaka 2003, na kupitia klabu mbalimbali kama Simba, Gefle IF, akarejea tena Simba kabla ya kutimkia Coastal Union na baadaye Mbeya City.

Alishaacha kabisa kucheza soka la ushindani na badala yake akawa anacheza la kujifurahisha kwenye timu yake ya mtaani Friends Ranger ya Magomeni Kagera.

Kutokana na vijana wengi kutojitambua, akajikuta ana uwezo wa kurejea tena Ligi Kuu kwenye kikosi cha African Lyon, lakini kikubwa zaidi hadi kwenye klabu ya Yanga.

Viongozi wa soka wa African Lyon na Yanga wamezunguka huku na huko na kuona uwezo na ubora wa Boban mkongwe ni bora zaidi kuliko wachezaji wengi vijana waliopo nchini. Kweli inasikitisha.

Tayari wachezaji wakongwe wameshaliona hilo, sasa wanaanza taratibu kurejea kwenye Ligi Kuu.

Januari 6 mwaka huu, African Lyon iliwachezesha wachezaji wengine wakongwe, Jabir Aziz na Ramadhani Chombo 'Redondo', hawa wote walifunga magoli kwenye mechi ambayo Lyon iliichapa Stand United mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru.

Chombo na Jabir nao ni kaliba ya Boban, ambao baada ya kuona mwezao ameshaula kwa mara pili na wao wanataka kuonyesha kuwa bado wamo ili ikiwezekana wasajiliwe hata kwenye kama Yanga, Azam, Simba, Mtibwa, Mbeya City na nyinginezo.
Kwa jinsi wachezaji wengi wa sasa vijana walivyo, tusishangae kuona ndoto zao zinatimia.

Ni kwa sababu wachezaji wa sasa wameshindwa kuwafanya wachezaji wakongwe wastaafu wenyewe kwa hiari yao kwa kushindwa kasi yao kutokana na kuwa na damu changa, badala yake wamewafanya wakongwe waonekane kama mvinyo ambao kila unavyozidi kuwa wa zamani, ndivyo unavyozidi kuwa mkali.

Kwa sasa wanatishia namba za vijana ambao wanaonekana hawajiongezi na wanategemea zaidi vipaji vyao, kuliko bidii, juhudi na nidhamu kwenye soka.

Binafsi nilitarajia wakongwe kurejea baada ya Boban kusajiliwa na Yanga.

Wachezaji wakongwe sasa wameonekana kuondoa woga wa kukimbizwa na vijana, wanarejea kwa sababu wanaona vijana wenyewe kasi yao ipo kama wazee.

Kumbuka kuwa hata Ulaya, wachezaji hustaafu siyo kwamba soka mguuni hakuna, au kipaji kimeisha, hapana, ila wanachokimbia ni kasi ya wachezaji vijana ndiyo inawatisha.

Umri ukienda kasi nayo hupungua. Mpira wa sasa wa vijana hauna kasi. Kama ni hivyo basi Boban, Chombo Jabir na wengine ambao walishastaafu au kuacha soka la ushindani wanaweza kurejea na kukitwanga kama kawaida.