Wakopaji kinamama, vijana walemavu, irejeshwe mapema

20Mar 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakopaji kinamama, vijana walemavu, irejeshwe mapema

KILA wakati inajulikana kwamba, mkopo ndio mkombozi wa kila kitu katika sura ya maendeleo ya kijamii na kuchumi. Mtu anachukua na kisha akajipanga namna ya kuikabili.

Siku zote mikopo imekuwa mkombozi kwa watu mbalimbali au taasisi, kutokana na kutumika katika kujiongezea mapato ndani ya maeneo husika.

Mikopo inatolewa katika makundi mbalimbali, ili mtu katika nafasi ya mmoja mmoja au taasisi, lengo ni kuyawezesha maeneo hayo kuinuka kiuchumi.

Tumeziona taasisi mbalimbali ambazo zinazotoa, mikopo kwa makundi mbalimbali, ikiwamo kampuni za simu ambazo nazo zinatoa mikopo.

Pamoja na kutoa mikopo na kampeni za simu, kila anayechukua mkopo, lazima alipe na tiba kulingana na viwango vilivyoidhinishwa.

Mikopo hiyo inakusanywa na pale inapotolewa na riba, inakusanywa na taasisi hizo, kisha unafanyika mzunguko ili kuwawezesha na kupata mikopo.

Katika baadhi ya taasisi, unapochukuliwa mkopo una masharti kwamba mtu anapochelewa kurejesha, hapatawi fursa nyingine kulipa.

Imeshatokea, katika mikopo hiyo, kuna kampuni au taasasi zimekuwa zikiuza mali za wateja wasiolipa mikopo.

Tukirejea kwa kina, mikopo ambayo Rais John Pombe Magufuli, aliagiza itolewe kwa wanawake, walemavu na vijana, aliweka wazi kwamba itolewe bila ya kuwatoza riba.

Pamoja na fadhila hiyo ya kiserikali, bado kuna baadhi ya vikundi vilivyochukua mikopo na kushindwa kurejesha kwa wakati, hali inayokwamisha wengine hata wakakosa fursa za kupata mikopo hiyo.

Baadhi ya watu wamekuwa wakilalamikia, kwamba wanakosa mikopo. Hivi karibuni, Diwani wa Kata ya Mabibo, jijini Dar es Salaam, Kassim Lema, anasema kuwa Wilaya ya Ubungo, imetoa mikopo zaidi ya shilingi bilioni tatu, kuviwezeshwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.

Anasema mbali na hilo, mpaka sasa kuna kiasi cha Sh. milioni 700 pekee ndio zimerudishwa na alinukuliwa akitamka hivi:

"Tumetoa zaidi ya Sh. bilioni tatu, kuvipatia vikundi vya wanawake, walemavu na vijana, lakini mpaka sasa marejesho yaliyopokelewa ni Sh. milioni 700."

Lema anasema, wale wasioelewa wataona kama mikopo haijawahi kutolewa, lakini waelewe kuwa mikopo imeshaanza kutolewa, lakini baadhi ya wanavikundi sio waaminifu.

Anafafanua kwamba, mikopo kutorejeshwa kwa wakati katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kamati husika imekaa na kutafakari jinsi ya kuanza kuwachukulia hatua wanavikundi ambao hawajarejesha mikopo husika.

Diwani Lema anafafanua kiasi cha shilingi bilioni tatu kilichogawiwa katika makundi hayo, kwamba kinamama walipata shilingi bilioni 1.6, vijana walipata shilingi bilioni 1.5 na walemavu Sh. milioni 180.

Anasema, pamoja na mikopo kutolewa bila ya riba, lakini baadhi ya vikundi vimeshindwa kuirejesha mikopo kwa wakati.