Wakulaumiwa Simba si Aussems peke yake

16Nov 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakulaumiwa Simba si Aussems peke yake

SIKU chache baada ya klabu ya Yanga kumuondosha kocha wake mkuu Mwinyi Zahera, ni kama bundi ametoka maeneo ya Jangwani na kuanza kuambaa kwenye mitaa ya Msimbazi.

Tayari baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba wameanza kumnyooshea kidole cha shahada Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems si tu kutokana na matokeo hafifu ya siku za karibuni, bali wanaonekana kutoridhishwa hata na aina ya soka linalochezwa na kikosi chao.

Wanachama na mashabiki wa Simba wanaonekana bado kuwa na dukuduku la kutolewa mapema kwenye michuano ya Ligi Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji.

Wanaonekana kama hawakutaka tu kuonyesha hasira zao wakati huo, baada ya kupozwa kuwa harisa zote sasa zitaelekezwa kwenye Ligi Kuu na hakuna timu ya kuisimamisha Simba.

Baada ya kuvumilia ilipochapwa na Mwadui bao 1-0, sare ya nyumbani ya bila kufungana dhidi ya Prisons imewafanya kutoa dukuduku lao wakisema kuwa Mbelgiji huyo ameishiwa mbinu, hivyo ni wakati sasa wa kuaondolewa.

Ni kweli kabisa Simba iliondolewa kizembe na UD Songo, kwani ukiangalia mwenendo wa timu hiyo baada ya hapo, ilifungwa mechi zote nne za nyumbani na ugenini.

Kwa ninavyoona ni kwamba matatizo ya Simba hayapo kwa kocha Aussems peke yake na hata kama akitimuliwa, matatizo bado yataendelea kuwapo.

Naweza kuainisha matatizo yapo sehemu tatu. Kocha ana sehemu yake ndogo, wachezaji wenyewe na baadhi ya viongozi waliopewa majukumu ya kusajili.

Nikianza na Aussems, nimesikia kuwa hapendi wachezaji wake wakae kambini kwa muda mrefu. Hili linaweza kumgharimu, kwani wachezaji wanaocheza soka Tanzania bado hawajajua kujitunza wenyewe na si kama wa Ulaya.

Kingine kuwachezesha wachezaji wengi wasio na kasi katikati ya uwanja. Sharaf Shiboub, Clatous Chama na Ibrahim Ajibu, wakicheza kwa pamoja, huwezi kuwa na timu inayoshambulia kwa kasi kwa sababu wote asilia yao ni kupaka rangi mpira na hawana kasi.

Ukiacha matatizo ya kocha, baadhi ya wachezaji wa Simba msimu huu kama Jonas Mkude na Chama hawako kwenye viwango vyao vilivyozoeleka, ukichanganya na upangaji wa wachezaji wasio na kasi unaikuta Simba iliyopooza.

Lakini pia wapo wachezaji ambao hawajitumi uwanjani. Unashangaa kuona Simba ina makocha wengi wa viungo na fiziki, lakini wachezaji wengi hawawezi kugombea mpira na wapinzani wakaweza kuuchukua. Wengi wanashindwa nguvu au wanaogopa kuingiza mguu.

Wachezaji wanaoonekana wana uwezo wa kupambana kwa kushindana nguvu ni Meddie Kagere, Paschal Wawa, Gelson Fraga, Hassan Dilunga, na Mzamiru Yassin tu, wengine wote wanaonekana kucheza kigoigoi.

Tatizo la tatu ni viongozi waliofanya usajili msimu huu. Timu kubwa kama ya Simba ina mastraika watatu tu kitu ambacho ni kosa kubwa na ni aibu.

Mfano ingekuwa inaendelea kwenye michuano ya kimataifa ingekuwaje kama ina Kagere tu mbele?

Simba inaonekana kwa kiasi kikubwa inaathirika kwa kukosekana kwa John Bocco. Msimu huu wote tangu uanze imekuwa ikisimamisha straika mmoja tu ambaye ni Kagere, akibanwa inakuwa mtihani kufunga kama winga Miraji Athumani hakusaidia.

Viongozi waliosajili msimu huu, walifanya makosa kwa kusajili straika mmoja tu Mbrazil Wilker Henrique da Silver, ambaye naye inaonekana uwezo wake ni wa kubahatisha.