Wakulima wakizingatia mafunzo dhuluma zitaisha

03Jul 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakulima wakizingatia mafunzo dhuluma zitaisha

MIAKA kadhaa iliyopita, wakulima wa pamba wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria walikuwa wakilalamikia changamoto walizokuwa wakikutana nazo  katika kilimo cha zao hilo ambazo zilisababisha wakate tamaa kuzalisha pamba.

Wakulima hao ni wa mikoa ya Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza na Mara, ambao malalamiko yao makubwa yalikuwa ni kuuziwa pembejeo mbegu feki ambazo hazioti, mbole feki ya majivu na pia ukosefu wa soko la zao hilo na pia kuibiwa katika mizani wanapouza kwenye magulio.

Kufuatia kilio hicho, serikali iliingilia kati na kudhibiti wasambazaji waliokuwa wakiwapa pembejeo feki na pia kukomesha mtindo wa kuchakachua mizani, ambao ulilenga kuwaibia kilo za pamba.

Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) ulio chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda na Biashara mara kwa mara imetoa elimu, kwa wakulima sehemu mbalimbali  pamoja na kuhakiki mizani zinazotumika kununulia zao.

Lengo kubwa ni kuhakikisha wakulima wanatambua mizani iliyo sahihi na inayoruhusiwa, ili wajilinde wenyewe pale maofisa vipimo wanapokuwa hawapo katika vituo vya kuuzia pamba.

Wakulima wanapotambua mizani iliyochakachuliwa na kuikataa, inakuwa ni rahisi kupata faida ya thamani halisi ya jasho lao, kuliko kuendelea kuibiwa na wajanja wachache wanaojinufaisha kwa jasho la wengine.

Pamba ni miongoni mwa mazao matano ya kimkakati ya biashara, ambayo serikali imevalia  njuga na kuahidi kuyasimamia ili kuhakikisha yanapata soko na pia kila mkulima anafaidika na jasho lake badala ya kudhulumiwa kwa namna yoyote.

Pamoja na pamba ni mazao mengine ni pamoja na tumbaku, kahawa, korosho na chai, ambayo yana mchango mkubwa wa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Hivyo  kwa kitendo cha kukamatwa watuhumiwa ni wazi uchakachuaji bado upo na unaweza kukwamisha juhudi za serikali za kufanikisha kilimo hicho cha mazao ya kimkakati.

Watuhumiwa wa uchakachuaji ndiyo wanaokwamisha juhudi za serikali za kuwakomboa wakulima wa pamba kwa kuendelea kuwaibiwa wakitumia mizani iliyochakachuliwa kana kwamba hakuna marufuku yoyote dhidi ya matendo hayo.

Ni hivi karibuni Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mwanza amenasa watuhumiwa wakiwa na mizani waliyoichezea ili kuwaibia wakulima kwenye vyama vya msingi vya kuuzia zao hilo.

Tukio hilo linaonyesha kwamba pamoja na juhudi za serikali, bado mtindo huo wa kuibia wakulima ni tishio, hivyo ni vyema serikali iendelee kuwamulika watu wa aina hiyo na kuwachukulia hatua za kisheria.

Vilevile kama ambavyo Wakala wa Vipimo umekuwa ukitoa elimu kwa wakulima na kuwahamasisha ili kuzitambua mizani zilizochakachuliwa, ni wakati wa kuzidisha elimu hiyo, kwa kuzingatia kwamba kuna uwezekano wa wakulima kuongezeka kila mwaka.

Wakulima wanapoongezeka, maana yake wengine ni wapya na huenda wasiwe na elimu kuhusu mizani hizo na hivyo wakawa waathirika kwa kuibiwa kirahisi bila kujua na kujikuta jasho lao likiishia mikononi mwa wahalifu wachache.

Serikali imeshafufua vyama vya ushirika, ambapo ununuzi wa pamba utafanywa na vyama hivyo, tena ni vile vinavyosimamiwa na wakulima wenyewe badala ya kuuza kupitia mawakala kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Utaratibu huo unamnufaisha zaidi mkulima kwa kuuza kupitia vyama vya msingi, kwani mazao yote yanayopatikana kutoka kwenye pamba kuanzia mbegu hadi nyuzi, anahusika kupata faida ya uuzaji wa mazao hayo.

Lakini uchakachuaji unapojitokeza tena, unawaumiza wakulima. Ndiyo maana kuanzia sasa wanatakiwa kuwa makini kutumia elimu waliopewa na wakala wa vipimo kutambua mizani zilizochakachuliwa na kuzikataa.

Kwa kuwa Wakala wa Vipimo anaweka wazi kuwa wasimamizi na watumiaji wa mizani ni wakulima wenyewe wa pamba, basi waongeze umakini na umahiri katika kuichunguza ili kuhakikisha kuwa hawaibiwi kirahisi pamba inapofikishwa kwenye magulio.

Wakala wa Vipimo umeweka wazi kwamba lengo lao ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya kile alichozalisha na siyo kupunjwa na wafanyabiashara wajanja wachache.

Hivyo ili kufikia Tanzania ya viwanda, wakulima na wafanyabiashara wazingatie matumizi ya vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokeaji wa mazao kwenye maghala.

Umakini ulioko katika pamba uende mbali na kufikia mazao mengine ili kuepusha dhuluma hii.