Katika baadhi ya shule za jijini Dar es Salaam, wanafunzi hao wanaporejea shuleni wanapokelewa na walimu wao bila kuchukua tahadhari za ugonjwa corona au UVIKO-19.
Walimu ambao ndiyo walikuwa wapokeaji wa wanafunzi pamoja na wanafunzi wageni hawakuonekana kufuata maagizo yanayotolewa na Wizara ya Afya ya kujikinga na virusi hivyo, ambayo hutangazwa kila mara kwenye vyombo vya habari zikiwamo redio na runinga.
Maagizo hayo ni kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kukaa umbali wa mita moja baina ya watu pamoja na kupata chanjo ya UVIKO-19 ambazo hutolewa kwenye vituo vya afya bure hasa kwa watu wazima.
Katika shule nyingi wanafunzi walionekana kujazana darasani, darasa moja likiwa na wanafunzi 80, wakikaa kwenye madawati ambayo yamekaribiana kiasi cha kwamba hakuna nafasi ya mtu kupita kwa nyuma.
Baadhi ya shule hazikuwa na ndoo za maji za kunawia mikono ambazo zilipaswa kuwekwa kwenye geti la kuingilia na sehemu nyingine ili wageni pamoja na wanafunzi wasafishe mikono yao kabla ya kuingia ndani.
Hata, zile zilizokuwa na ndoo watoto hawakuonekana kuzijali kwani walikwenda kununua vitu na kula bila ya kunawa mikono na hakukuwa na mwalimu wa kusimamia hilo.
Katika shule ya Msingi Ruvuma iliyopo Manispaa ya Temeke, mwalimu wa darasa la kwanza, alikutwa amezungukwa na kundi la wanafunzi wakigombania kusahihishiwa ili wawahi kwenda nyumbani, lakini hakuwa na barakoa.
Katika mazingira hayo, mwalimu huyo ambaye hakuwa na barakoa aliyekuwa akiwatuliza wanafunzi hao waache vurugu, ni rahisi kuambukizana virusi hivyo na wanafunzi hao ambao nao wangekwenda kuambukiza ndugu na jamaa , ambapo ndani ya muda mfupi idadi ya maambukizi na hata vifo ingeongezeka.
Pengine kukaa nyumbani kwa muda mrefu kumewafanya kusahau kuwa ugonjwa huu upo, na hii ni kutokana na kwamba watoto hawakuwa na watu wa kuwakumbusha kuhusu ugonjwa huo hatari kwa kuwa wazazi wanadhani kuwa hilo ni jukumu la walimu.
Kwa kuwakumbusha tu kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia Januari 3, mwaka huu Tanzania ilikuwa na jumla ya wagonjwa wa UVIKO-19, 30,564 na vifo 740 hali inayoonyesha kuwa maambukizi yanaongezeka ingawa kwa kasi ndogo.
Kama wahenga wanavyosema ‘yaliyopita si ndwele’, ni wakati uongozi wa shule kutilia mkazo suala la UVIKO-19 kwa kurudisha nidhamu ya woga na hofu juu ya ugonjwa huo kwa watoto.
Walimu hawana budi kuanza upya kuelimisha wanafunzi juu ya ugonjwa huo hatari, jinsi unavyoambukiza na athari zake kwa afya zao, lakini pia njia muhimu za kujikinga na ugonjwa hupo.
Kwa kuwa kujifunza kwa kuona na vitendo ni bora zaidi walimu wanapaswa kuonyesha mfano kwa kuvaa barakoa kila wakati, kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono wakiwa darasani ili wanafunzi wajifunze kutoka kwao.
Umma unapaswa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kazi kubwa inayofanywa ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanaishinda vita dhidi ya UVIKO-19, kwani kasi ya maambukizi nchini sio kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine kama vile Russia ambayo mpaka kufikia January 16 ilikuwa na jumla ya wagonjwa milioni 10.8 wagonjwa wapya wakiwa 31,252 na vifo vipya 688 kwa mujibu wa mtandao wa World meter.