Waliokosa elimu rasmi wasibweteke, wachangamkie fursa hizi za serikali

28May 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Waliokosa elimu rasmi wasibweteke, wachangamkie fursa hizi za serikali

ELIMU ni haki ya msingi ya kila mtoto, ingawa kuna baadhi ya watoto ambao hawakubahatika kuipata kutokana na changamoto mbalimbali.

Hata hivyo, pamoja na changamoto zinazochangia baadhi yao kutopata elimu, bado kuna njia wanayoweza kuitumia kupata.

Njia hiyo ni ile iliyoanzishwa na serikali kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA).

Mpango huu unalenga kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ingawa ni nje ya mfumo rasmi.

Serikali ilichukua hatua za kuanzisha mpango huo kwa kutambua kwamba elimu ndio urithi pekee unaoweza kumkomboa mtoto kifikra, hasa kwa kuzingatia kwamba elimu ni kati ya haki za msingi za kibinadamu.

MEMKWA inahusisha makundi mawili, la kwanza likiwa ni rika la watoto walio na umri kati ya miaka 10-13, wanaosoma kwa muda wa miaka miwili hadi minne na kufanya mtihani wa darasa la nne.

Kundi la pili ni la rika la vijana wa miaka kati ya 14 hadi 18.

Mwaka 1999 MEMKWA ilianzishwa kwa majaribio kwenye baadhi ya wilaya zikiwamo za Ngara mkoani Kagera, Masasi mkoani Mtwara, Songea Vijijini mkoani Ruvuma na Kisarawe mkoani Pwani.

Baada ya programu hiyo kuonyesha mafanikio, mwaka 2003 serikali ilianzisha madarasa ya MEMKWA katika shule za msingi kote nchini lengo likiwa ni kuhakikisha wale wote waliokosa elimu rasmi wanaipata.

Pamoja na juhudi hizo za serikali za kutaka kuhakikisha Watanzania wote wanapata elimu, bado kuna changamoto kufuatia baadhi yao kutojua kusoma na kuandika.

Hii inatokana na kile kilichosemwa bungeni na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, kwamba asilimia 20 ya Watanzania hawajui kusoma na kuandika.

Waziri Manyanya alisema hayo Septemba mwaka jana, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Tasca-Restuta Mbogo (CCM) kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.Mbunge huyo alihoji kama kuna mpango wa serikali kurudisha elimu ya watu wazima iliyokuwapo miaka ya nyuma.

Kwa hali kama hiyo ni wajibu wa kila Mtanzania kupambana na adui ujinga kutokana na ukweli kwamba tayari serikali imeshatoa fursa ya kumwezesha kila aliyekosa elimu rasmi kuipata kwa njia ya MEMKWA.

Hata wale ambao ni watu wazima, bado wana fursa kwenye mfumo wa elimu ya watu wazima, wakajua kusoma na kuandika badala ya kubweteka.

Ikumbukwe kuwa kusoma na kuandika ni mwanga wa kumwezesha mtu kuendesha maisha yake na hata kupambana na adui maradhi na umaskini.

Kwa hiyo MEMKWA ni fursa nzuri kwa vijana, ambao hawajui kusoma na kuandika ili waitumie kuondokana na adui ujinga anayeweza kuwa kikwazo cha wao kuendelea.

Mbali na MEMKWA, kwa sasa serikali inatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, hivyo mazingira ya kujipatia elimu yamerahisishwa.

Vilevile si vibaya kwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kuandaa mkakati wa kusaidia kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika kwa kutambua kwa maana ujinga ni adui wa maendeleo.

Jamii itambue kuwa iwapo kama watu wengi watakuwa hawajui kusoma na kuandika, itakuwa vigumu kwa nchi hii kufikia lengo lake la Tanzania ya viwanda ambayo inahimizwa kwa ajili ya maendeleo.

Kwa kukumbusha ni kwamba Mwalimu Julius Nyerere alitangaza vita kwa maadui watatu baada ya nchi kupata uhuru mwaka 1961, ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

Lakini maadui maradhi na umaskini hawawezi kuondoka kabla ya kumwondoa adui ujinga, hivyo Mjadala unaona ni muhimu kuunga mkono juhudi za serikali zinazotaka kila mtoto wa Kitanzania apate elimu.

Hivyo ni muhimu kurudi darasani kwa wale ambao wamesoma lakini wakatoka bila kujua kusoma na kuandika na pia ambao hawakubahatika kupata elimu, wajiunge na MEMKWA au kisomo cha watu wazima.

Inawezekana wapo baadhi ya watu ambao wanaona aibu kuhudhuria madarasa ya MEMKWA au kisomo cha watu wazima, lakini watambue kuwa elimu haina mwisho na ina mchango mkubwa katika maendeleo.

Sensa ya mwaka 2012 ilionyesha kuwa asilimia 22 ya Watanzania walikuwa hawajui kusoma na kuandika, na huenda takwimu hizo zikawa zimeongezeka au kupungua iwapo jamii itakuwa imetambua umuhimu wa elimu.