Wanachama kumbukeni CCM mpya haitaki makandokando

15Mar 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Wanachama kumbukeni CCM mpya haitaki makandokando

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi ya chini hadi taifa na tayari waliozoea kutumia rushwa kupata uongozi wameshaonywa kwamba wasijihusishe na vitendo hivyo vinginevyo watashughulikiwa.

Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza hilo na hata viongozi wengine wa chama wamekuwa wakiongeza uzito kile ambacho bosi wao anakitaka.

Machi mwaka huu Chama Cha Mapinduzi kitaanza kufanya uchaguzi katika ngazi mbalimbali kuanzia shina, tawi, kata, wilaya, mkoa na kumalizia na uchaguzi wa ngazi ya taifa Desemba.

Magufuli anataka mwanachama achaguliwe kutokana na sifa zake bora ndani ya chama na siyo fedha kama ambavyo inadaiwa kwamba miaka ya nyuma kulikuwa na mchezo wa aina hiyo.

Tayari wenyeviti na makatibu wa chama kote nchini wameshafundwa jinsi ya kusimamia haki katika kuteua wagombea na kusimamia uchaguzi ndani ya chama utakaofanyika mwaka huu uwe huru na haki.

Viongozi hao wenye jukumu la kuongoza vikao vya kuchambua na kupitisha majina ya wagombea na kusimamia uchaguzi na wale watakawania uongozi hawana budi kusoma ishara za nyakati ili kuhakikisha wanatimiza kile ambacho mwenyekiti wao taifa anakitaka.

Baadhi ya mikoa ikiwamo Dar es Salaam wameshapanga kuwategeshea fedha za moto wale wote watakajihusisha na rushwa katika uchaguzi huo ili wawanase na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawile amekuwa akisisitiza hilo anapokutana na viongozi wa jumuiya hiyo mkoani kwake kwamba atahakikisha hakuna mgombea atakayepitishwa kwa rushwa.

"Hii ni CCM mpya ambayo haina makandokando na tayari mwenyekiti wetu wa chama taifa amekuwa akihimiza hilo kwamba hakuna atakayechaguliwa kwa rushwa, hivyo nasi hatuna budi kumuunga mkono," aliwahi kukaririwa akisema Mkandawile.

Kwa hiyo njia pekee ya kujiepusha na hayo ni wale ambao wanajiandaa kutumia fedha kupata uongozi kukubali kwamba hii ni CCM mpya ambayo haitaki kuwa na makandokando.

Kumekuwapo na malalamiko kwamba baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa ni chanzo cha chama kupoteza nafasi katika uchaguzi kwa sababu hushiriki 'kubeba' wagombea wasiotakiwa na wananchi.

Hao ndio ambao Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwaita kwa jina la madalali wa chama wanaouza viongozi ndani ya chama hicho na kusema hawatakiwi tena na kuwataka watafute kazi nyingine ya kufanya.

Kama nilivyosema awali baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakituhumiwa kuwasaidia watu kupanga safu, kuwabeba watu na kuwachagua wanaowapenda badala ya kuachia wapigakura kazi hiyo.

Inadaiwa kuwa viongozi hao huahidiwa ama hupewa chochote ili kufanikisha hilo na sasa viongozi wa ngazi ya juu wa CCM wameliona hilo na kulipiga marufuku kwani rushwa inasababisha wasipatikane wagombea wanaofaa.

Katika mazingira hayo wapo baadhi ya wanachama ambao waliwahi kutamka hadharani kwamba CCM sasa imebaki ya watu wenye fedha na kwamba asiye nazo hawezi kupata uongozi!

Kwa maana hiyo rushwa isipotumika katika uchaguzi watapatikana wagombea wanaokubalika na wengi, kwani ukweli kwamba wanachama wazuri wamekuwa wakishindwa kugombea kwa kutokuwa na uwezo wa kifedha.

Hivyo ni vyema kila mhusika akazingatia maelekezo wa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Magufuli kwa kutumia nafasi yake kutenda haki ili kupata wagombea ambao upatikanaji wao hautokani na rushwa.

Ninaamini kwamba msisitizo wa mwenyekiti kwamba viongozi watakaojiingiza katika rushwa, atawashughulikia umewafikia wote, hivyo ninadhani mwaka huu watapatikana wagombea bora na wenye sifa zinazotakiwa.

Kwa kawaida uchaguzi ni sehemu ya uhai wa chama, kwani wanaochagulia ndio wenye jukumu la kuoongoza chama na kuweka mikakati ya ushindi kwenye chaguzi zinazohusisha vyana vingine, hivyo hawatakiwi kuwa na makandokando.

Mbali na wale wanaotumia fedha kupata uongozi, wapo wanaoitwa mapandikizi ndani ya chama ama mamluki ambao mchana huwa ndani ya CCM na kisha usiku chama kingine, hao nao wametakiwa kumulikwa katika uchaguzi wa mwaka huu.