Wanafunzi wasinyanyaswe daladala

10Jun 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanafunzi wasinyanyaswe daladala

TATIZO la wanafunzi kunyanyaswa kwenye mabasi ya daladala jijini Dar es Salaam linaendelea kushika kasi siku hadi siku licha ya watu wengi kuonyeshwa kukerwa na mwenendo huo.

Changamoto hiyo ni kama vile imekosa ufumbuzi kutokana na ukweli kwamba, ni ya muda mrefu na imekuwa zikipigiwa kelele na jamii lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa na vyombo husika ili kuiondoa.

Nasema hivyo kwa sababu, ni kama imekuwa ni kuona makondakta na madereva wa daladala kuwazuia wanafunzi wanapotaka kupanda magari kuwahi shuleni ama kurudi nyumbani.

Utaratibu huu umewafanya hata baadhi ya watu kuona kama ni jambo la kawaida wanafunzi kuzuiwa kupanda magari hayo, kwani huwa hawathubutu kuukemea, hali inayochangia kuendelea kuwapo kwa mchezo huo.

Ikumbukwe kuwa, wanafunzi hawapandi bure, bali wanalipa nauli kama kawaida kulingana na viwango vilivyowekwa na Sumatra, lakini bado wanazuiwa eti kwa sababu nauli wanayoitoa ni ndogo!

Kwa mujibu wa viwango vya nauli vya Sumatra, mwanafunzi anatakiwa kulipa Sh. 200 kwa ruti moja, lakini makondakta wamekuwa wakiwazuia wasipande daladala ama walipe nauli ya mtu mzima ambayo ni kati ya Sh. 400 hadi 600.

Utaratibu huo umekuwa ukichangia kuwafanya wachelewe vipindi shuleni ama kurudi nyumbani pia wanawaongezea wazazi na walezi bajeti isiyotarajiwa kwa sababu tu ya tamaa ya fedha.

Ni vyema ikaeleweka kuwa hakuna mzazi ama mlezi anayependa mtoto wake apate taabu, nadhani ni wachache wenye tabia hiyo, kinachosababisha watoto wao wasome shule za mbali ni mfumo wenyewe wa elimu.

Mfano mtoto anaweza kuchaguliwa kwenda kusoma sekondari ya Kisauke huko Madale wakati anaishi Kimara ama Kibamba, hivyo atalazimika kupanda daladala ili kuwahi shule kwani ndiyo usafiri wa umma.

Anatumia usafiri huo wa umma kwa sababu wazazi wake hawana gari ama njia nyingine ya kumfanya awahi shule, kwani siyo kila familia ina magari binafsi, hivyo kumzuia kupanda daladala ni kumnyanyasa kwa kumfanya asiwahi vipindi shuleni.

Wakati mwingine inawezekana watoto wakaosoma shule binafsi, kwani wazazi wanaangalia ni wapi zilipo shule zenye ubora, na hapo ndipo watoto wanapolazimika kusoma shule za mbali na nyumbani kwao.

Kwa mazingira hayo unakuta wanalazimika kuamka asubuhi na mapema kuwahi usafiri wa umma ambao ni daladala ili wafike shuleni mapema, lakini wanajikuta wakikwamishwa na makondakta kwa kushirikiana na madereva.

Daladala linaweza kupitiliza kwenye kituo pale dereva na kondakta wake wanapoona kuna wanafunzi, ama wanaweza wakasimama lakini wasiwachukue kutokana na sababu wanazozijua wenyewe ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na wananchi.

Ni kama jamii imezoea na hata watoto wenyewe ni kama wazoea hali hiyo kutokana na ukweli kwamba ingawa ni ya muda mrefu, hakuna hatua za makusudi za kuhakikisha kero kwa watoto hawa zinakwisha.

Nasema hivyo kwa sababu wengi wao wamekuwa wakihangaika kwenye vituo vya daladala bila kuwa na uhakika wa usafiri hali ambayo inasabisha wafike shuleni wakiwa wamechelewa na hata wakati mwingine kuadhibiwa na walimu.

Ukipata nafasi ya kuzunguka maeneo mbalimbali ya vituo vya daladala utakuta makundi ya wanafunzi yakisubiri usafiri na hata wakati mwingine baadhi yao hulazimika kutumia usafiri wa malori ama magari mengine ambayo kwa namna moja ama nyingine siyo salama kwao.

Ikumbukwe kuwa mazingira kama hayo yanachangia kuwaathiri kielimu kwani wanatumia muda mwingi kutafuta usafiri wa kwenda shule ama kurudi nyumbani na kukosa nafasi ya kutosha kwa ajili ya kujisomea.

Katika mazingira kama haya siyo rahisi mwanafunzi anayehangaika na usafiri, akafika nyumbani akiwa na afya kiakili ya kumfanya aketi mezani na kujikumbushia mawili matatu aliyofundishwa na walimu wake shuleni.

Kama imeshindikana kuwadhibiti watu hawa, basi ni vyema wanafunzi watafutiwe magari yao ya kuwapeleka shule na kuwarudisha nyumbani kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kuliko kuwaacha wakiteseka kana kwamba hawana haki ya kupanda daladala.