Wanahabari watumie uhuru huu kikamilifu

03May 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanahabari watumie uhuru huu kikamilifu

LEO ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambayo  huadhimishwa Mei 3 ya kila mwaka kwa lengo la kukuza uelewa wa umuhimu wa uhuru wa tasnia ya habari.

Aidha, yanakumbusha kuviheshimu pia ili kulinda haki ya kupata habari kwa kila mmoja kwa kuwa ni taarifa sahihi ndizo zinazoleta uelewa na kujua mambo.

Uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari ni moja ya haki ya msingi ya kiraia inayoipa jamii haki ya kupata habari na kusambaza taarifa, haki ya uhuru wa kujieleza na haki ya uhuru wa maoni ambazo ni nguzo muhimu katika kuzingatia misingi ya demokrasia.

Ni kwa mantiki hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, amewahi kugusia uhuru huo na kuagiza kufunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyofungiwa huku akiwataka wahusika kutotumia ubabe kuvidhibiti.

Pamoja na hayo, akashauri vyombo vya habari visifungiwe kibabe akisema; "Watakapofanya makosa adhabu zitolewe kulingana na sheria inavyoelekeza, viacheni vifanye kazi yao isionekane wanazuiwa kuongea."

Kauli kama hiyo kutoka kwa kiongozi wa nchi, inatia matumaini kwamba anatambua na kuthamini mchango wa vyombo vya habari kwa jamii na taifa kwa kuwa bila hivyo hakuna kuenea taarifa kutoka kwa wananchi kwenda kwa viongozi na kwa wanaowaongoza kwenda kwa umma, na anaagiza viheshimiwe.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye naye anaongeza kuwa anataka vyombo vya habari visisite kuikosoa serikali, huku akitaka ukosoaji uwe wa kujenga na siyo kubomoa, kwa kuwa vikiikosoa serikali bila kutoa mbadala ikakasirika itakuwa siyo vizuri.

Kwa kauli hizo, ni wazi kuna dhamira ya dhati ya kudumisha uhuru wa vyombo vya habari, hivyo ninadhani sasa ni wajibu wa waandishi wa habari kutumia uhuru huo vizuri, kwani hakuna uhuru usio na mipaka.

Ni wazi kwamba serikali inatambua umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa  uhuru na kujali uzalendo wa nchi  bila kuvunja sheria, hivyo suala la kutambua mipaka ya uhuru wanaopewa ni la muhimu.

Wajibu wa waandishi wa habari ni kuwa mastari wa mbele kuhabarisha umma wa Watanzania kwa kutoa taarifa kwa kuzingatia maadili yanayoongoza tasnia ya habari na kufuata sheria na katiba ya nchi.  

Iwapo waandishi watakwenda kinyume wanaweza kujikandamiza wenyewe kwa vyombo wanavyofanyia kazi kufungiwa, kutokana na kukiuka maadili na kubaki wakilalamika kukandamizwa, kumbe makosa yanaweza kutoka kwao.

Miaka ya hivi karibuni, vyombo  vya habari vimeendelea kuongezeka nchini vikiwamo vya mitandao ya kijamii, hali inayoonyesha uwapo wa uhuru wa  vyombo hivyo, jambo la msingi ni kufanya kazi kwa kuzingatia maadili.

Ninaamini kwamba Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni nafasi ya pekee ya kuwapa waandishi fursa ya kutafakari na kuenzi wajibu wao muhimu kwenye jamii kama kioo kinachoimulika.

Hivyo ingependekeza kama kila mmoja atahakikisha anatimiza wajibu wake inavyotakiwa, katika kuendeleza taaluma hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwenye jamii na taifa linalotegemea pia tasnia hiyo kwa maendeleo.

Iwapo kila mwandishi atazingatia maadili ya kazi yake, hakutakuwa na ongezeko la usambazaji wa taarifa zisizo sahihi na za uzushi kupitia mitandao yaa kijamii ambazo zimekuwa zikijitokeza kila mara.

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani isaidie kuwabadilisha wale ambao wamekuwa wakijisahau na kujikuta wakisambaza taarifa zisizo sahihi na kusababisha taharuki kwenye jamii, badala yake wafuate maadili.