Wananchi wadau muhimu ujenzi miundombinu elimu

19May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wananchi wadau muhimu ujenzi miundombinu elimu

NYUMBA za walimu wa shule za msingi zilizopo nchini ni 41,321 wakati mahitaji halisi ni nyumba ni 222,115, upungufu unaosababisha baadhi ya walimu kuishi mitaani katika nyumba za kupanga.

Serikali inaahidi kuendelea kujenga nyumba za walimu kadri fedha zinavyopatikana, lengo likiwa ni kuboresha mazingira na makazi kwa walimu.

Ndivyo alivyowahi kusema bungeni aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakati huo, Joseph Kakunda, alipokuwa akijibu maswali ya wabunge.

Anagusia kuwa ujenzi wa nyumba za walimu ni jukumu la wadau wote kuanzia serikali kuu, za mitaa na wananchi na akatoa wito wadau wengine kuchangia ujenzi huo.

Sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uhaba wa nyumba za walimu na ushiriki wa wadau katika kujenga nyumba hizo ni wa muhimu.

Juhudi zinazofanywa na serikali za punguza uhaba wa nyumba za walimu linahitaji kuungwa mkono ili walimu wapate makazi.

Upungufu unawalazimisha kupanga mitaani na kukutana na usumbufu ukiwamo wa kutishiwa maisha ambao wangeuepuka kama wangekuwa wanaishi katika nyumba zao.

Mchango wa wananchi ni muhimu kwani utasaidia kila mmoja kubeba sehemu ya ujenzi huo kuliko kuachia upande mmoja na mwisho wake ni kuendelea kuwa uhaba wa nyumba za walimu.

Wadau wa elimu wakishiriki kikamilifu watakuwa wamesaidia kupunguza uhaba huo wa nyumba za watumishi hao wa umma na pia kuwafanya wasitembee na kuchoka kabla hawajafika kazini.

Katika mazingira hayo ya kusafiri au kutembea umbali mrefu husababisha wanafunzi, kukosa msaada wa ziada kwa walimu wanapouhitaji baada ya muda wa masomo kwani kila mmoja anakimbilia kuwahi nyumbani na kuondoka mapema shuleni.

Hivyo ujenzi wa nyumba hizo ni jambo ambalo haliepukiki na linatakiwa kushirikisha wadau wengi hasa wazazi ili kutoa mchango wao katika kufanikisha ujenzi huo.

Kwa mfano wananchi wanaweza kushirikishwa kama nguvukazi wakisomba maji, mawe, kokoto, mchanga na sementi katika ujenzi wa nyumba hizo na kufanikisha jambo hilo.

Siyo hilo tu bali pia inaweza kuweka mipango wakachangia hata fedha kiasi kidogo katika ujenzi huo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali na kufanikisha ujenzi wa nyumba za walimu.

Ninasema hivyo, kwa sababu ipo mifano ya wananchi katika maeneo mbalimbali ambao sasa wanashiriki katika wa nyumba za walimu wakitoa nguvukazi yao na hata kuchangia chochote.

Mfano mmojawapo ni katika kata mbalimbali za Wilaya ya Musoma, kwa sasa wananchi wanashiriki ujenzi wa nyumba hizo ili kuwatoa walimu katika mazingira ya upangaji.

Hii ni hatua nzuri ya kusaidiana na serikali katika kuikabili changamoto hiyo ya muda mrefu inayoendelea kuwatesa walimu, lakini ninaamini ipo ndani ya uwezo wa jamii ya maeneo husika.

Kinachotakiwa ni kuhamasisha na kuelimisha jamii kutambua umuhimu wa kushiriki katika shughuli za ujenzi wa miundombinu ya elimu kama ambavyo inafanyika wilayani Musoma na maeneo mengine.

Kwa mfano katika Kata ya Bukumi, wakazi wa kijiji cha Buira, wanachanga Sh. 12,000 za nyumba ya walimu huku pia nguvukazi yao ikitumika kusomba mawe, maji, mchango na kufyatua matofaili ya nyumba hiyo.

Wao wameunga mkono juhudi za serikali ambayo imetoa Sh.milioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu wa Shule ya Msingi Buira ulisimama miaka 19 iliyopita.

Leo wanaendelea baada ya sababu za kitaalamu kupatiwa ufumbuzi ili kuhakikisha nyumba inakamilika, ambayo ina vyumba vitatu vya kulala, choo, bafu, stoo na jiko.

Iwapo ujenzi wa nyumba hiyo utakamilika utawapunguzia walimu gharama ya kupanga uraiani au mitaani na pia wakati mwingine inamfanya mwalimu aheshimike ndani ya jamii kuliko ilivyo sasa.

Kwa hiyo kila mmoja ana wajibu wa kushiriki kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na hasa kwenye ujenzi wa nyumba zao ambazo ni muhimu zijengwe kwa wingi nchini.