Wanaofyeka barabara  kama hawajali sheria

03Dec 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Wanaofyeka barabara  kama hawajali sheria

KUFAHAMU matumizi bora ya  barabara na sheria zake si jambo linalowahusu madereva wanaoendesha vyombo vya moto pekee  bali hata  wengine wote wanaotumia barabara hizo. Elimu hiyo itasaidia  kuepusha ajali nyingi ambazo zingeweza kuepukwa.

Watu wengi wanaotumia barabara wanafikiri wanaopaswa kuzingatia sheria za barabarani ni madereva wanaotumia vyombo vya moto pekee.

Matumizi ya barabara yanawahusu hata wanaofagia, wanaofyeka barabarani ili kila mtumiaji ajiweke katika hali salama ya kuepusha ajali kwake na kwa mwenzake.

Kumekuwa na tabia ya watu wanaopewa kazi ya kufyeka majani barabarani kutozingatia ni wakati gani anatakiwa aache kufyeka ili kuepusha madhara kwa wanaotumia barabara hizo.

Hali hiyo inatokea kutokana na wanaofanya kazi hiyo kutokuwa na elimu ya sheria za barabarani na hivyo kufanyakazi hiyo kiholela.

Mara nyingi watu wanaofyeka majani barabarani hawajali wanapoona magari au watu wanaopita na kuendelea kufyeka.

Madhara yanayosababishwa na ufyekaji wa aina hiyo ni pamoja na kuwajeruhi watu wengine wanaotumia barabara au kuleta athari kwenye magari kwa kuvunjwa vioo pale mafyekeo yanapochota mawe au vitu vingine vigumu kwa bahati mbaya.

Kuna baadhi wanaotambua sheria na wanapoona watu au magari yanapita, wanasimama kufyeka ili kuruhusu watu kupita ndipo waendelee.

Hata hivyo, kuna baadhi wanatambua, lakini kutokana na kutozingatia sheria hizo anaona aendelee kwa kuwa anajua hakuna sheria itakayombana.

Wadau wa matumizi ya barabara wamekuwa wakipiga kelele kuhusu sheria za barabarani kufanyiwa marekebisho ili watu wote waweze kuzifuata.

Kwa sheria iliyopo hakuna sehemu inayombana mtu wa aina hiyo kupewa adhabu pale anapofanya kosa la aina hiyo, matokeo yake aliyejeruhiwa au kuharibiwa mali yake anashindwa kumbana.

Watu wengi wamekuwa wakitumia barabara vibaya kwa kuwa sheria haziwabani, wakiwamo wanaofanya biashara kwenye vituo vya mabasi.

Watu hao hugeuza vituo hivyo kama mali yao hata wananchi wanapohitaji kujihifadhi kipindi cha mvua au jua, wanakosa nafasi kutokana na kuhodhiwa na wafanyabiashara hao.

Kwa upande wa wafagiaji wa barabara, wamekuwa waangalifu wanapofanyakazi kwa kuweka alama za kuashiria kazi inaendelea ili hata watu wengine waweze kuchukua tahadhari.

Umuhimu wa kufanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani, lazima utiliwe mkazo ili kuepusha ajali za kizembe.

Marekebisho hayo pia yatasaidia kuwabana watu wengine wanaotumia vibaya barabara kwa kutumia mwanya wa upungufu wa sheria.

Kuna tabia pia ya watu kutumia simu wakati wakiendesha magari hali inayosababisha wakati mwingine foleni isiyokuwa na sababu.

Dereva anaendesha gari huku akituma ujumbe kwenye simu na mwendo wa gari akiwa amepunguza na kusababisha magari mengine kupunguza mwendo.

Aidha, baadhi ya madereva hujisahau wakati wanapokuwa kwenye foleni kwa kuchati na simu zao na magari yanaporuhusiwa kutembea anaendelea kuwazuia wenzake kuondoka.

Simu zimekuwa chanzo kingine kinachosababisha ajali za kizembe kwa watu kujisahau kwa kuendesha huku wakiongea na simu.

Katika nchi zingine, sheria zinawabana watu wa aina hiyo na huchukuliwa hatua kali ili makosa hayo yasijirudie.

Tabia ya watu kuongea na simu huku wakiendesha vyombo vya moto imeshika kasi pia kwa madereva wa bodaboda pamoja na abiria wao.

Sheria ya Barabarani (Kifungu cha 168 R.E. ya 2002) imetunga Sheria za Barabara kama mwongozo rasmi wa namna ya kutumia barabara kiusalama na kwa ubora. Ni kwa ajili ya wale wote wanaosafiri barabarani, ikiwa ni pamoja na watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, waendesha pikipiki, na madereva.

Iwapo kila mmoja atafuata sheria kutakuwa na matukio machache ya kugongana na foleni.

Kanuni za Barabara ni mchanganyiko wa sheria na ushauri. Kanuni hizi ni tafsiri rahisi ya maelezo magumu ya Sheria za Barabarani na kanuni zinazohusiana nazo. Iwapo hazitafuatwa, mtu anavunja sheria, na kama atakamatwa na kutiwa hatiani atatozwa faini na kuzuiwa kuendesha.

[email protected]; Simu: 0774 466 571