Wanaohama wanaufahamu  mkataba na wapiga kura?

30Dec 2017
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Wanaohama wanaufahamu  mkataba na wapiga kura?

MWAKA 2017 ulikuwa na mengi, japo unapoondoka kuna machache tunayohitaji kuyatupia jicho pevu kwani ni dhahiri yameacha alama na maswali kwenye kumbukumbu za Watanzania.

Yapo mengi lakini mojawapo ni hili la baadhi ya wanasiasa hususan wabunge wanaohama vyama baada ya kukaa kwenye uwakilishi kwa miaka miwili, yaelekea huenda bado hawajafahamu msingi mkuu wa mkataba kati yao na wananchi au wapiga kura au ‘social contract’ kama wanavyounadi wanazuoni wa kada ya sheria na hata ile ya sayansi ya siasa.

 

Kimsingi, wabunge kama sehemu ya pili ya bunge, ambacho ni chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano, jukumu lao kubwa, kwa niaba ya wananchi, ni kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye Ibara ya 63 (2) - (3).

 

Na isitoshe, ibara ya 65 (1) – (2) ya katiba inaelekeza tena kuwa maisha ya kila bunge yatakuwa ni muda wa miaka mitano.

 

Yaani kuanzia tarehe ambayo bunge jipya limeitishwa kukutana kwa mara ya kwanza mara baada ya uchaguzi mkuu na kuishia tarehe ya kuvunjwa kwa bunge hilo kwa ajili ya kuwezesha uchaguzi mkuu mwingine wa kawaida kufanyika.

 

Msingi wa Dhamana ya Cheo cha Ubunge.

Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1)(a) na 73 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

 

Kila mbunge wa kuchaguliwa nchini, kazi yake kubwa ni kufanya uwakilishi wa wananchi wenzake bungeni kutoka katika majimbo ya uchaguzi kwa kipindi cha miaka mitano.

 

Hawa ndiyo watu wenyewe, hasa, kwa asilimia kubwa ndiyo hufanya au kusababisha Bunge la Jamhuri ya Muungano kuitwa bunge au muhimili wa dola.

 

Athari za kushindwa kuheshimu dhamana

Mbali na mlengwa wa kisiasa, katika fikra za mchumi yakinifu na makini hasa kwa taifa linalojinadi kuelekea uchumi wa viwanda, taathira yake ni mbaya japo kwa jicho la mashabiki, ambao kusema kweli kwao ni sawa na kusaliti, hili kwao siyo jambo rahisi hata hidogo kuliona au kulipazia sauti.

 

Gharama za uchaguzi hakuna asiyefahamu kuwa ni kubwa mno, tena hasa kwa chaguzi hizo za marudio bila ya sababu za msingi.

 

Na wanasiasa wote wanajua ni kwa jinsi gani fedha hizo zinaweza kutumika kusogeza gurudumu la uchumi mchanga wa Tanzania kufika mahala flani ili kusaidia kuondoa umaskini. Wanasiasa rejeeni ibara ya 9 (c) na (i) ya katiba.

 

USHAURI

Licha ya ukweli kuwa ibara za 20 (1) na 29 (1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 zinatoa haki kwa kila raia kujiunga na chama chochote kwa mlengwa wa kuhifadhi au kuendeleza maslahi binafsi au maslahi mengineyo yakiwamo na yale ya kisiasa. Bado hii pekee haitoshi kutoa mwanya kukinzana na ibara ya 30 (1) ya katiba hiyo hiyo.

 

Ibara hii inasema, haki na uhuru huo havitatumika na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.

 

Kimsingi, kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 29 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

 

Zaidi, watu wote, pamoja na viongozi wa kisiasa-wabunge , wanatakiwa na sheria kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa.

 

Kulingana na kile ambacho katiba na uchambuzi vinaonyesha haitokuwa haramu kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuja na ‘Sheria Maalum’ ambayo itakuwa na mlengwa wa kulinda maslahi ya taifa kwa ujumla dhidi ya ‘Matumizi Mabaya ya Rasilimali za Taifa’’ kama huu unaoonekana kujitokeza zaidi kwa mwaka huu wa 2017 - Ibara ya 30 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.  Watanzania tukumbuke, ‘’Uhuru bila ya mipaka ni sawa na utumwa huru-ambao ni hatari zaidi!’’

 

Inapoingia 2018 , Watanzania heshimu na kulinda katiba ambayo pekee ni sheria kuu inayotuletea wote ustawi na maendeleo.